Sunday, November 24

Zawadi: Mwakilishi wa Konde anaepambania kuzitatua changamoto za wananchi.

‘Asema, watu wayasemee mazuri anayoyatekeleza sio kumbeza’

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

“NIMECHIMBA visima nane katika Jimbo langu, visima sita ni vipya na viwili vilikuwepo zamani lakini vilikuwa havitumiki tena kutokana na uchakavu,” si maneno ya mtu mwengine bali ni ya mwakilishi wa Jimbo la Konde Zawadi Amour Nassor.

Zawadi ni mwanamke anaepambania kuzimaliza changamoto ndani ya jimbo lake ambazo zilikuwa zikimkosesha usingizi kabla ya kuwa kiongozi.

Mama huo wa makamo anaendelea kutimiza malengo yake aliyojiwekea baada ya kuingia kwenye chombo cha kutoa maamuzi, ambayo ni ndoto yake ya muda mrefu.

Katika kipindi hiki cha muda mfupi cha uongozi wake, amefanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima, hali ambayo imewapunguzia usumbufu wananchi hasa wanawake na watoto ambao ndio wahanga wakubwa.

Mwakilishi huyo anasema, upatikanaji wa maji katika jimbo lake ulikuwa ni wa kusuasua kiasi ambacho watu hutumia muda mrefu kutafuta huduma hiyo na kushindwa kufanya shughuli nyengine za maendeleo.

“Lakini sasa wananchi wa jimbo langu wanafaidika na huduma ya maji safi na salama kwani, kwa upande wa tatizo hilo nimelitatua kwa asilimia kubwa, kwa kweli najivunia,” anasema huku akitabasamu.

Kwa vile alizaliwa na kukulia katika jimbo hilo, alikuwa anaona changamoto zote zinazowakabili wananchi ingawa hakuwa na uwezo wa kutatua, lakini baada ya kuwa kiongozi ametafuta njia ya kuzitatua.

Mafanikio anayoyapata kwenye kutekeleza shughuli zake ni kwamba, anashirikiana na wananchi wake katika kuibua changamoto, kuzisemea na kuzipatia ufumbuzi.

Zawadi alifanya juhudi mbali mbali kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama ambapo alizungumza na wahisani na hatimae kupata fedha zilizomsaidia kutatua changamoto hiyo, ambayo kwa sasa imekuwa historia.

“Kabla ya kuwa mwakilishi nilikuwa Katibu wa Jumuia ya Elimu na Maadili Konde ambayo ilishughulika na maswala ya Dini, Tahfidhil-Quran, mayatima, mihadhara, hivyo wahisani hao walikuwa wanaelewa harakati zangu na mmoja miongoni mwao alinishawishi nigombee,” anahadithia.

Alipofanikiwa kupata nafasi ya uwakilishi mwanamama huyo,  aliahidiwa na muhisani huyo kumsaidia kwa hali na mali katika kutekeleza majukumu hasa kwa vile alizijua juhudi zake mapema na uaminifu alionao.

Na hakurudi nyuma muhisani huyo na alitekeleza ahadi zake za kumsaidia mwakilishi huyo na miongoni mwa mambo aliyomsaidia ni uchimbaji huo wa visima.

Kabla ya kuchimbwa visima hivyo, wananchi walikuwa wanatumia maji ya mito, maziwa na visima visivyofunikwa, hali ambayo ilihatarisha maisha yao kwani maji yale hayakuwa salama kwa matumizi.

Amekuwa akikutana na wananchi kila anapofika kisiwani Pemba, kwani kwa sasa muda wake mrefu anautumia Unguja ambako ndio sehemu yao ya kazi.

 

Changamoto zote zilizopo kwenye jimbo lake huzitetea katika Baraza la Wawakilishi na baadae kupata baraka, ambapo hutumia mfuko wa jimbo kutatua ama wahisani na wakati mwengine hutumia fedha zake mfukoni, lengo ni kuisaidia jamii.

 

Visima saba vimegharimu shilingi milioni 14 kwa kila kimoja na kisima kimoja kimegharimu shilingi milioni 21 kutokana na kuwa ni kikubwa na kinatoa huduma kwa vijiji vingi.

