NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
SHIRIKA la Umeme Zanzibar(ZECO) limewataka wananchi wa Kisiwa panza Wilaya ya Mkoani Pemba, kutoa taarifa kila wanapoona kuna dalili za uharibifu wa miundombinu ya Umeme, inayofanywa kwa makusudi au kutokea hitilafu mabali mbali, ili shirika liweze kuchukua hatua ya kurekebisha.
Akizungumza na wananchi wa Kisiwa hicho, katika mkutano maalum ulioandaliwa na ZECO kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi, juu matumizi ya umeme huko katika skuli ya Kisiwa panza.
Afisa wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ZECO Pemba Haji Khatib, aliesema kukaa kimya bila kutoa taarifa kunaweza kupelekea kutokea kwa athari mbali mbali ikiwemo kukosekana kwa huduma.
Alisema miongoni mwa mambo yanayopelekea uharibifu wa miundombinu ya umeme, ni pamoja na kuacha majani ya miti kufikia transfoma au waya za line kubwa, harakati za kuchimba mchanga au mashimo karibu na miundombinu kwa shughuli za kijamii ikiwemo kilimo na ujenzi.
“Kumekua na tabia kwa baadhi ya wananchi kuchimba mchanga au kuchoma moto majani karibu na nguzo za umeme, kitu ambacho kinaweza kusababisha hatari,”alisema.
Alisema mengine ni kukata miti na kuangukia katika nyaya za umeme, badala ya mtu kukata huamua kukaa kimya bila ya kutoa taarifa kwa shirika, hadi taarifa kama hizo kufika shirika tayari athari ishakua kubwa.
Aidha alizitaja athari zinazoweza kupatikana kutokana na uharibifu wa miundombinu ni pamoja na kukosekana kwa huduma, hatari za kuunguwa kwa vifaa vinavyotumia umeme na hata vifoo, hivyo aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo na kutoa taarifa kwani wao ndiyo wanaokaa katika jamii.
Kwa upande wake Afisa kutoka ZECO Ali Faki Ali, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa kutumia huduma za umeme hasa pale wanapotumia vifaa kama pasi, makuka, mafriji na vyenginevyo kwa ili kuweza kuwa salama katika matumizi yao na kuepusha athari.
Aidha aliwataka wanaotumia kuka wahakikishe wanatumia vitambaa vikavu, kuvaa viatu kutokana na kuka kuwa na unyevu unyevu wanapoweka sufuria jikoni, vyenginevyo kunaweza kuwapatia shida huku akiwataka watumiaji wa pasi kuacha kugusa kwa mkono wakati wa kuagalia moto.
Naye Afisa Huduma kwa wateja katika shirika la Umeme Pemba Ali Faki Omar, aliwataka wananchi wa Kisiwa panza kujisajili na kuunganishiwa umeme katika shirika hilo, kwani idadi ya wananchi waliounga umeme kisiwani humo ni ndogo ikilinganishwa na visiwa vyengine vidogo vilivyopo Pemba.
Nae Haji Makame Yussuf mkaazi wa Kisiwa hicho, aliliomba shirika hilo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi na utunzaji wa miundombinu, kwani badi wananchi wengi hawajawa na uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya umeme jambo ambalo hupelekea kufanya mambo yanayoweza kuwapelekea hatari.
Hata hivyo Moh`d Jabiri ambaye pia ni mkaanzi wa kisiwa hicho aliliomba shirika la umeme kuangalia uwezekana wa kuwa na vifaa vya umeme kwa ajili ya wananchi
MWISHO