Friday, October 18

Wajumbe wa bodi ya Jukwaa la haki za watoto wakutana kisiwani Pemba kujadili mpango kazi mpya.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MRATIBU wa Jukwaa la haki za Watoto Zanzibar Sohpia Leghela, alisema lengo la mkutano mkuu wa bodi ya ushauri ya Watoto Zanzibar ni kuwaleta Watoto pamoja kuweza kujadiliana na kutoka na mpango kazi wa mwaka 2024/2025.  

Mratibu huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano huo, uliowashirikisha wajuumbe wa bodi hiyo kutoka Unguja na Pemba, na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema katika mkutano huo, mapendekezo ambayo watoto wameweza kuyatoa ni pamoja na kutoa elimu juu ya haki za Watoto, kwa Watoto wenyewe pamoja na kufika kwa jamii.

Alisema ni kufika kwa jamii na kuelezea umuhimu wa mabaraza ya Watoto, pamoja na kukutana na viongozi wa serikali, hasa ngazi ya wilaya kujadiliana nao namna gani wanaweza kuyawezesha mabaraza ya watoto ngazi ya Wilaya na kufanya kazi vizuri.

Aidha alisema watoto hao wamependekeza kukutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa ajili ya kuzungumza nae kuhusiana na masuala mbali mbali yanayowahusu watoto.

“Mambo mengi yamezungumzwa katika mkutano huu, kila mmoja ameonyesha utayari wake katika kuhakikisha watoto wanafikia maelengo yao kimaendeleo na kielimu,”alisema.

Nae Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Pemba Mwanaisha Ali Massoud, alisema imani yake ni kuona Watoto hao watachangia ili kuona maoni yao yanachukuliwa na kufanyiwa kazi.

“Hakikisheni katika mpangokazi huu munachangia ipasavyo kwa kutoa maoni yenu, ili mpango kazi unaokuja uweze kutekelezeka na kuwa bora Zaidi,”alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la watoto Zanzibar Alhadhir Khamis Abrahman, alisema kuna baadhi ya vitu mpango kazi uliopita hawakuweza kuvitekeleza kutokana na muda na kutokuwezeshwa na wadau na viongozi wa serikali.

Alisema malengo yao haswa ni kuhusu changamoto zinazowakabili watoto, mwaka uliopita na mwaka huu pamoja na mapendekezo yao juu ya viongozi wa serikali nini wafanye na kupasa sauti za Watoto.

“Watoto wanakumbana na changamoto nyingi na kupaza sauti zao wendi wao hawawezi, sasa sisi baraza ndio chambo chao cha kufikisha changamoto zao kwa viongozi wa serikali na wadau wengine ili haki zao waweze kuzipata,”alisema.

Kwa upande wake katibu mstaafu wa barala za watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aboubakar Sadik, alisema wamelazimika kukutana ili kuandaa mpango kazi ambao utahakikisha baraza la Watoto Zanzibar linakua imara.

Alisema katika mpango kazi huo utahakikisha baraza la Watoto linakua endelevu, kutoa elimu juu ya wajibu wa mtoto katika jamii, kupunguza changamoto za udhalilishaji wa Watoto katika jamii.

“kutekelezwa kwa mpango kazi huo ni mafanikio kwa bodi ya ushauri ya Watoto Zanzibar na baraza la Watoto Zanzibar, pamoja na kuwepo na ustawi mzuri wa Watoto,”alisema.

Katika mkutano huo wajumbe wa bodi ya Watoto zanzibar wamweweza kupitisha mpango kazi wa mwaka 2024/2025.

MWISHO