 

” Visima vyote nane vimegharimu shilingi milioni 119,000,000,  nawashukuru sana wahisani, Serikali na wananchi wangu kwa kuniunga mkono katika kuyatekeleza haya,” anaelezea mwakilishi huyo.

 

Shehia ya Kifundi alichimba visima viwili, shehia ya Msuka Magharibi visima viwili, shehia ya Msuka Mashariki visima viwili, shehia ya Tondooni kimoja na shehia ya Kiuyu kwa Manda kisima kimoja ambacho ndicho kilichogharimu shilingi milioni 21.

 

HARAKATI ZAKE ZA KUSAKA UONGOZI.

 

Alikuwa mwalimu wa skuli ya Makangale na alifundisha kwa muda wa miaka tisa, ambapo kipindi hicho Wizara ya Kilimo ilifikisha mradi wa vijiji 12 vilivyozunguka msitu wa Ngezi ndani yake ukawemo mradi wa kuwawezesha wanawake.

Kwa vile alikuwa mwalimu, mradi ulimchagua kuwa Afisa Ufuatiliaji kwa sababu alikuwa anavijua vyema vijiji vilivyozunguka msitu huo.

Ulimjengea uwezo mkubwa ambapo alizijua jamii kiundani na kugundua kuwa wanakabiliwa na matatizo mbali mbali, huku wanawake na watoto wakiwa wahanga wakubwa.

Hiyo ilimpa hamasa ya kuongeza elimu yake ya chuo aweze kufika mbali, ili siku moja aweze kusimama kutetea haki za wananchi ambazo wanastahiki kuzipata.

“Mwaka 2007 nilipata kuingia kwenye mradi wa kupambana na udhalilishaji ambao uliosimamiwa na TAMWA, hivyo katika harakati zile pia nilipata uzoefu, vile vile nilipata kujifunza sheria kwenye kituo cha huduma za sheria kama Msaidizi wa sheria,” anafafanua.

Alianza kuona faida pale alipochaguliwa kuwa Msaidizi mwalimu mkuu, hivyo alipata nafasi zaidi ya kuripoti matukio ya udhalilishaji mara kwa mara na ndipo akaona kwamba, kumbe kuna haja zaidi ya kuisaidia jamii yake.

“Kwa mbaali kwenye hisia zangu zikaja chembe za siasa mwaka 2018, nikajisemea kwani nikitoka nikienda kujitangaza nitapewa nafasi hii? nianzeje, nipite wapi kwani mimi ni mwanamke, sina pesa, nasikia udhalilishaji ni mwingi,” alijuliza maswali mengi.

Alimfuata mzee mmoja kupata ushauri lakini alimuangusha na alipoona ameng’ang’ania alimwambia agombee viti maalumu, ingawa hakuridhika na ndipo alipoamua kumfuata mzee mwengine na kumshauri kwamba, akiwa tayari akachukue fomu agombee.

Ilipofika muda aliingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea na hatimae aliibuka mshindi, ambapo ametimiza azma yake na sasa anatatua changamoto ndani ya jamii kwa kushirikiana na wananchi wake.

Anasema kuwa, tamaa ya kupata ilikuwa ni kwa asilimia ndogo kutokana na watu kumdharau na kummbeza, lakini alishindana na watu 11 na hatimae jina lake likarudi na kuendelea kuingia katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 kugombea nafasi hiyo.

CHANGAMOTO ZINAZOMKABILI KWA SASA

Wawakilishi wanatakiwa kutekeleza masuala yaliyomo kwenye jamii yake, ingawa jambo la kusikitisha ni kuwa wananchi hawajui hilo, bali wanahitaji wasaidiwe mmoja mmoja, jambo ambalo ni kikwazo.

“Baadhi ya wanajamii wana uwelewa mdogo kuhusu dhana ya mwakilishi au mbunge, kwa sababu wanataka tuwasaidie labda umpe mtu pesa au vyakula nyumbani kwake, ingekuwa wanajua majukumu yetu, basi kusengekuwa na malalamiko kwani changamoto za jamii tunazitatua,” anafafanua.

