Sunday, November 24

KOICA YAKABIDHI DAHALIA LA WANAWAKESKULI YA TUMBE

BAKAR MUSSA ,PEMBA

WAZIRI wa Kilimo , Umwagiliaji na mali asili Zanzibar , Shamata Shaame Khamis ameipongeza Serikali ya Korea Kusini  kupitia Shirika lake la KOICA ( Korea International Cooperative Agency) kwa juhudi zake wazozichukuwa za kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar misaada mbali mbali ikiwemo Elimu.

Alisema Elimu ndio kitu muhimu katika maisha ya mwanaadamu kwani huwezi kufanya jambo lolote bila ya kuwa na elimu na ndio Mwaasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar hayati Abeid Aman Karume akatangaza kuwa Elimu itolewe bila ya malipo (Elimu bure).

Alieleza hayo huko katika Skuli ya Sekondari Chwaka Tumbe , kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar , Tabia Maulid Mwita wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Dakhalia ya Wasichana iliojengwa na Taasisi ya KFHI kwa ufadhili  wa KOICA (Korea International Cooperative Agency)  Korea kusini.
.

Alifahamisha Mapinduzi ya mwaka 1964 yameleta Uhuru, Umoja na Mshikamano , hivyo ni vyema kuyalinda na kuyatetea kwa nguvu zao zote kwani ndio yaliowafanya wawe na uwezo wa kujinasibu wao ni Wazanzibar.

Alisema katika kuona umuhimu wa Elimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukuwa juhudi mbali mbali za kuboresha mazingira mazuri ya Elimu ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa sambamba na kuongeza maslahi mazuri kwa walimu ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.

Alifahamisha kuwa kutokana na mazingira hayo ya kujisomea kumekuwa na ongezeko kubwa na ufaulu wa Wanafunzi kwa madarasa tafauti kinyume na hapo kabla.

Shamata , alisema kujengwa kwa Dakhalia hiyo kutawafanya wanafunzi wawe na muda mkubwa wa kujisomea na kudurusu masomo yao kwa nafasi kubwa tafauti na wanapokuwa majumbani kwao.

“ Kuwepo kwa Dakhalia hii munanafasi nzuri kwenu ya kuweza  kudurusu masomo yenu tafauti munapokuwa majumbani kwenu kwa vile mutakuwa hakuna majukumu mengine munayopewa , hivyo hamuna budi kuzithamini
juhudi hizi zilizochukuliwa na KFHI kwa kusoma kwa bidii kubwa “, alisema.

Alieleza kuwa mbali na wadau hao wa Maendeleo  KOICA(Korea International Cooperative Agency) lakini hata Serikali ilikuwa na sababu ya kujenga Dakhalia katika eneo hili , ingawaje Serikali inaazma hiyo na kutowa fursa sawa kwa wanafunzi wa kike na kiume.

Shamata aliipongeza KOICA kwa kujenga majengo mbali mbali ikiwemo Dakhalia na Vyoo kwa Skuli ya Sekondari Chwaka Tumbe na Vyoo kwa Skuli ya Sekondari ya Shumba Vyamboni.

“ Elimu kwa mtoto wa kike ni muhimu kwani inamfanya aweze kujielewa na kujitambuwa na kuwa mlezi nzuri wa familia yake”, alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mkazo katika elimu hata katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025 imeeleza juu ya kuboresha Elimu kwa mtoto wa kike.

Kwa upande wake Mtedaji mkuu wa KFHI( Korea Food for the Hungry International) , Ms, Sommie Koh alisema wanayofuraha kubwa kukamilika kwa Dakhalia hiyo ya Wasichana katika Skuli ya Chwaka Tumbe kwani itawasaidia kupata fursa ya kupitia masomo yao kwa utulivu.

Alieleza ujenzi huo pia utawasaidia Wazazi wa watoto wa kike kusaidiwa ulezi wa watoto kwa vile watakuwa wanaishi kwenye Dakhalia hiyo wakati wote wakiendelea na masomo yao.

