Wednesday, January 8

DC Micheweni awataka akinamama kutumia uzazi wa mpango kuimarisha afya zao, watoto

NA ZUHURA JUMA  – PEMBA

MKUU wa Wilaya Micheweni Mgeni Khatib Yahya amewataka akina mama wa vijiji vya shehia ya Tumbe Mashariki kujiunga na uzazi wa mpango, ili kuwanyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili kamili kwa ajili ya kujenga familia bora.

Akiuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo katika uzinduzi wa utowaji wa elimu ya afya na lishe alisema, uzazi wa mpango ni muhimu katika makuzi bora ya mtoto na mama.

Alisema kuwa, suala la uzazi wa mpango kwa akina mama ni jambo muhimu sana kutokana na hali zao, kwani linawafanya watoto kuwa na afya njema, akili nzuri pamoja na makuzi bora sambamba na yeye kuimarisha afya yake kwa kupata mapumziko.

‘’Mama anapopumzika baada ya kujifungua anapata muda wa kupumzika, hivyo afya yake inaimarika na mtoto anapata kukua vizuri,’’ alisema Mkuu huyo.

Aidha alieleza kuwa, lishe bora kwa mama na mtoto inahitajika zaidi, hivyo ni vyema kutumia vyakula vya mboga na matunda kwa kujenga afya iliyobora kwa watoto wao.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali aliwataka akinamama hao kuvitumia vituo vya Afya kwa ajili ya kupata matibabu, kwani huduma zimeboreshwa vituoni humo.

‘’Serikali imeimarisha huduma za afya mjini na vijijini ili kusudi mupate huduma bora, hivyo akina mama ni muhimu kufika kwenye vituo vya afya kupata maelekezo mbali mbali kwa ajili ya kuimarisha afya zenu,’’ alifahamisha.

Alisema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu hiyo vijijini kwa lengo la kuwasaidia akina mama kujua umuhimu wa afya ya uzazi na lishe bora kwa watoto na wajawazito.

Mwananchi Omar Hassan Suleiman na Riziki Amour Ali walisema, suala la uzazi wa mpango na lishe lina umuhimu mkubwa katika familia, kwani linamfanya mtoto kukuwa vizuri na kumkinga na maradhi mbali mbali ikiwemo utapia mlo na safura.

Akitoa elimu ya upandaji wa mboga muhudumu wa Afya ya jamii Rashid Khatib Hamad alisema, ni vyema wanajamii kupanda mboga kwenye viroba, ajili ya kujipatia virutubisho katika mwili.

Zoezi hilo la utowaji wa elimu ya Afya yangu vijijini limezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, ambapo vijiji kumi vya shehia za Tumbe zitafikiwa kupatiwa elimu hiyo.

                                                 MWISHO.