Friday, December 27

TRA, ZRA zatakiwa kufanya tafiti ili kuibua vyanzo vipya vya ukusanyaji kodi

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

NAIBU Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hamad Hassan Chande, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), kufanya utafiti wa kina kwa kuangalia vyanzo vipya vya mapato, ili viweze kutumika katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alisema kwa muda mrefu taasisi hizo zimekua zikitumia vyanzo vya mapato vilivyozoeleka, kitu ambacho wanapaswa kwa sasa kubuni vyanzo vipya ambavyo vitakua mbadala wa vyanzo vikongwe.

Naibu waziri Chande, aliyaeleza hayo katika kilele cha sherehe za wiki ya shukrani kwa mlipa kodi kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ilioambatana na kauli mbiu “Kodi Yetu, Maendeleo Yetu, Tuwajibike”, mkutano uliofanyika mjini Chake Chake.

Aidha alizisisitiza taasisi hizo kuhakikisha zinaimarisha mifumo yao ya ukusanaji wa kodi, ili wananchi wasiweze kupata usumbufu wakati wanapolipa kodi hizo.

“Lazima tuwe wa kweli katika suala zima la kodi, kwa muda mrefu tumekua na vyanzo ambavyo sasa vinatakiwa kubadilika na kua na vipya vya ukusanyaji wa kodi,”alisema.

Hata hivyo aliwataka watumishi wenzake kuhakikisha wanakusanya kodi kwa kufuata misingi ya upendo na uadilifu, ili wafanya biashara kuona kodi ni kitu cha kawaida.

“Kwenda kufunga duka la mtu hujaisaidia serikali, wala kumkomoa mtu bali unajikomoa wewe kwa kukosa kukusanya kodi, katika vyanzo vyako 10 basi kimoja umeshakipoteza na vitabakia tisa,”alisema.

Katika hatua nyengine Naibu Waziri Chande, aliwashauri watendaji wa TRA na ZRA, kuwa na ukaribu na wafanyabiashara ili kuweza kutimiza malengo ya serikali katika suala zima la ukusanyaji wa kodi.

Hata hivyo alisisitiza suala zima la utoaji wa risiti zakieletronik kwa wafanyabiashara wanapouza bidhaa zao, sambamba na wanunuzi kudai risiti za kieletronik.

Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema kitendo cha kulipa kodi ni kitendo cha kinidhamu, watahakikisha wanasimamia jukumu la wananchi kulipa kodi ili serikali iweze kutekeleza malengo yake.

Alisema uvukaji wa lengo la TRA ni kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa serikali za Mikoa, Wilaya na wananchi kuhamaisika ulipaji wa kodi kwa hiyari.

“Jukumu la kusimamia kodi ni TRA na ZRA lakini sisi ndio wasimamizi wakubwa wa kodi, kwani kodi ndio chanzo kikuu cha kuendesha nchi yoyote duniani,”alisema.

Hata hivyo Mkuu huyo aliwataka wasimamizi hao wa kodi kuacha tabia ya kutumia nguvu katika suala la ukusanyaji wa kodi, kwani kitendo hicho hakifai na wala hakikubaliki.

“TRA inapokwanza na mtu ambae hataki kulipa kodi wanakuja kwetu, haipendezi kufunga maduka kwani kufanya hivyo ni kupelekea kuwaonea wafanyabiashara, ukifunga duka ndio utapata hiyo kodi unayoitaka,”alisema.

Nae Naibu Kamishna TRA Zanzibar Saleh Haji Pandu, alisema kwa sasa suala la kodi wanatakiwa kulipa uzito wa hali ya juu, hivi sasa serikali imeingia katika mkakati wa kukifungua kisiwa cha Pemba kiuchumi, TRA imeweza kusogeza huduma kwa wingi ndani ya kisiwa hicho.

Alisema TRA imeshajiweka tayari kwa kuongeza wafanyakazi, ili kuweza kukava maeneo yote kwa ajili ya kukusanya kodi kwa maendeleo ya Zanzibar, pale wawekezaji watakapowekaza ndani ya kisiwa hicho.

Kwa upande wake Meneja TRA Pemba Arif Maohamed Said, aliwataka wafanyabiashara, taasisi kuhamasika kuendelea kulipa kodi kwa hiyari, kwani kodi hizo zinarudi kwa jamii katika kupatiwa maendeleo.

MWISHO