“ Ujenzi wa Dakhalia hii umejumuisha na miradi mengine tafauti kama vile ujenzi wa Vyoo na sehemu za kunawa mikono , pamoja na kutowa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu, wanafunzi na wazazi wa Skuli ya Sekondari ya Chwaka Tumbe na Shumba Vyamboni kwa Pemba”, alisema.

Ms, Sommie Koh aliwataka Walimu kuzidisha bidii kwa kusomesha zaidi ili kuwafanya Watoto wa kike waweze kukamilisha ndoto zao za kimasomo.

Nae Mkurugenzi wa KOICA (Korea International Cooperation Agency) Ofisi ya Tanzania Mr. Jongbun. Joo alisema Tanzania ni moja ya nchi kubwa ambayo imekuwa ikishirikiana nao katika kufanikisha miradi mbali
mbali ikiwemo ya Elimu na ndio ikawa tayari kufadhili mradi wa kuwajengea mazingira rafiki ya kujisomea kwa watoto wa kike.

Alieleza katika mradi huo ulitowa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanafunzi wa kike waweze kujitambuwa na kujiamini katika Skuli za Chwaka Tumbe na Shumba Vyamboni kwa Pemba ambapo katika kisiwa cha
Pemba wamekuwa wakifanya kazi na Skuli mbili na Ungua skuli tatu.

“ KFHI, kwa ufadhili wetu wa KOICA wameweza kujenga Dakhalia mbili moja ikiwemo hii ya Chwaka Tumbe kwa Pemba  na nyengine iko Mtule kwa Unguja”, alisema Mr , Jongbun.

Alisema KOICA itaendelea kuwa karibu sana na Serikali katika kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo ya wananchi wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba aliwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassan kwa
kuruhusu na kushirikiana na Wadau wa maendeleo ikiwemo KOICA kuleta miradi mikubwa nchini.

Aliwataka Wazazi kuekeza katika Elimu ili kuthamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali na Wahisani kwa kuwashajiisha Watoto wao kusoma kwa bidii ili waweze kukamilisha ndoto zao.

“ Elimu ni ufunguo wa Maisha hivyo shirikianeni na Walimu , na kamati za Skuli kuhakikisha Watoto wa kike kama ilivyodhamira ya Wahisani wetu hawa wanasoma na kufikia upeo wa akili zao kwani ukimuelimisha
mtoto wa kike umeielimisha jamii mzima”, alisema .

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kaskazini Pemba aliwataka Wazazi kutokuwapa majukumu makubwa ya kazi watoto hususan wa kike sambamba na kuwaozesha Waume mapema na kuwahimiza kusoma ili Taifa liweze kupata wataalamu .

Kwa upande wake Naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar , Mwanakhamis  Adam Ameir akitowa taarifa ya kitaalamu katika ujenzi wa jengo hilo la Dakhalia alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwezi june 2023 na umemalizika  kwa wakati ambapo zaidi Shiling milion 337 zimetumika.

Alisema Dakhalia hiyo inauwezo wa kuchukuwa wanafunzi wa kike 80 kwa wakati mmoja na tayari KFHI kwa ufadhili wa KOICA(Korea International Cooperative Agency ) wameshaweka Vitanda na magodoro sambamba na chumba cha Matron kwa ajili ya ulinzi wa wanafunzi.

“ Dakhalia ni sehemu muhimu ya kujisomea ,hivyo aliwataka Wanafunzi wa kike watakaotumia jengo hilo kuitumia fursa hiyo kwa kujisomea kwa bidii sambamba na kulitunza kwa usafi”, alieleza.

Aliwashukuru Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusukuma mbele gurudumu la Elimu

Hata hivyo aliipongeza Taasisi ya KFHI ( Korea Food for the Hungry International ) kupitia ufadhili wa KOICA ( Korea International Agency) kwa msaada wao mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo Elimu.

MWISHO.