Saturday, December 28

Waziri Shamata azindua ofisi ya elimu Wilaya ya Mkoani.

NA AMINA AHMED-PEMBA.

Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalilenga kuondosha utawala wa kidhalimu na kuwafanya wananchi kufurahia matunda ya Uhuru kwa kuwaletea maendeleo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Mifugo na Maliasili Mh. Shamata Shaame Khamis katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Elimu Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni Miongoni mwa Shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema katika kupiga hatua kimaendeleo suala la elimu ni muhimu hivyo Serikali imekua ikiimarisha Miundo mbinu ya kielimu ili kusukuma mbele kasi ya maendeleo nchini.

Amesema kutokana na jitihada za Serikali za kutatua changamoto za kielimu mafanikio yanaonekana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ufaulu katika ngazi mbali mbali.

Amewataka wananchi kuthamini jitihada hizo kwa kuendelea kuwaamini na kuwaunga Mkono Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Akizungumzia suala la udhalilishaji amesema bado nchi inakabiliwa na janga hilo hivyo amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za kutokomeza vitendo hivyo vya udhalilishaji.

Aidha amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Nae Naibu Waziri wa Elimu Na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Abdulghulam Hussein amesema zaidi ya Skuli 62 za ghorofa zimeshajengwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Amesema Ofisi za Wilaya ni mkakati katika Utekelezaji wa mageuzi makubwa ya Elimu yanayolenga kuimarisha ubora wa huduma za elimu nchini.

Pia  amewataka wananchi kutunza miundo mbinu ya majengo na vifaa ili viweze kutumika kwa muda mrefu.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar . Khamis Abdullah Said akisoma taarifa ya kitaalamu kuhusu Ujenzi wa Ofisi hiyo amesema jumla ya Tsh. milioni 182 zimetumika kukamilika ujenzi wa Ofisi hiyo ambayo awali jengo hilo lilianzishwa na Baraza la Mji Mkoani.

Amesema Wizara inamatunaini makubwa kwamba kasi ya ufuatiliaji itaongezeka kutokana na uwepo wa Ofisi hizo ambazo zimeshajengwa katika Wilaya saba.

Amewapongeza Walimu wa Wilaya ya Mkoani kwa matokeo mazuri ya Mitihani ya darasa la saba mwaka 2023 ambapo Wilaya hiyo imeibuka ya kwanza Kitaifa.