Sunday, November 24

Wadau wa maendeleo ya vijana wapitia sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2023

Na Maryam Talib – Pemba. 

WADAU wanaoshuhulikia uratibu wa maendeleo ya vijana kisiwani Pemba wametakiwa kuongeza juhudi  na kasi ya utekelezaji wa maswala ya vijana kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika nchi.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya vijana Zanzibar Shaib Ibrahim Mohamed alipokuwa akifunga kikao cha siku moja cha upitiaji wa ripoti na sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2023 kwa wadau wa maendeleo ya vijana katika ukumbi wa Samael Gombani Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Mkurugenzi huyo akitoa pongezi kwa wadau hao alisema ipo haja ya kuongeza juhudi ya ushirikiano katika utekelezaji wa shuhuli zao kwa mwaka 2024 kama ilivooneshwa maendeleo na mafanikio kwa mwaka 2023.

“Ninachoamini kwa mwaka huu 2024 kutaongezeka kasi, ari  katika utekelezaji wa shuhuli za maendeleo ya vijana” alisema Mkurugenzi huyo.

Akisoma ripoti yake katika kikao hicho cha mapitio ya ya kota Bimkubwa Masoud Abdalla ambae ni muelimishaji rika Vikunguni aliisema wamekua na waelimishaji sita , wanawake watatu na watatu wanaume katika kituo chao.

Bimkubwa alisema katika ripoti hiyo wameweza kuwafikia vijana sabiini ambapo arobaini wanawake na thelethini wanaume wakiwemo wapya ishirini na tano na arobaini na tano ni wa marudio.

Alisema katika wateja wao wote hao baada ya kupatiwa elimu walifanya vipimo maabara ikiwemo kipimo cha HIV na wote majibu yao yamekuwa salama.

Hata hivyo ameiomba Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo kupitia taasisi yake ya vijana kuwapatia elimu  kwa lengo la kuwafikia vijana walio wengi Zaidi.

Nae Said Salim Othman ambae ni afisa ajira Ofisi ya Raisi Kazi Uchumi na Uwekezaji katika kikao hicho cha kupitia ripoti ya miezi sita julai  – Disemba  alisema Serikali hii ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiwapatia fursa nyingi vijana kwa lengo la kukukuza uchumi ikiwemo kuanzishwa kwa mabaraza ya vijana, mafunzo kwa vijana ili kuwawezesha na kuwakuza kimaisha.

Said alisema kwa upande wa ajira rasmi Wilaya zote nne Kisiwani Pemba kumekuwa na ajira 89, Wilaya ya Chake Chake  ajira 48 wanaume 33 wanawake 15, Wilaya Mkoani ajra 22 ,wanawake 6 wanaume 16 ,Wilya ya Wete 16, wanaume 11 wanawake 5 na  Wilaya ya Micheweni ajira 3 wanaume 2 wanawake 1.

kwa upande wa ajira zisizo rasmi zimekuwa ni 2094 kwa Wilaya zote nne Kisiwani Pemba wilaya ya Chake Chake 493 Wilaya ya Mkoani 832 Wilaya ya Wete 467 na Wilaya ya Micheweni ajira 302 ,pia idara ya ajira imeweza kuratibu kwa ajili kutoa mafunzo ya simu katika chuo cha Karume Mbweni Zanzibar jumla ya vijana 20 kutoka katika Wilaya zote nne za Pemba wameweza kuchaguliwa kwa ajili ya kujiunga mafunzo hayo ya ufundi simu.

Nae Ali Mussa Bakar ambae ni Afisa Vijana Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba alisema suala hili la upitiaji wa ripoti za Utekelezaji wa maendeleo ya vijana kwa kila muda ni jambo jema ambalo linaleta hamasa kwa kila mdau kujua wajibu wake katika kuwatekelezea vijana huduma zao na pia kuleta maendeleo endelelevu katika Nchi.

MWISHO.