Wednesday, January 15

Zaidi ya wakulima 3000 wanapokea fedha zao kupitia TigoPesa

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WAKULIMA wa Zao la karafuu Kisiwani Pemba, wameshauriwa kuendelea kupokea fedha zao kwa kutumia TigoPesa, kufanya hivyo ni kuwasaidia vijana waliojiajiri wenyewe kuwa mawakala wa mitandano ya siku.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa TigoZantel Zanzibar Azizi Said Ali, wakati alipokua akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana na utoaji wa zawadi, kwa wakulima wa zao la karafuu Kisiwani Pemba, hafla iliyofanyika Mjini Chake Chake.

Alisema wameamua kuwa karibu zaidi na wale wanaoshirikiana nao kwa kukubali kulipwa kutumia TigoPesa, kwani waliokubali kulipwa ni ndugu zao na wametoa sadaka kubwa kwa vijana waliojiajiri kupitia uwakala.

Alisema tokea mwaka huu kuanza msimu, zaidi ya wakulima 3439 wamelipwa fedha zao kupitia miamala ya TigoPesa, na kuwataka wakulima wenye miamala mikubwa kuendelea kupokea fedha zao kupitia tigoPesa.

“Haya ni mafanikio makubwa licha ya huu kuwa ni msimu mdogo, lakini haizidi asilimia 20 waliolipwa kupitia TigoPesa, hata wakiwemo wenye miamala mikubwa,”alisema.

Aidha Mkurugenzi Azizi alisema fedha kwenye mfumo rasmi hauwezi kupotea, kwani siku ikitokea mtandao wa Tigo kutokufanya kazi basi pesa ziko salama na zimesibitishwa na B.O.T.

Alifahamisha kwamba tigoZantel imejipanga kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo nchini, hii ni kutokana na kurudisha kwa wananchi kile wanachokipata.

Nae Mdhamini wa ZSTC Wilaya ya Chake Chake Khamis Khamis, aliwapongeza wakulima wa karafuu kwa kuendelea kupokea fedha zao kupitia mtandao wa TigoZantel.

Alisema mfumo wa kuchukua fedha keshi unajulikana madhara yake, huku akiwasisitiza kuendelea kupokea fedha zao kupitia TigoPesa, kwani wanafaidika wengi ikiwemo vijana ambao wamejiajiri kama mawakala.

“Vijana wengi sana wamejiajiri kupitia mawakala na sisi wakulima ndio tulioamua kuwawezesha na tuendelea pia kuwaunga mkono wenzetu hawa,”alisema.

Hata hivyo aliwashukuru wakulima wa karafuu kwa kuendelea kuuza karafuu zao shirika la ZSTC, kwani wamefanya maamuzi sahihi na sio kuuza kwa njia ya magendo.

Mapema meneja wa Tigo Zantel Zanzibar Salum Nassor Mohamed, alisema wakulima wa karafuu na TigoZantel ni kitu kimoja, wanapaswa kuendeleza umoja huo kwani bado msimu wa karafuu haujamaliza.

Kwa upande wao wakulima wa zao la karafuu Kisiwani Pemba, wameahidi kuendelea kupokea fedha zao kwa kutumia miamala ya simu ikiwemo TigoPesa.

MWISHO