Thursday, January 16

DC Chake ahimiza Amani amesema maendeleo yoyote duniani hayawezi kufanyika pasi nakuwepo na amani.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema maendeleo yoyote duniani hayawezi kufanyika pasi nakuwepo na amani ndani ya mataifa hayo. 

Alisema vipo vichochoea vikubwa katika mataifa licha ya kuwa na uwezo mkubwa wakifedha, wataalamu lakini pasi na kuwa na amani katika mataifa hayo maendeleo kwao ni kikomo.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa amani uliowashirikisha wanawake kutoka makundi mbali mbali, watu wa ustawi wa jamii, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa wanawake na amani, unaotekelezwa na kituo cha majadiliano kwa vijana Zanzibar (CYD) kwa ufadhili wa shirika la WIIS-Kenya kwa kushirikiana na USIP na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema pasi na amani maendeleo ni shida kupatikana, yapo mataifa yalikuwa na amani na maendeleo makubwa baadae, amani yao wakaichezea kwa kuitia mikono na kuiharibu sasa hivi mataifa hayo yamekua ni dhalili kabisa.

“Tunapaswa kutambua kuwa amani ndio kitu cha kwanza katika sehemu yoyote ile, kwani misingi bora ya maendeleo inaanzia hapo, CYD imekua mstari wa mbele kuhamaisha amani kwa wanawake,”alisema.

Alisema pamoja na amani iliyopo saivi kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, ikiwemo uvutaji wa madawa ya kulevya watumiaji ni vijana, udhalilishaji wa wanawake na Watoto, hivyo ni jukumu la akinamama kutoa taarifa pale wanapoona bishara ya uzaji wa madawa hayo.

“wanawake wananafasi kubwa kupambana na masuala ya udhalilishaji ikizingatiwa wanawake wapo majumbani muda mwingi, lazima kufuatilia mienendo wa Watoto yao, sehemu anazocheza na makundi ya rafiki zake,”alisema.

Mapema Mratibu wa CYD Pemba Ali Shaban, alisema malengo ya mradi ni kuongeza uwezo kwa jamii hasa wanawake, ili zaidi na wao waweze kujielekeza na kusaidia katika suala zima la kutunza amani, kwani suala la amani ni mtambuka linahitaji wanajamii wote.

Alisema kwa muda mrefu sana wanaume walikua wanasimama mbele katika masuala yote yanayohusu amani, na wanawake wakawa wamewekwa nyuma, sasa umeonekana upo umuhimu mkubwa kwa wanawake kupatiwa elimu ya kutosha juu ya suala zima la amani.

“Wanawake muda mwingi wapo majumbani au mitaanai, wanaume wanakwenda kwenye mihangaiko yao, sasa hapa ndio nafasi yake mwanamke kujua viashiria vyote vya uvunjifu wa amani ili aweze kutoa taarifa kwenye mamlaka husika,”alisema.

Aidha alisema mwanamke anaweza kujua mabadiliko ya vijana na kuona hicho kinaweza kupelekea kua kiashiria cha uvunjifu wa amani, tayari lipo wimbi kubwa la vijana wameanza kutoweka na kwenda kusiko julikana.

Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Hashim Ali Hashim, alisema wamelazimika kutoa elimu ya amani kwa sababu, wanawake ni sehemu ya walezi wa familia inayowazunguka na kuona matokeo ya haraka ya suala zima ya amani.

Alisema wanawake ni watu wenye uwezo wa kushawishi jamii na kupelekea maoni kwenye jamii na mabadiliko kupatikina, huku akiwataka Wanawake kuweka mkazo katika malezi ya familia zao.

“Uvunjifu wa amani unaanza kwenye familia na vijana wakiwa wadogo, wanawake ndio wanaokaa Zaidi na familia wakifanya majukumu yao ya ulinzi wan chi na serikali ikifanya majukumu yake basi suala la uvunjifu wa amani halitokuwepo,”alisema.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema mwanamke ananafasi kubwa ya kuhakikisha amani ndani ya ngazi ya familia inapatikana, pamoja na ndani ya jamii.

Walisema mwanamke anatumia muda mwingi kuwepo majumbani na kujua nani ameingia ametoka, hivyo itakua ni rahisi kwao kutoa taarifa kwa viongozi wa shehia.

MWISHO