NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amsema Serikali imeanza utekelezaji wa mageuzi katika mfumo wa elimu, ili kuhakikisha vijana wanapata elimu inayowezesha kukabiliana na changamoto za mazingira yao halisi.
Rais Mwinyi aliyaeleza hayo katika viwanja vya skuli ya sekondari Maziwang’ombe Wilaya ya Micheweni, mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi skuli hiyo ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuanzia mwaka 2024, Serikali itaanza majaribio ya mtaala mpya wa elimu ya sekondari, mtaala ambao utalenga kujenga ujuzi wa vijana katika fani mbalimbali kwa kuzingatia mazingira yao.
“Kwa Maziwang’ombe, hii inamaanisha vijana watapata ujuzi unaoendana na mazingira yaliotuzunguka, ikiwa ni pamoja na uwekezaji unaotarajiwa katika ukanda huu,” alisema .
Aisha alisema hatua hiyo ni muhimu sana kwani itahakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora, wanafundishwa mambo yanayowavutia na kufaa kwa mazingira yao, hivyo aliitaka jamii kuhakikisha inaunga mkono mabadiliko haya, kwani yataleta matokeo chanya si tu kwa vijana, bali pia kwa maendeleo ya jamii na uchumi wa eneo kwa ujumla.
Aidha alisema ufanisi wa utekelezaji wa mageuzi hayo ni lazima uendane sambamba na uimarishaji wa nguvu kazi ya walimu, kwani uwepo wa majengo ya kisasa hayatoshi pasi na kuwepo kwa walimu wenye sifa na uwezo wakufundisha.
Alisema serikali inatambua changamoto ya uhaba wa walimu inayoikabili visiwa hivi, hususani Wilaya yetu ya Micheweni kwani takwimu zinaonesha katika ngazi ya elimu ya msingi, kwa wastani Wilaya hii ina uwiano wa wanafunzi 76 kwa mwalimu mmoja mara mbili zaidi ya uwiano huo katika Wilaya ya Mjini.
Katika hatua nyengine alisema Serikali katika mwaka huu wa fedha imekusudia kuwajiri walimu wapya 1500, ili kupunguza pengo hilo, Pamoja na kuajiri walimu, sambamba na kuhakikisha walimu wanapata stahiki zao na wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
“Katika jitihada za kuhakikisha kwamba tunaboresha usimamizi na utoaji wa haki kwa walimu, Serikali imeridhia pendekezo la kuanzisha Tume ya Utumishi ya Walimu, wizara ya elimu inaendelea na taratibu za kuanzisha tume hiyo ambayo itakuwa muhimu sana katika kufanikisha malengo yetu ya maendeleo ya elimu nchini,”alisema.
Hata hivyo alisema Mapinduzi yaliyofanyika 1964 yameleta uhuru, umoja na mshikamano kwa Wazanzibari wote, ambapo sasa kila mmoja anajivunia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
Rais Dkt.Mwinyi alisema Serikali ilitangaza elimu bure kwa wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, sasa kuna skuli za kisasa za ghorofa katika maeneo ya mijini, pia vijijini na kwenye visiwa vidogo vidogo, kama vile Maziwang’ombe, Gamba , Kojani na Tumbatu.
“Kabla ya Mapinduzi Zanzibar iliandikisha wanafunzi 25,432 Unguja na Pemba katika ngazi zote, sasa kufuatia kuimarika kwa miundombinu idadi ya wanafunzi imeongezeka nakufikia wanafunzi 592,781, kuanzia ngazi ya maandalizi hadi sekondari,”alisema.
Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa majengo haya 25 katika maeneo mbali mbali, lengo la Serikali nikuhakikisha inatatua kadhia ya muda mrefu ya vijana kusoma kwa shifti mbili, yaani vipindi vya asubuhi na mchana, na kutatua msongamano wa wanafunzi darasani kufikia wanafunzi wasiozidi 45 kwa darasa moja.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, alisema watahakikisha wanaendelea kusimamia na kutekeleza ile dhamira yake ya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu iendelee vizuri.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema katika serikali ya awamu ya nane Mkoa huo umeweza kupata miradi mbali mbali ya maendeleo, ikiwemo skuli, Hospitali, barabara na majengo mengine.
Alisema Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekua ni raisi wa mfano, katika kusimamia na kutekeleza kwa vitendo matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo yaliasisiwa 1964, kwani miradi ya elimu ni moja ya matunda hayo.
Mapema katibu Mkuu Wizara ya Elimu Khamis Abdulla Said, akisoma taarifa ya Kitaalamu, alisema ujenzi wa skuli hiyo umefikia asilimia nzuri na unatarajiwa kugharimu Bilioni 6.2 hadi kukamilika kwake.
Alisema skuli hiyo inatumia mfumo wa biogas, maji ya makaro husafishwa na kutumiwa kwa kumwagia bustani, kwani ni mfumo wa kisasa .
Nae Mzee Khatib Najarawe Arif, alisema mabadiliko ya maendeleo ni makubwa yaliyofanywa na Rais wa awamu ya nane, katika kuhaikisha wananchi wanapata elimu bora.
Alisema wananchi wa Maziwang’ombe wataendelea kumuunga mkono Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kwani maziwang’ombe ameweza kuibadilisha kwa kiasi kikubwa katika suala la maendeleo.
MWISHO