Thursday, November 14

“Tumieni kalamu zenu kutetea sheria ya habari zenye mapungufu” Shifaa Said

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea kutumia kalamu zao kufanya utetezi wa wa sheria ya habari zenye mapungufu ili zifanyiwe maboresho.
Akifungua mafunzo ya siku mbili katika Ofisi ya TAMWA Chake Chake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchechemuzi na utetezi kutoka TAMWA Shifaa Said Hassan alisema iwapo waandishi wataendelea kutumia kalamu zao vizuri kufanya utetezi wa sheria hizo, itasaidia kupata sheria zilizo bora na zisizonuima uhuru wa habari.
Alisema kuwa, zipo sheria za Usajili wa Wakala wa Habari na Magazeti na Vitabu nambari 5 ya mwaka 1988 ambayo imerekebishwa Sheria nambari 8 ya mwaka 1997 na ile sheria ya Tume ya Utangazaji nambari 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa maboresho nambari 1 ya mwaka 2010, ambazo baadhi ya vipengele vyake vinanyima uhuru wa habari, hivyo kuna haja ya kufanyiwa marekebisho.
Akiwasilisha mada ya mapungufu yaliyomo kwenye Sheria hizo mwezeshaji Hawra Shamte alisema, ni kifungu cha 4 cha kuanzishwa kwa bodi ya ushauri ambacho Mwenyekiti wake huteuliwa na mamlaka ya uteuzi, hivyo kuna haja kwenye kipengele hicho wadau wapendekeze majina na kuyafikisha katika mamlaka hiyo, kwa ajili ya kuteuliwa.
“Kifungu chengine ni nambari 1 kinachompa mamlaka Waziri kwa amri iliyoandikwa anaweza kumtaka mwenye leseni yeyote kutangaza…, na pia tume ya Utangazaji isiachiwe kufanya kazi yeyote bali kifungu kieleze kazi maalumu ambayo itafanya” alifafanua muwasilishaji huyo.
Aidha aliwataka waandishi wa habari kuendelea kuzisoma Sheria hizo, ili kufahamu vipengele ambavyo vinaendelea kunyima uhuru wa wanahabari, jambo ambalo litasaidia katika utetezi.
Nao waandishi walioshiriki  mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo kwani wao ndio waathirika wakubwa wanaokandamizwa na sheria hizo
Mafunzo hayo ya siku 2 yaliwashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali kisiwani pemba yenye lengo la kutetea sheria kandamizi za habari, ili zifanyiwe marekebisho.
                   MWISHO.