Na Maryam Talib – Pemba.
MKUU wa Mkoa Kusini Pemba Matar Zahor Masoud amewataka Wakandarasi wa Uwanja wa Mpira Gombani waendelee kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuendana na muda waliopangiana kumalizia ukarabati huo.
Mkuu huo wa Mkoa aliyasema hayo alipokuwa akifanya ziara ya ukaguzi wa ukarabati wa uwanja huo wa Gombani uliopo Mkoa wa Kusini Pemba Wilaya ya Chake Chake .
Amesema kazi iliyofanywa na wakandarasi hao ni kubwa lakini bado inahitajika juhudi za ziada kuweza kuukamilisha kwa wakati na kuweza kuutumiwa kwa sherehe za Mapinduzi kama ilivyokusudiwa.
“Kwenye hili naomba wakandarasi muwe wakweli tujue kitu cha kushika mana tarehe tulizokusudia kuzindua haziko mbali’ alisema Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo aliutaka uongozi wa Wizara ya Habari na wakandarasi kusimamia vyema ukarabati wa uwanja huo kwani isingependeza kuona uwanja wa Amani unazinduliwa kwa tarehe iliopangwa ukashindwa wa Pemba wakati uwanja wa Amani umekuwa na matengenezo makubwa zaidi kuliko wa Pemba.
Alisema ipo haja ya kuhimizana na kuendana na wakati kwenye miradi kwa mujibu ilivopangiwa kwani kumesitishwa mambo mengi ya kimaendeleo na kupishwa ukarabati wa Uwanja huo.
Nae Enginear wa Company ya Diamond Builder wa Uwanja huo Ismail Moh’d Ismail alisema wanaendelea kufanya vikao vya huduma za kumalizia ukarabati huo wakiamini watakabidhi kwa tarehe waliokubaliana.
Nae Afisa MdhaminI Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau alisema wameyapokea vyema maoni ya Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuyachukua kwa uzito wake na kuyafanyia kazi kwa wakati uliokusudiwa.
MWISHO