NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA) imezindua kampeni ya Home Stay, yenye lengo la kutambua majengo ambayo hayajasajiliwa na yanalaza wageni ndani ya Wilaya ya Chake Chake.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Kodi Pemba kutoka ZRA Ali Khatib, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ndani ya Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema kumekua na nyumba nyingi zinalaza wageni ndani ya wilaya hiyo, lakini bado hazijatambulika rasmi na ZRA jambo ambalo linaleta ukakasi.
“Kampeni hii leo tuemizindua ikiwa tumo katika mwezi wa shukurani kwa mlipa kodi, na majumba yapo yanayolala wageni ila hayajatambuliwa leo tumeamua kuwapatia elimu wamiliki ili kuweza kuzisajili nyumba zao,”alisema.
Alisema kuna umuhimu mkubwa ni kuzitambua na kupeana taaluma, juu ya kuzisajili nyumba hizo kwa kufuata taratibu za kuendesha biashara zao.
Alifahamisha kwamba Serikali ya awamu ya nane ni muumini wa kodi rafiki kwa wananchi wake, hivyo kile ambacho mgeni analipa basi na serikali inataka ipate kidogo kupitia mgeni huyo.
Hata hivyo aliwashukuru masheha kwa kushirikiana nao na kuweza kuzitambua nyumba hizo, katika meneo yao ambayo kuna nyumba zinalaza wageni na bado hawajazisajili.
Nae Afisa anaesimamia majengo ya biashara na yakawaida kutoka ZRA Ahmed Abdulrahman Shehe, aliwataka wamiliki kulipa kodi kwa hiyari ZRA ili kodi zao ziweze kuchangia uchumi wa Zanzibar.
Kwa upande wake Afisa Kutoka ZRA Nassor Ahmed Said, alisema wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni, wanatakia kusajili nyumba zao ili waweze kulipa kodi pamoja na nyumba hizo kutambulika kisheria.
Nae Mwakilishi wa nyumba ya kulala wageni Mkoroshoni Rashid Mohamed Said, aliishukuru ZRA kwa kuweza kuwashajihisha kusajili nyumba zianzolaza wageni na kukubali kulipia kodi ZRA katika taasisi husika.
“Ni jambo zuri la kupita na kutoa elimu kwani wamiliki wengi hawafahamu umuhimu wa kusajili majengo yao, kama yanapaswa kusajiliwa na kulipia kodi serikalini,”alisema.
Aliwataka ZRA kuhakikisha wanakitangaza kisiwa cha Pemba kiutalii, ili wageni wengi waweze kukifahamu na kumiminika kufika kutembelea kisiwa hicho.
Hata hivyo aliwataka ZRA kuendela kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya suala zima la ulipaji wa kodi, sambamba na kuwapunguzia kodi hiyo ili na wao waweze kunufaika.
Kwa upande wake Mohamed Ali Hamad (kley), alisema nyumba yake anapokea wageni wake mbali mbali na wanalala na kulipia kidogo, hivyo ni muhimu kwa ZRA kuendela kushamaisha juu ya suala la usajili wa majengo hayo.
MWISHO