NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Simai Mohamed Said, amesema wananchi wa Zanzibar wanakila sababu ya kuyalinda, kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, kwani yamepelekea wazanzibar kuwa wamoja na kufanya shuhuli zao kwa amani na utulivu.
Alisema hivi sasa Zanzibar ipo katika serikali ya Umoja wa kitaifa hakuna ubaguzi wa kisiasa, huku akiwapongeza walimu kwa kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi wao, bila ya kujali siasa zao kwani muda wake haujafika.
Waziri Simai aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na walimu, wananchi wa Wilaya ya Wete mara baada ya ufunguzi wa Ofisi ya Elimu na Mafunzo ya Amali Wilaya ya Wete, Mitiulaya ikiwa ni shamrashamra za miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar.
Aidha alisema Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, inakwenda spidi na inamsaidia yeye katika kuleta maendeleo, Umoja na Amani ya Zanzibar.
“Sisi viongozi tumepewa maelekezo na hatutofanya masikhara viongozi wote tuliobahatika, lazima tuulinde umoja na mshikamano wetu tulionao, ili kutimiza maelengo ya serikali ya awamu ya nane,”alisema.
Alisema wananchi wamekua wakiendelea kushuhudia miundombinu ya elimu ikiimarika kila kona ya nchi hii, ujenzi wa skuli 25 za magorofa za kisasa Unguja na Pemba, ambapo kwa mara ya kwanza Serakili inajenga Ofisi za Wizara ya Elimu kila wilaya kitu ambacho hakijawahi kutokea.
Alifahamisha kuwa ujenzi wa maktaba unaenda sambamba na ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza kujenga utamaduni wakujisomea na kuhamaisha wananchi kuhusu matumizi ya maktaba na kujenga maktaba tatu Unguja na Pemba ambapo Wizara imeshapindukia shabaha ya utekelezaji.
Hata hivyo Waziri Simai alisema mategemeo ya Ofisi hizo zitasaidia kutatua changamoto zilizopo katika skuli na kuondosha urasimu na kulifanya eneo la Mitiulaya kutaweza kuimarisha huduma ya elimu na utoaji waelimu bora.
Aidha alisema ujenzi wa ofisi hizo kunatoa mwanga mpya katika kuboresha hali ya elimu katika wilaya ya wete, hiyo ni hatua muhimu inayoendana na dhamira ya serikali jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono.
Mapema Naibu waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Abdull-ghulam Hussein, alisema Rais Dk.Mwinyi kipaombele chake kikubwa amekwenda kuongeza bajeti ya Wizara ya Elimu na lengo la kuboresha miundombinu na tayari wameanza kwa kujenga skuli za Gorofa za Msingi na Sekondari.
Alisema pia Rais aliahisi kwenda kujenga skuli za Gorofa pamoja na za maandalizi lengo ni kutoa huduma bora kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu wao.
Akitoa salamu za Mkoa wa Kaskazini Pemba Mkuu wa Mkoa huo Salama Mbarouk Khatib, alisema katika kufanikisha malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi ameweza kufanikisha malengo ya Mapinduzi hayo kwa Vitendo ikiwemo miradi mbali mbali ya maendeleo nchini.
Aidha aliwataka watendaji wa jingo hilo kuhakikisha wanalitunza na kulilinda, ili kuweza kudumu kwa muda mrefu kwani adhma ya kujengwa majengo hayo ni kuboresha huduma na utendaji wakazi na kuwaweka wafanyakazi katika mazingira mazuri ya kazi.
Akitoa amelezo ya Kitaalamu juu ya mradi wa huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam Ameir, alisema ujenzi wa Ofisi hiyo imegharimu jumla ya shilingi Milioni 342,000,000/= ambapo ni fedha za serikali.
Alisema majengo hayo tayari yameshajengwa katika Wizara Saba za Zanzibar, ikiwemo Wete, Chake Chake, Mkoani, Wilaya ya Mijini, Kaskazini A, Kati na Magharibi B.
MWISHO