NA HAJI NASSOR, PEMBA
WATU wenye ulemavu kisiwani Pemba, wamesema bado wanamashaka na utekelezaji wa haki zao, ikiwemo ajira, miundombinu ya kuyafikia majengo ya umma na upatikanaji huduma za kijamii kwa ina ya mazingira yao.
Walisema, wamekuwa na watetezi wengi mno katika taifa, lakini kwenye utekezaji halisi, wanaendelea kukumbana na vikwazo, hali inayosababisha kuwavunja moyo, kwa baadhi ya wakati.
Hayo waliyasema Novemba 27, 2023 kwenye kongamano la siku moja, lililoandaliwa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ na kufanyika ofisi ya Umoja wa Watu Wenye Ulemavu ‘UWZ’ Mkanjuni, ikiwa ni muendelezo wa mikutano, ya ndani ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji.
Walisema, hadi miaka ya hivi karibuni, yapo majengo ya umma yanajengwa bila ya kuzingatia miundombuni yao, jambo linalowavunja moyo na kujiona wanatengwa.
Mjumbe wa ‘UWZ’ Nassor Suleiman, alisema wamekuwa wakijuliza kwamba sasa wafike pahala, wasizungumze jambo lolote wanapotakiwa kutaja changamoto zao, kwa kuhofia kutofanyiwa kazi.
‘’Kwa mfano hata ujenzi wa soko letu jipya la Machomanne Chake chake, kuna sehemu kubwa inavizingiti, na hili wakati linajengwa sheria yetu mpya imeshatungwa, sasa tunajiuliza mbona tunasahauliwa kutekelezewa maoni yetu,’’alieleza.
Mjumbe wa ‘UWZ’ wilaya ya Wete Katija Mbarouk Ali, alisema changamoto kubwa, ni kukosa uhakika wa kutekelezwa kwa vitendo, juu ya dhana ya ajira kwao wao.
‘’Tunasikia tu kwamba, watu wenye ulemavu wanatakiwa waajiriwe kwa asilimia kadhaa, lakini hatuoni jambo hilo, likitekelezwa kwa vitendo, na bahati nzuri sera na sheria zipo, sasa hapa hatujui tufanye nini,’’alilalamika.
Alieleza kuwa, changamoto nyingine ni kuweko kwa watendaji katika ofisi za umma za watu wenye ulemavu, wasiokuwa na ulemavu, jambo linalosababisha kukosekana kwa upokeaji mzuri.
Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar ‘JUWAUZA’, Hidaya Mjaka Ali, alisema katika eneo la mahkama bado watu wenye ulemavu na hasa viziwi, hawajatendewa haki.
‘’Hakuna mkalimani rasmi katika mahkama zetu, na wakati mwingine hutafutwa lakini hasa kwa kesi za udhalilishaji pekee, je hizi kesi nyingine haki ya watu kwa kundi hili inapatikanaje,’’alihoji.
Mwanachama wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu Pemba, Salim Abdalla Salim alisema, pamoja na juhudi za serikali za kutaka watu wenye ulemavu, wapatiwe haki zao, lakini wapo wanaokwamisha.
‘’Serikali imeweka mikakati na sera nzuri, kwa ajili yetu, lakini sasa inatakiwa kila jambo lisimamiwe kwa dhati, ili kuhakikisha tunapata haki zetu,’’alifafanua
Akizungumzia siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, alisema ni muhimu kwao, kutafakari namna wanavyopatiwa haki zao za binaadamu, ikiwemo kushirikishwa.
Mjumbe wa Jumuiya ya wasioona wilaya ya Mkoani ‘ZANAB’ Halima Suleiman Kombo, aliishauri Tume ya Utumishi serikalini, kuhakikisha wanaweka mifumo jumuishi, wanapotangaaza ajira kupitia mitandaoni.
‘’Kama dunia imefika mbali, wenye taasisi za kutoa ajira, watumie mifumo jumuishi, maana wako wananchi wanaulemavu wa uoni, sasa mifumo nayo isiwatenge,’’alifafanua.
Akifungua kongamano hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria Chake chake ‘CHAPO’ Kassim Ali Omar, alisema kongamo hilo, ni jukwaa kwa watu wenye ulemvu, kueleza changamoto zao.
‘’Watu wenye ulemavu wanachangamoto kadhaa, na ndio maana CHAPO, ikaamua kukutana na nyinyi, ili kuzitumia siku 16 hizi za kupinga ukatili na udhalilishaji,’’alieleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani Nassor Hakim Omar, alisema njia moja ya kupunguza changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu, ni kuzisemea kila wanapopata nafasi.
‘’Msikae kimnya kila mnapopata nafasi, changamoto zilizopo mzizungumze, na sisi wadau wa haki jinai, tunaendelea kushirikiana kila wakati, ili kuhakikisha tunafikia ndoto zetu,’’alieleza.
Mwakilishili wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete Said Hassan Rashid, alisema kama nchi haijakuwa na sera maalum na kutekelezwa, changamoto za watu wenye ulemavu zitazungumzwa bila ya kumalizika.
Mkurugenzi wa ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali aliwataka viongozi hao wa jumuiya za watu wenye ulemavu, kushirikiana na wasaidizi wa sheria, ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zao.
‘’Pamoja na changamoto hizo, lakini sihaba serikali imeweka miundombinu mizuri kwa ajili yenu, kama kuwepo wa Idara, mikopo na sheria nambari 8 ya mwaka 2022 iliyokuja kulinda haki zenu,’’alifafanua.
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake CHAPO, imo katika mikutano yake kadhaa, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji.
Mwisho