Friday, December 27

MABADILIKO TABINCHI NI AJENDA YA KIDUNIA-RC MATTAR

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema suala la mabadiliko ya tabinchi kwa sasa ni ajenda ya kidunia, kwani dunia kwa sasa inapita katika changamoto kubwa ya mazingira magumu sana juu ya suala hilo.

Alisema hayo hayajatokezea bali ni mchakato wa muda mrefu ambao binaadamu wamefanya, kila mtu kwa nafasi yake lakini pia wapo waliochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati akizungumza na wanachama wa Pemba Press Club, wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani yaliyoandaliwa na PPC kwa ufadhili wa utpc, maadhimisho yaliyofanyika mjini Chake Chake.

Alisema zipo nchi zenye viwanda vikubwa duniani, ndio zinazochangia uchafuzi wa mazingira kutokana na moshi unaotoka viwandani humo.

“Nasisi kwa nafasi zetu tumekata miti kwa shuhuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii, bahati mbaya baada ya dunia hii tulionayo hatuna nyengine mbadala na hii tumeshaiharibu,”alisema.

Aidha alisema wakati umefika wa kufanya jitihada za kurekebisha tulipoharibu, kwa kupanda miti na kurithisha kijani kilichopo kwa vizazi vinavyokuja.

Hata hivyo alisema ni wakati wa kuwafahamisha Watoto majumbani, skuli juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kwa kupanda miti katika maeneo mbali mbali ikiwemo miti ya matunda na kivuli.

Alisema waandishi wa habari wananafasi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya suala zima la uhifadhi wa mazingira, ikizingatiwa mabadiliko ya hali ya hewa, mvua za mara kwa mara, kiangazi kisichotarajiwa kinachotokea.

Mkuu huyo alisema ni wakati wakuwatengeneza Watoto katika suala zima la uhifadhi wa mazingira, kwani wakipatiwa elimu basi watakua walimu kwa wenzao.

Aidha mkuu huyo aliwataka waandishi hao kuandika habari za uchunguzi ambazo zitasaidia jamii kwa kiasi kikubwa, ambazo zitaleta matokeo mazuri kwa wananchi.

Mwenyekiti wa PPC Bakar Mussa Juma, alisema hakuna asiejua kama mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri, hususan ndani ya kisiwa cha Pemba, kwani Zaidi ya maeneo 48 yanaingia maji chumvi na matuta Zaidi ya sita, yamejengwa kuzuwia maji hayo kuvamia mashamba ya wakulima.

Aliwataka wananchi kuhifadhi mazingira, kwani kasi ya ukataji wa miti imekua kubwa kuliko uhifadhi wamazingira, pamoja na kasi ya upandaji wa miti ikiwa ndogo.

WANACHAMA WA PEMBA PRESS CLUB, WAKIPANDA MITI AINA YA MIKANDAA KATIKA ENEO LILILOHARIBIWA NA MAJI CHUMVI HUKO KAMBINI KICHOKOCHWE WILAYA YA WETE

Nae katibu wa kamati ya uhifadhi wa mazingira shehia ya kambini Kichokochwe Bakar Suleiman Juma, alipongeza PPC kwa kushiriki kikamilifu zoezi la upandaji wa miti, ili kuhifadhi mazingira ambayo yamekua yakiharibiwa kwa muda mrefu.

Alisema watu wa ukanda wa mashariki ni waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi, kutokana na bahari kuwa karubu sana, na uharibifu wa mazingira ni mkubwa sana.

“Jambo lolote kama waandishi wa habari hawajaliunga mkono basi linaweza kuwa sio sahihi, sisi watu wakambini tuko pamoja na nyinyi katika suala la uhifadhi wa mazingira,”alisema.

Jumla ya miti elfu kumi imepandwa katika zoezi la upandaji wa miti huko kambini kichokochwe Wilaya ya wete, ambapo kauli mbiu ya ujumbe wa siku ya uhuru wa habari duniani ni “WAANDISHI WA HABARI NA MABADILIKO YA TABI NCHI”.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari portal.
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355