Monday, September 16

PPC yaanza kuvitangaza vivutio vya Utalii Pemba.

Yasema sababu na Uwezo wa kufanya hivyo wanao
Kuunga mkono kauli ya Rais wakiwa kama waandishi  na Wananchi ni wajibu wao


HABIBA ZARALI ,PEMBA

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya ameahidi kuendelea kutowa elimu kwa wananchi wa Wiaya hiyo juu ya umuhimu wa Utalii na kuboresha vivutio vya utalii ndani ya maeneo yao.

Alitowa ahadi hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba ‘PPC’ katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika maeneo ya makumbusho ya Haroun site , Chwaka Tumbe wilayani humo.

Alisema katika wilaya ya Micheweni kumebarikiwa na vivutio vingi vya utalii vinavyoendelea kukuwa siku hadi siku jambo ambalo ni faraja kubwa kwa wananchi na Serikali kwa ujumla katika kukuza Uchumi.

“Zamani wilaya ya Micheweni suala la utalii lilikuwa halitakiwi hata kulitaja, lakini leo hii wananchi wameshajihika vyema na wanahitaji kuwepo”,alisema.

Akivitaja baadhi ya vivutio vya utalii vilivyomo Wilayani humo alisema ni pamoja na makumbusho ya Kihistoria, mapango ya asili, fukwe zenye hadhi kubwa , mahoteli mbali mbali, misitu ya hifadhi, visiwa vyenye.ndege wa aina mbalimbali, lahaja za kipekee na mambo mbalimbali ya utamaduni.

Wakati huo huo mkuu huyo wa wilaya alisema kuimarika kwa shuhuli za Utalii ndani ya Wilaya hiyo zote hizo ni juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mwinyi za kuhamasisha uwepo wa

Utalii kisiwani Pemba na kutaka kuendelezwe kuvumbuwa vivutio vipya ili Utalii uweze kukuwa hasa ukizingatia naingiza asilimia kubwa pato la nchi.

“Niwapongeze sana Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (Pemba Press Club), kwa uamuzi wenu wa kizalendo wa kuona kuna haja ya kumuunga mkono Rais wetu wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuvitangaza na kuvitembelea vivutio vya Utalii kwa ajili ya kukuza sekta ya Utalii kisiwani mwetu, nawaomba musiishie hapa”, alisema.


Kwa upande wake Ofisa Mdhamini Wizara ya Utalii Kisiwani Pemba, Zuhura Mgeni Othman alisema Utalii katika awamu ya nane ya Uongozi wa Dk, Hussein Ali Mwinyi umeimarika kwa kiasi kikubwa jambo ambalo ndani ya Kisiwa cha Pemba kumekuwa na uingiaji wa wageni kwa shughuli za Utalii kutoka mataifa mbali mbali Ulimwenguni.

Alieleza kuwa hilo linatokana na kuwepo kwa vivutio vingi ndaia ya Kisiwa cha Pemba sambamba na kuwepo  Usafiri wa angani na Baharini ambapo  kisiwa cha Pemba kimekuwa kikipokea meli kubwa za kitalii ambazo zinakuja na watalii wengi kwa ajili ya shuhuli hizo tafauti na miaka ya zamani.

Alifahamisha Wizara ya Utalii imekuwa na mashirikiano makubwa na jamii pamoja na Serikali za mikoa yote miwili ya Pemba jambo ambalo limehamasisha uvumbuzi wa vivutio mbali mbali vya Utalii ambavyo wananchi wenyewe wamekuwa wakishiriki kuviibuwa na kuviripoti kweye Wizara.

Mdhamini huyo aliipongeza Klabu ya Waandishi wa habari Kisiwani Pemba kwa kuendeleza ushirikiano na Wizara ya Utalii na Mambo ya kale Pemba kwa kuamuwa kuvitembelea, kuvitangaza vivutio hivyo sambamba na kuunga mkono kauli za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi  la kukifunguwa kisiwa cha Pemba kiuchumi kupitia sekta ya Utalii.

“Wanachama na Uongozi wa Klabu ya Waandishi wa habari Pemba ( Pemba Press  Club) kwa niaba ya Wizara yangu ya Utalii niwaambie ahsanteni sana kwa uamuzi wenu muliofanya ya kutaka tushirikiane  kuutangaza Utalii wa kisiwa cha Pemba,”alisema Mdhamini huyo.

Alifahamisha  kuwa wa wamefarajika sana kuona kundi la wanahabari limeamuwa kufanya kazi ya Kizalendo ya kutangaza nchi yao kwa ajili ya kukuza Uchumi wa nchi kwa kutangaza vivutio vya Utalii  na kuwataka Waandishi hao kupitia Klabu ya Waandishi wa habari waendelee kufanya hivyo kwa kauli moja ‘kazi iendelee”,

Zuhura alieleza kuwa mbali na Waandishi kuvitembelea na kuvitangaza vivutio vya Utalii Pemba  lakini pia ata wao  wamepata fursa ya  kufanya Utalii wa ndani, na Wizara hiyo itaendelea kundi hilo muhimu la Waandishi wa habari kutika kuunga mkono Azma ya Rais wa Zanzibar ya kukiinuwa kisiwa cha Pemba Kiuchumi kupitia sekta ya Utalii kwa kadri hali itakavyoruhusu.

