Monday, January 27

“Ni vyema kuzitumia siku 16 kwa kujadili na kutafakari namna ya kuongeza juhudi katika mapambano ya ukatili wa kijisnia”-Bibi Jeanne  Clark

NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.

Wadau katika mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wametakiwa kuongeza juhudi katika kuvifichua vitendo hivyo ili viweze kuchukuliwa hatua na kukomeshwa kabisa ndani ya jamii.

Wito huo umetolea na Bibi Jeanne  Clark kutoka Ubalozi wa Marekani wakati alipokuwa akizungumza na wadau hao ikiwa ni pamoja na  wanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashkata , Maafisa wa Jinsia, wanaharakati kutoka Jumuiya ya Waandishi wa habari   Tanzania  Tamwa pamoja na wanafunzi kutoka Skuli za Madungu na Chuo cha Mwalim nyerere na Utumishi wa Umma  Kisiwani Pemba huko katika Ukumbi wa maktaba ya American Conner Chake Chake   ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Amesema Udhalilishaji una maana pana hivyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake na popote alipo  kuhakikisha anapinga aina zote za vitendo vya udhalilishaji ili jamii iweze kubaki  salama.

Kwa upande wao wadau hao wamesema  licha ya kwamba juhudi mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa katika kupambana na vitendo hivyo  bado elimu zaidi inahitajika  kwa jamii  ili   iweze kufahamu athari ya vitendo hivyo kijamii, kisiasa na kiutamaduni huku wakivitaka vyombo vya sheria kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.

Wamesema Vitendo vya Udhalilishaji vimekuwa vikifanyika kila sehemu  ndani ya jamii ikiwa ni ndani ya familia, maskulini, kwenye nyumba za ibada na hata kwenye sehemu za kazi hivyo  ni vyema kuzitumia siku 16 kwa kujadili na kutafakari namna ya kuongeza juhudi katika mapambano hao.

Siku  16 za kupinga ukatili na udhalilishaji zimekuwa zikiadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 November hadi tarhe 10 Disemba ya kila mwaka ulimwenguni kote.

MWISHO.