NA, AMINA AHMED MOH’D-PEMBA.
ZAITUNI Abdulkarim Njovu ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Zaina Foundation inayotetea haki ya kutumia mitandao ya kijamii kwa wanawake Tanzania.
Taasisi hiyo ambayo makao makuu yake makuu yake ni Dar es Salam ilianza harakati hizo mwaka 2017 na kufika Zanzibar mwaka 2022.
Zaituni alisema walifikia uamzi wa kuwa na hio taasisi baada ya kugundua kuwepo changamoto nyingi, ikiwemo ya ukatili wa kijinsia mtandaoni.
Vile vile zipo changamoto za kiuchumi, kiwango cha chini cha elimu ya matumizi sahihi ya mtandao na wanawake kidogo kutumia haki hiyo .
Vile vile sheria sio rafiki kwa mwanamke kukingwa anapofanyiwa udhalilishaji mtadaoni.
Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi za mwaka 2022 Tanzania inayo wanawake 31,6899( asilimia 51) na wanaume ni 30,530,130 (asilimia 49).
Kwa hali ilivyo sasa wanawake, kutokana na kuhofia usumbufu wa udhalilishaji wanashindwa kufikia malengo yao.
Kwa bahati mbaya wanakosa ulinzi na kupelekea kupata usumbufu, vitisho, kukerwa, kuvunjiwa heshima na hata udhalilishaji wa kimwili.
Hali hii ndio iliopelekea wanawake wengi kukaa pembeni na matumizi ya kidigitali .
“Tulianzisha taasisi kwa lengo la kushirikiana na serikali katika kusaidia kutatua changamoto zinazomzuia mwanamke kutotumia ipasavyo digitali’’, alisema Zaituni.
Kabla ya kuamzisha taasisi hii ni wanawake wachache ambao walikuwa wanatambua haki yao ya kutumia ipasavyo mfumo huu.
“Ushiriki wa wanawake umeongezeka na ule woga wa kutumia mitandao ya kijamii umepungua, tofauti na miaka ya nyuma’’, alisema Zaituni.
Awali walikuwa wanafanya kazi Tanzania Bara tu na kufka kwao Zanzibar kumesaidia pia kuwaelesha wanawake wa Visiwani juu ya haki hii.
Alisema asilimia 80 ya malengo yaliokusudiwa na taasisi yamefikiwa na wanafurahia kuwa na mchango mkubwa katika kutungwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa za Mtu ya mwaka 2022 ( The Personal Data Protection Act 2022).
Marekebisho yaliofanywa katika baadhi ya sheria zinazohusu masuala ya digitali kuanzia mwaka 2018 nayo pia ni mafanikio ya taasisi hiyo .
“Licha ya kuwa na mapungufu madogo madogo, tunaamini tmepata mafanikio ambayo taasisi yetu imeyasimamia na kuwasaidia wanawake kutumia haki zao za kidigitali zikiwa rafiki zaidi kwa mwanamke’’. aliongeza.
Aidha elimu juu ya kujua haki za kidigitali kwa wanawake imeongezeka na jumla ya wanawake 4300 kutoka makundi mbali mbali.
Miongoni mwa waliopata elimu hii ni wanawake wanasheria,wanasiasa, wanafunzi wa vyuo vikuu skuli za msingi pamoja na waandishi wa habari.
CHANGAMOTO KWA WANAWAKE
Zaituni anaona bado kuna uhitaji mkubwa kwa wanawake kuweza kuzitambua na kutumia ipasavyo haki zao za kidigitali, hususani Zanzibar.
Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi yao na hivi sasa wanatafuta rasilimali kutekeleza malengo waliyojipangia.
Hatahivyo, licha ya juhudi wanazofanya mapokezi kwa kwa baadhi ya wanawake bado sio ya kuridhisha na sheria licha ya kufanyiwa marekebisho bado ina dosari.
Kwahivyo, sheria zinahitajika marekebisho zaidi ili kumlinda na kumpa nguvu mwanamke katika matumizi ya mtandao ili kwenda sawia na wanaume katika matumizi.
UFUMBUZI WA CHANGAMOTO
Miongoni mwa mikakati endelevu ya Zaina Foundation ni kuendelea kushirikiana na wanawake katika kutumia fursa na haki yao ya kidigitali ili wanufaike kwa kujikomboa kiuchumi.
