Na Mukrim Mohammed
Benki ya Exim Tanzania imesisitiza dhamira yake kuhudumia wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ndani na nje ya nchi ili kuunga mkono na kwenda sambamba na kasi pamoja na dhamira ya serikali katika kuchochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu.
Afisa Mtendaji wa Benki ya Exim Bw Jaffari Matundu alitoa ahadi hiyo mbele ya Raisi wa Zanzibar Dr. Hussein Mwinyi alipotembelea banda la benki hiyo kwenye Mkutano wa pili wa wadau wa sekta utalii Zanzibar (Z -Summit) unaofanyika visiwani humo hii leo.
Kwa mujibu wa Bw Matundu, kufuatia jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuendeleza sekta ya utalii, Benki ya Exim imewekeza zaidi katika kuwahudumia wadau wa sekta hiyo ili waweze kunufaika na jitihada hizo za serikali kupitia huduma mbalimbali za kifedha zinazotolewa kwa kuzingatia mahitaji mahususi ya wadau hao.
“Udhamini wetu mkuu kwenye mkutano huu ikiwa ni mara ya pili mfululizo ni uthibitisho wa wazi kabisa katika kuthibitisha dhamira yetu hiyo muhimu. Kupitia ushirikiano wetu na Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI) tumeweza kutoa suluhisho za kifedha kwa wanachama wake pamoja na wadau wengine. Ushirikiano huu unadhihirisha msaada endelevu wa Benki ya Exim kwa sekta muhimu za uchumi, haswa sekta ya utalii ya Zanzibar.’’ Alisema.
Kwa mujibu wa Bw Matundu, kupitia mchanganyiko wa teknolojia na ujuzi, benki hiyo inatoa huduma mbalimbali ambazo zimekuwa na athari chanya kwa wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo wanawake na vijana wajasiriamali.
“Uaminifu wetu katika kutoa viwango vya ushindani katika huduma mbalimbali umekuwa ukiwahakikishia wateja wetu kupata huduma nzuri bila vikwazo. Zaidi jitihada zetu katika utoaji wa mikopo ili kukuza mitaji ya wadau wa sekta ya utalii zimeendelea kuleta tija zaidi sio tu kwa wadau hawa bali pia hata kwetu kama benki.’’
Akizungumza kwenye Mkutano huo Rais Mwinyi pamoja na kuwapongeza waandaaji na wadhamini wa mkutano huo, alisema serikali hiyo imejipanga zaidi katika kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, umeme, maji na viwanja vya ndege ili kuandaa mazingira yanayoweza kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii visiwani humo.
Aidha Rais Mwinyi aliendelea kutoa wito kwa raia wazalendo visiwani humo kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii ili waweze kufaidi matunda ya uwekezaji unaoendelea kufanywa na serikali katika kukuza na kuboresha sekta hiyo.
“Ni hivi karibuni tu tumepitisha Sheria mpya ya Uwekezaji ya mwaka 2024 ambayo inatoa vivutio vingi katika sekta ya utalii na maeneo mengine. Kupitia sheria hii wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii wanalindwa vema na zaidi sheria hii inaambatana na vivutio mbalimbali kwenye eneo la kodi,’’ alibainisha.
Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Bw Mudrick Ramadhan Soraga alisema serikali imejipanga kukuza maendeleo jumuishi na endelevu katika sekta ya utalii sambamba na kuwasaidia wawekezaji wadogo na wakubwa katika sekta hiyo.
Awali akizungumza kwenye Mkutano huo Mwenyekiti wa ZATI Bw Rahim Bhaloo alisema mkutano huo uliofanikiwa kuvutia wadau zaidi ya 600 unaofanyika kwa mara ya pili visiwani humo unalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo watoa huduma pamoja na watumiaji wa huduma hizo lengo likiwa ni kuongeza wigo wa Zanzibar katika jukwaa la utalii kimataifa.
Mwisho.