Sunday, November 24

Akinamama wenye VVU wapumzike baada ya kujifungua-Dk. Rahila

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

AKINAMAMA wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wametakiwa kupata mapumziko baada ya kujifungua, ili wapate kuimarika kiafya pamoja na mtoto wake, huku akifuata maelekezo ya daktari wakati gani kwake anaweza kubeba mimba.

Aizungumza na mwandishi wa habari hizi, Msimamizi wa Vituo vya kutoa huduma kwa watu wenye VVU Dk, Rahila Salim Omar alisema, mwili unapotoa kiumbe unahitaji kujirejesha tena katika hali ya kawaida na ndipo uweze kubeba mimba nyengine.

Alisema kuwa, wakati wa ujauzito kinga ya mwili inashuka, kwa hiyo uwezekano wa kupata maambukizi mengine unakuwa ni mkubwa kiasi kwamba anaweza kupata maambukizi mengine yatakayoweza kumsababishia mtoto kupata VVU.

Alifahamisha kuwa, afya ya mama huyo inakuwa bado haijarudi katika hali yake ya kawaida, hivyo virusi vinaweza kupanda kwa vile kinga yake imeshuka na hatimae kumuambukiza mtoto.

“Hata kama mama mwenye VVU tumempima jana, basi akija leo ikiwa tumemgundua na ujauzito, tunampima tena wingi wa virusi, je idadi haijaongezeka?”, anaelezea.

Daktari huyo alieleza kuwa, ikiwa virusi vimeongezeka, wanampa huduma ya ziada kuweza kumkinga mtoto na maambukizi hayo, ambapo wanampima kila baada ya miezi mitatu mpaka pale atakapoachisha.

Kwa upande wake dk, Khamis Hamad ambae Msaidizi Meneja Kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Kifua kikuu, Homa ya ini na Ukoma, alieleza kwa mama mjamzito ambae anaishi VVU anahitaji zaidi kuzaa kwa mpangilio kutokana na kuwa kinga yake imepungua.

“Ingawa wajawazito wote kinga yao hupungua lakini hawa wanaoishi na VVU inapungua zaidi, hivyo anatakiwa apangiwe muda wa kuzaa kulingana na idadi ya virusi alivyonavyo”, alisema.

Alifahamisha kuwa, mimba za papo kwa papo, zinasababisha mwili kutokujirudi na unakuwa dhaifu, hivyo mama atakuwa hana mda wa kumshughulikia mtoto alienae, kwa malezi na hata katika mfumo wa kula.

‘’Mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama kwa miezi sita bila kumchanganyia chochote, lakini ikiwa mama atabeba mimba nyengine kabla ya wakati unaotakiwa, atamkosema mawanwe haki zinazostahiki’’, alieleza daktari huyo.

Maryam Salum ni mama anaeishi na VVU mkaazi wa Mabaoni Chake Chake alisema, alipata elimu kupitia madaktari na aliambiwa kwamba anapotaka kubeba mimba afike kliniki kupewa ushauri.

“Najitahidi kufuata ushauri wa daktari ili kumkinga mtoto wangu dhidi ya maambukizi, kwa sababu unapotaka kubeba mimba unapewa maelekezo na ni ni vizuri uyafuate”, alifahamisha.

Alisema, baada ya kubeba mimba anatakiwa kutumia dawa vizuri na chakula kizuri kwa lengo la kujenga afya yake na mtoto, ili kumkinga mtoto asipate maambukizi ya VVU.

Maryam Said Abdalla mkaazi wa Chake Chake ambae anaishi na VVU, alieleza kuwa, kuna umuhimu mkubwa kwa mama mwenye VVU kutumia uzazi wa mpango hasa kwa vile kinga zao ni tofauti na akinamama wasioishi na virusi vya Ukimwi.

“Kinga yetu ikishuka zaidi, lile fuko la uzazi linaweza kubeba maambukizi na likamsababishia mtoto maambukizi hayo”, alisema Maryam ambae pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wanaoisha na VVU Wilaya ya Chake Chake.

Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar aliwataka akinamama hao kutumia njia za uzazi wa mpango kuhakikisha wanapata muda wa kupumzika, ili mwili ujirudi katika hali nzuri.

Alisema kuwa, ipo haja ya kufuata ushauri wa daktari mara kwa mara, jambo hilo litasaidia kumkinga mtoto na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

MWISHO.