Hii itakwenda sambamba na kuongeza ushawishi kwa wanawake kutoa taarifa endapo watafanyiwa ukatili wakati wakitumia haki ya kidigitali.
WANAWAKE WALIOFIKIWA NA ZAITUNI WASEMAJE.
Riziki Abdalla Ali ,mwandishi wa Uga Media aambaye ni mmoja wa watu waliopata mafunzo ya haki za kidigitali alikiri kuwa alikuwa hajuwi umuhimu wa kuweka Nywila (neno la siri) katika vifaa vyake vya matumizi, lakini kwa. sasa imekuwa miongoni mwa vipaumbele vyake.
‘’Nilikuwa nafuata tu mkumbo wa wasap bila ya kuelewa kwa undani njia nzuri ya kutumia “, alisema Amina Omar.
Alisema mafnzo yamempa uelewa mpana wa matumizi ya mtandao kwa njia salama.
Khadija Rashid Nassor ambae ni mwandishi wa habari kutoka radio jamii Mkoani alisema mafunzo yamempa yeye na vijana wenzake uelewa mzuri wa kutumia mtandao kwa njia yenye tija.
Asia Mwalim, mwandishi wa kujitegemea wa gazeti la Zanzibar leo alisema mafunzo yamemsaidia kujikomboa kiuchumi kwa kumuonyesha njia rahisi za kutumia mitandao katika kazi yake ya habari .
Lailat Ali Msabah ambaye ni mwandishi wa habari wa Jicho Letu Tv, Pemba, alisema ukosefu wa elimu ni kikwazo kinachopelekea baadhi ya vijana kukosa uhuru wa kuendesha shughuli zake za kihabari mtandaoni.
‘’Ukosefu wa kukosa utaalamu wa masuala ya mitandao ni moja ya sababu iliyopelekea kuchelewa kufika mbali kwa Tv yake hiyo ya mtandaoni na kukosa kujiendeleza kiuchumi’’, aliseleza.
Fatma Abrahman,wa Jifunzee in advance online TV, alisema alichokuwa anafanya ni kusambaza habari zake, lakini hakuwa na uwezo wa kujilinda na hii ilipelekea kubadilisha akaunti ta kijiditali zaidi ya mara 10.
” Licha ya kuisajili blogi yangu, lakini sina utaalamu wa kuitengeneza na hii kuifanya kutokuwa rasmi na ya kuvutia kama za watu wengine’’. alisema Fatma Hamad, Mwandishi wa blogi ya Pemba ya Leo.
Alisema palikuwepo dhana potofu ya kuwa matumizi ya mitandao ni kwajili ya wanaume peke yao na kwamba haupo uhuru wa kufanya hivyo kwa wanawake.
‘’Mimi ni mtumiaji mzuri wa mitandao, lakini usumbufu ni mkubwa na wanaume wananisumbua sana na wengine wananitukana bila ya sababu’’, alisema Raiffa Abdalla Makame, mwandishi na mshereheshaji kupitia mtandao wa Instagram.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA ya mwezi Oktoba mwaka jana idadi ya watumiaji wa huduma za intaneti imeongezeka kutoka 29,169, 958 katika mwezi Juni, 2022 hadi kufikia 31,112,163 Septemba mwaka huo.
Idadi hiyo ni ya watumiaji wa kidigitali katika mitandao ya kijamii ya Facebook Tweeter, Insatgram, whatsApp na Youtube.
Mgawanyiko ni aasilimia 46 ya wa wanawake, na 54% ni wanaume.
Utafiti huo ni kwa mujibu wa taasisi ya Women at Web Tanzania ulioitwa Tathmini ya Unyanyasaji wa Kijinsia Mtandaoni uluofanywa mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka 2022 umeonesha asilimia 77 ya wanawake wameacha kutumia baadhi ya mitandao ya kijamii yenye tija kuendesha shughuli zao ambao umefanywa kwa baadhi ya wanawake ambao ni wanasiasa.
Hii imetokana na kutaka kuziepuka changamoto ziliopo mtandaoni ambapo ni wanawake 394 kutoka maeneo mbali mbali walifikiwa na kutoa majibu sawa katika utafiti huo.
Utafiti pia umeonyesha wanawake hao huishia kutumia zaidi mtandao mmoja tu wa WhasApp ambao hauna usmbufu kama mitandao mengine yenye tija.
Mwisho