Friday, January 10

WAZIRI wa Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ afungua  Ofisi ya Elimu Wilaya ya Chake Chake,

NA ABDI SULEIMAN,  

WAZIRI wa Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Massoud Ali Mohamed, amesema kuwa wazanzibari wamekua huru katika kupanga shuhuli za kuleta maendeleo, kama inavyokumbukwa mwaka 1964 serikali iliyokua ikiongozwa na hayati Mzee Abeid Amani Karume, alipotangaza elimu bure na vijana wote kutakiwa kupata elimu.

Alisema ni elimu hiyo mtu anatakiwa kuipata popote alipo bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anayalinda na kuenzi na kudumisha kwa maendeleo ya nchi.

Aidha alisema mbali na skuli 25 zinazoendelea kujengwa hivi sasa, tayari maendeleo makubwa yamepatikana katika sekta ya elimu nchini.

“hatua ya mafanikio ya mwanaadamu hakuna njia nyengine ya mkato wowote ispokua ni suala zima la kupata haki yake ya elimu, hata viongozi wa dini waliotangulia walihimizwa kusoma,”alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Massoud, Waziri Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Shaame Khamis, huko katika viwanja vya Tenisi Chake Chake mara baada ya ufunguzi wa Ofisi ya Elimu Wilaya ya Chake Chake, ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi.

Aidha alisema serikali ya awamu ya nane imepitiliza katika malengo yake kuyajenga na kuyatetea Mapinduzi ya 1964 kwa hatua mbali mbali zilizofikiwa ikiwemo miradi mbali mbali ya elimu inayoendelea kujengwa na kuboresha sekta ya elimu nchini.

Waziri huyo aliwataka viongozi wa ofisi ya Wizara elimu, kuhakikisha jengo na vifaa vilivyomo wanavitunza na kuvithamini, ili malengo ya sekta ya elimu kuona yanatimia kwa vitendo ikiwemo kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

“Serikali itaendelea kuimarisha ofisi za elimu za Wilaya na Mikoa, ili huduma bora ziweze kupatikana kama ilivyo uzuri wa majengo husika,”alisema.

Hata hivyo aliwataka wazazi kuhakikisha wana waandikisha skuli Watoto wao mapema, ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya nane katika kuboresha miundo mbinu ya elimu.

Nae naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Abdughulam Hussein, alisema serikali ya awamu ya nane imeanza kufanya mageuzi makubwa katika sekta elimu, kwa kujenga ofisi za Wilaya na kuendelea na Mikoa.

Aidha aliwatahadharisha maafisa hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao vizuri kwa kufuata taratibu zote, vyenginevyo ataondokana na kupatiwa nafasi afisa Mwengine.

Akitoa salamu za Mkoa wa Kusini Pemba, Mkuu wa Mkoa huo Mattar Zahor Massoud, alisema Rais Dkt.Mwinyi amesema uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo majengo, Vifaa vya kisasa, ajira za walimu na maslahi yao.

Alisema sehemu kubwa ya bajeti ya Zanzibar ukiachilia suala la Ulinzi, inapelekwa kwenye sekta ya elimu ambayo Rais ameipa kipao mbele Zaidi kwani inatokana na misingi ya Mapinduzi.

“Sote tunafahamu Marehemu Mzee Abeid Amani Karume jambo la mwanzo alilolifanya ni kutangaza elimu kuwa bila ya malipo, akiamini wananchi na Watoto wakizanzibar wanastahiki kupata elimu kwa mujibu wa uwezo wao, jitihada ambazo serikali ya awamu ya nane inaendelea,”alisema.

Aidha Mattar alifahamisha kwamba kama tunataka kujenga taifa imara, lililo na watu walio na elimu, lililo na watu wenye uwezo wakutumiakia nchi yao kwa muda wote lazima tuwekeze katika elimu.

Alisema suala la elimu ni jambo la kwanza, lazima tushajihishike katika kuwekeza kwenye elimu kwa Watoto, hivyo kila mzazi anajukumu la kuhakikisha anafutilia maendeleo ya elimu kwa Watoto wao.

Mapema akisoma taarifa ya kitaalamu ya ujenzi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said, alisema ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu shilingi Milioni 342 hadi kukamilika kwake.

MWISHO