Saturday, December 28

Rais Dkt. Mwinyi aweka jiwe la msingi skuli ya Sekondari Utaani.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, amesema mara baada ya kushika hatamu, tarehe 23 Septemba 1964, Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya kwanza iliyoongozwa na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, ilitangaza elimu bure, ili kutoa fursa sawa kwa wananchi wake wote kupata elimu bila ya ubaguzi wowote. 

Alisema fursa za elimu zilifunguka na kupata elimu ikawa ni haki ya msingi kwa kila raia, hali iliyopelekea Serikali kuweka mikakati mbali mbali katika utekelezaji wa tamko hilo la elimu bure.

Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi aliyaeleza hayo, huko katika viwanja vya skuli ya Sekondari Utaani mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi skuli hiyo, ikiwa ni shamra shmra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha alisema gharama zote za elimu zilibebwa na Serikali na Miundombinu mbalimbali ya skuli, ilianza kujengwa ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya elimu.

Alifahamisha kwamba mikakati ya utelekezaji wa malengo ya Mapinduzi ya kuhakikisha kila mmoja, anapata haki yake ya elimu imekuwa ikiendelezwa katika kila awamu inayoongoza nchini, kwani hayo yanadhihirishwa na hatua kubwa ya maendeleo iliyoifikia katika kutanua fursa za upatikanaji wa elimu Unguja na Pemba.

Hata hivyo alisema ujenzi wa skuli hiyo ya ghorofa tatu ya utaani ni ushahidi wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwani inatekeleza kujenga madarasa 1,500 ya msingi na sekondari katika kipindi cha miaka mitano, 2020 – 2025.

“Ni jambo la kujivuania ndani ya miaka mitatu wamevuka lengo hilo, ambapo sasa jumla ya madarasa 2,273 sawa na asilimia 150 ya malengo ya ilani yamejengwa kupitia ujenzi skuli mpya na kukamilisha madarasa ya yaliyoanzishwa na wananchi Unguja na Pemba,”alisema.

Katika hatua nyengine alisema ujenzi wa skuli ni miongoni mwa skuli 25 za ghorofa zinazojengwa Unguja na Pemba, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, ambapo serikali kupitia Wizara ya Elimu imejenga ofisi saba za elimu za Wilaya, ili kuimarisha uongozi wa elimu katika ngazi za Wilaya na muda mfupi ujao itakamilisha ofisi za Elimu katika wilaya nne zilizobaki.

Aidha alisema vitendo hivyo vya uimarishaji wa Miundombinu ya elimu ni endelevu, serikali imejipanga kuendeleza kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani pia kushirikiana na washirika wa maendeleo.

Alisema uwekezaji huo katika elimu utakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa mbali mbali ikiwemo vya kufundishia, kujifunzia sambamba na kuajiri walimu wenye sifa ili kukabiliana na tataizo la upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi na hesabu.

Hata hivyo alisema nijambo la kutia moyo jitihada zinazofanywa na serikali za uwekezaji katika elimu zimewezesha kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani mbali mbali ya Taifa.

Akizungumzia suala la matokeo ya mitihani ya kidato cha Sita iliyofanyika mwaka huu wa 2023, inaonesha kuwa kati ya wanafunzi 2,587 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 2,570 wamefaulu kuendelea na masomo ya chuo kikuu katika kiwango cha Divisheni I hadi III, asilimia 65.9 wamefaulu katika masomo ya Sayansi.

Alisema wanafunzi waliopata Divisheni 4 wamepungua kutoka wanafunzi 199 mwaka 2021, na kufikia wanafunzi 15 mwaka 2023 na wanafunzi waliofeli kwa kiwango cha Divisheni 0 wamepungua, kutoka wanafunzi 99 mwaka 2021 na kufikia wanafunzi 2 mwaka 2023.

Hata hivyo alisema Serikali itahakikisha hali hiyo inaimarishwa zaidi na kufikia 0 aslimia ya kufeli mitihani, kwa upande wa mitihani ya kidato cha nne, asilimia ya ufaulu imeongezeka kutoka 55.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 74.0 mwaka 2022. Ni matumaini yetu kuwa uwekezaji unaondelea kufanywa na Serikali utachochea zaidi uimarishaji wa ufualu wa vijana wetu.

“Nimatumaini yetu kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na serikali katika sekta ya elimu utachochea Zaidi uimarishaji waufaulu wa vijana,”alisema.

Aidha aliwaomba wananchi kuendelea kuipa ushirikiano serikali katika kutekeleza mikakati ya mageuzi katika elimu ili kuhakikisha vijana wanapata elimu ilio bora kwa maslahi yao jamii na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo alisema hawanabudi kuhakikisha Watoto wanawandikisha skuli na kuwasimamia ili kupata haki yao ya elimu, kwani kufanya hivyo ni kuchangia malengo ya mapinduzi, ya kuwapatia Watoto elimu bila ya ubaguzi.

Kwa upande wake Waziri wa ELimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, alisema serikali inaendelea kuboresha miundombinu, inalipa mishahara wanafunzi ambapo kila serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapoingia elimu inakua ni kipaombele chake.

Aidha alimshukuru Rais Dkt.Mwinyi kwa kuifanya sekta ya elimu kuwa kipaombele chake, kwani uwepo skuli hiyo ni jitihada zake za kuhakikisha miundombinu ya elimu inaimarika.

Nae naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mohamed Said dimwa, alisema CCM inampongeza sana Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 98 zimekamilika.

Alisema CCM ndio daraja kati ya wananchi na serikali yake, kwani miundombinu ya skuli 62 inayojengwa imeondosha aduwi ujinga, kila wilaya hospitali za maana aduwi maradhi ameshaondoka.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la  Wete kupitia chama cha ACT-Wazalendo Omar Ali Omar, alimshukuru Rais Dkt.Hussein kwa maendeleo makubwa anayoendelea kuyafanya ndani ya jimbo la Wete, ikizingatiwa kuwa maendeleo hayana siasa wala chama.

Alisema kilio cha wananchi wa utaani sasa kimeondoka baada ya skuli ya ghorofa kuekewa jiwe la msingi, kwani kilio chao hicho baada ya skuli kongwe kuungua moto na kuvunjwa.

Mapema mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema wananchi wa mkoa huo hawatomuungusha na kazi anayoifanya wanaiunga mkono moja kwa moja.

Alisema serikali ya awamu ya nane imefanya mambo mengi makubwa, kwani serikali yake imeweza kuinyanyua wilaya ya wete kimaendeleo na miradi mikubwa ya maendeleo.

Akisoma taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said, amesema ujenzi wa skuli hiyo unatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 6.2 hadi kukamilika kwake.

MWISHO