NA FATMA HAMAD, PEMBA
Septemba 21 mwaka huu Blog ya Pemba ya leo iliibua changamoto ya kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama katika kituo cha Afya cha Wesha wilaya ya Chake chake Pemba, ambapo kilio hicho kimepatiwa ufumbuzi kwa sasa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari huko kituo cha afya wesha Safinia Said na Rukia Khamis ambao ni wajawazito waliokwenda kupata huduma kituoni hapo walisema zaid ya miezi 3 kulikuwa hakuna maji kituoni hapo.
Walisema kwa sasa shida ya maji imepungua kwani maji yanapatikana ijapokuwa hayatoki siku zote ni kwa mgao.
”kwa sasa hatuendi na madumu ya maji tunapokwenda kujifungua kwani maji ya zawa ikifika zamu ya kutoka huwa yanapatikana hapa kituoni,, walisema
Hivyo tunaiomba Wizara ya Maji iyongeze juhudi ili kuona maji yanapatikana masa yote 24 kwani suala la uzazi ni kitu cha kila siku jambo ambalo litaondosha usumbufu kwa mama wajawazito pamoja na wazazi wanaokwenda kujifungulia kituoni hapo.
Kwa upande wake Yusra Amour Juma aliejifungulia kituoni hapo alisema alihudumiwa vizuri na hakupata shida iyoyote kwani maji yalikuwa yanatoka kwa wingi kwa siku hiyo aliyokwenda kujifungua.
”Nashukuru nilipokwenda kujifungua sjakwenda na dumu langu la maji, kwani ilikua hapo kituoni yanatoka, alieleza.
Ali Juma Na Haji Khamis walisema kipindi cha nyuma wakilazimika kuchukuwa maji yao wakati wanapokwenda kuwapeleka wake zao kujifungua, ila kwa sasa tatizo hilo limeondoka.
Daktari mkuu wa kituo cha Afya cha Wesha Abdulnassir Hemed Said alisema wanategema maji kutoka Mamlaka ya maji Zawa, hivyo siku wakiyatoa na Hospitalini yanafika ile changamoto kubwa kwa sasa imepungua.
Alisema kwa kipindi hiki maji yanatoka, licha ya kuwa hayatoki siku zote bali yanatoka kwa mgao.
”Licha ya changamoto ya Maji kuwa haijaondoka moja kwa moja lakini imepungua, Kwani kwa sasa hivi ndani ya wiki moja tunapata maji siku mbili au tatu, hiyo ni afadhali, alisema.
Alisema changamoto inayowakabili kwa sasa kituoni hapo ni kukosekana kwa Tenki la kuhifadhia maji.
”Tenki tunalotumia ni dogo, ni la lita 2000 na pia linavujisha Maji hayakai, alieleza.
Hivyo ameomba kupatiwa tenki lenye ujazo wa kilomita 5000 ili maji yaweze kufika angalau kwa siku tatu, jambo ambalo litaondosha moja kwa moja tatizo hilo kituoni hapo hususan kwa vile hayatoki siku zote.
Alieleza kwa mwezi wamekuwa wakizalisha wajawazito kati ya 12 hadi 14, ambapo idadi imeongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambacho maji yalikuwa hayapatikani moja kwa moja.
Akitaja sababu inayopelekea kuwepo kwa mgao wa maji Afisa uhusiano wa mamlaka ya Maji Zanzibar Zawa Ofisi ya Pemba Suleiman Anass Masoud alisema ni ungaji wa maji kiholela kwa wananchi katika laini za kusambazia maji.
Alieleza kuwa tayari mafundi wao wako katika hatua za mwisho kufanya ukarabati katika sehemu zilizo haribika, hivyo wananchi wakae tayari kwani muda wowote shida hiyo itamalizika.
Nae Afisa mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali ameupongeza uongozi wa wizara ya maji kwa jitihada walioifanya ya kuhakikisha maji yanapatikana kituoni hapo, jambo ambalo litapunguza changamoto za Wauguzi, wajawazito pamoja na wazazi wanaojifungulia kituoni hapo.
Sera ya Wizara ya Afya ya Zanzibar ya mwaka 1990 ni kuhakikisha inaimarisha huduma ya afya ya mama na mtoto, ili kupunguza Vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vya watoto wachanga.
Sekta ya maji inakubwa na ongezeko la mahitaji ya maji kunakochochewa na ongezeko la idadi ya watu, Uvamizi wa vianzio vya maji pamoja na mwitikio mdogo wa wananchi kuchangia huduma ya maji.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Umoja wa Mataifa [UN] ya machi 22/2023 inasema duniani kote watu Bilioni mbili hawana huduma ya maji safi ya kunywa, na Bilioni 3.6 wanakosa huduma za usafi zinazosimamiwa kwa usala.
MWISHO.