Pia anafahamisha kuwa, muda wake mkubwa anakuwepo kisiwa cha Unguja kikazi, kwa sababu kwenda barazani ni kama kwenda kazini kwa taasisi nyengine, ingawa jamii inahisi umewakimbia jimboni kwako na kuhamia kwengine.

Bado kwenye jamii kuna changamoto ya kuwavunja moyo na kukuharibia viongozi wanawake, ingawa haiathiri sana kwani yeye anasimamia majukumu yake katika kuhakikisha anafanikiwa lengo lake la kuihudumi jamii.

“Mazuri yaliyofanywa hayasemwi hata kama wanayaona, hivyo hutumia mwanya huo kutuchafua na hiyo inatokezea hata kwa wananchi wa chama chako, jambo ambalo sio zuri,” anaeleza.

Mume wa mwakilishi huyo anasema, mke wake anamuunga mkono katika kila hatua aliyokuwa akipitia na ndio maana ameweza kufanikiwa.

“Mimi ilikuwa sisikilizi maneno ya watu, ilikuwa naangalia mke wangu anataka nini na malengo yake ni yepi, hivyo nilimpa moyo na kushirikiana nae, akawa jasiri kugombea na hatimae amefanikiwa,” anasema.

Aliwashauri wanaume wenzake, wasiwawekee vikwazo wake zao wanapokuwa na nia ya kugombea uongozi, kwani ni waaminifu, hivyo ni rahisi kuyatekeleza yale waliyoyaahidi.

WANANCHI

Zainab Hamad Juma mkaazi wa Ungi Msuka anasema, siku zote mwanamke anapoongoza sehemu mambo mengi hunyooka na ndio maana katika jimbo lao wamejengewa visima vingi kwa wakati mmoja.

“Kuna viongozi hukaa majimboni miaka mitano mpaka kumi lakini huoni alichokifanya, lakini mwakilishi wetu huyu anajitahidi kupigania kila pahala kuhakikisha tunapata maendeleo,” anasema mama huyo.

Kombo Khamis mkaazi wa Kiuyu kwa Manda yeye anasema, kutokana na mafanikio aliyoyaona kipindi hiki cha uongozi wa mwakilishi huyo, ameamini kuwa wanawake wanaweza kuleta mabadiliko kwa muda mfupi sana.

ASASI ZA KIRAIA 

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wana mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.

“Na tumeona kwamba wanawake wengi waligombea katika chaguzi zilizopita, walionesha moyo mzuri wa kugombea na hii tunataka tuione mwaka 2025 wagombee wengi zaidi, ili tufikie 50 kwa 50 kwenye vyombo vya kutoa maamuzi,” anaeleza.

Kwa Pemba, TAMWA imeshawapatia mafunzo wanawake 70 wenye nia ya kugombea na wamewaunganisha na wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbaliakuwatoahofuhiyokwasasawaashiikia.

Mkuugezi wa PEGAO Pemba Hafidh Abdi Said anaeleza, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi za uongozi, wanaonekana juhudi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu yao.

Anasema, hatua hiyo inaoesha wazi kuwa viogozi wanawake wana uwezo wa kulefikisha maendeleo endelevu katika jamii hivyo wananchi waendelee kuwaunga mkono katika kuwachagua.

Mwaka 2020 wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi ni 29 kati ya 75 ya wawakilishi wote huku wanaume wakiwa 46.

Ambapo wanawake waliogombea ni 61 na walioshinda ni nane (8), huku wanaume waliogombea wakiwa 190 na walioshinda ni 42

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, wanawake walioingia Baraza la Wawakilishi mwaka 2015 ni 28 sawa na asilimia 36, kati ya wawakilishi wote 84.

Serikali, kwa kutambua umuhimu wa mwanamke, Sera na Sheria mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi.

Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke na taifa lake.

Katiba ya Zanzibar mwaka 1964 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 imeeleza wazi katika kifungu nambari 67 (1) kuwa, kutakuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia 40 ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.

MWISHO.