Nae Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Pemba  (Pemba Press Club) Bakar Mussa Juma  wakati akizungumza na Waandishi wa habari huko katika eneo la kivuti cha utalii la Pango la kijiji Makangale  alisema klabu yao imekusudia kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi  ya kukiunuwa kisiwa cha Pemba kiuchumi ikiwemo sekta ya Utalii.

Alieleza kuwa Klabu ya Waandishi wa habari inao wajibu, haki na sababu ya kufanya hivyo kwanza wao ni wananchi pia wanayorasilili na uwezo wa kuvitangaza vivutio vya Utalii vilivyopo Pemba kwa vile Klabu inaraslimali kubwa ya Vyombo vya habari vingi ambao wafanyakazi wake
ni wanachama wa Klabu hiyo.

Alifahamisha Klabu ya Waandishi wa habari Pemba ( PPC) itaendelea kufanya hivyo kwakushirikiana na Wizara ya Utalii na mambo ya kale Pemba , hatuwa kwa hatuwa kwani Uchumi unapokuwa wanaofaidika ni wananchi na waandishi pia wamo katika kundi hilo kwa vile ni wananchi na wanahitaji mambo mbali mbali ikiwemo miundo mbinu ya maendeleo na Mishahara.

“Mimi nikiwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Pemba( Pemba Press Club) niwaambie kuwa hili tunalolifanya tunawajibu wa kulifanya na halina mjadala , leo tumeanza ziara hii kwa Wizara ya Utalii lakini hatutasimama muda wowote Wizara hii ikiwa tayari kushirikiana nasi tutafanya hivyo”, alisema.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema sio kwamba Wizara ya Utalii imependelewa na Klab ya Waandishi wa habari ya Pemba kupewa ushirikiano wa kutangaza kazi zao za Utalii, lakini Wizara hiyo imetaka ushirikiano  na Klabu hiyo.

Alifahamisha iwapo kuna taasisi ama Wizara inataka kushirikiana na Klabu hiyo basi milango iko wazi kwa kutangaza maendeleo yalioko Pemba ambayo yamefanywa na Serikali iliopo madarakani.

“Niseme kuwa Wizara ya Utalii imewasha moto kwa kuamuwa kushirikiana na Klabu yetu kutangaza kazi zake, lakini moto huu hautazimika tuko tayari kushirikiana na taasisi na wizara yoyote kuyatangaza maendeleo yao yaliomo katika taasisi zao “, alieleza.

Kwa upande wake Ofisa msimamizi uhifadhi eneo la Chwaka Tumbe Abdulrahman  Said Khamis  alisema ni vyema wananchi kufika katika vivutio hivyo kwani vinaonesha tawala zilizokuwepo kabla ya Mapinduzi na historia na tamaduni zake.

Kwa upande  wake Msaidizi meneja wa hoteli ya Mantarif ilioko Makangale  Haji Khamis Ali alisema sekta ya utalii imepiga hatuwa kubwa tofauti na hapo awali kutokana na wakaazi wa maeneo ya karibu na hoteli wameanza kuelewa maana ya Utalii na kuwa na mashirikiano makubwa na wawekezaji.

Alisema mashirikiano hayo yamewawezesha jamii kusaidiana kwa hali na mali pale wanapotokewa na shida na wawekezaji wa mahoteli yaliokaribu nao kama vile Manta reef Hotel .

Akitaja faida wanazopata wananchi hao kupitia utalii ni pamoja na kupata ajira, jamii kuuza bidhaa zao mbalimbali kupitia sera ya Utalii kwa wote na wafanyakazi wanaofanyakazi katika Hoteli hiyo  hujifunza lugha mbalimbali.

“Sisi kama Wawekezaji tumekuwa na mashirikiano makubwa na jamii ya hapa Makangale na tumekaa kama ndugu tunasaidiana kwa mambo mbali mbali ya kibinaadamu na kijamii”, alisema.

Nae mwananchi wa kijiji cha  Makangale Fatma Mohamed na Ased Ali Said walisema wanajivunia kuwepo vivutio vya utalii katika maeneo yao wanayoishi na kuiomba serikali kuboresha miundombinu hasa ya barabara na kuviboresha vivutio hivyo ili wageni waweze kuwa na urahisi wa kuyafikia.

Ziara ya Klabu ya Waandishi habari Pemba ( Pemba Press Club) imefanya ziara hiyo kwa nia ya kuunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk, Hussein Ali Mwinyi ya kukiinuwa kisiwa cha Pemba kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo  Utalii.

            MWISHO.