Friday, December 27

PPC, CFP WAPANDA MITI ZAIDI ELFU KUMI ILI KUHIFADHI MAZINGIRA

MWENYEKITI wa PPC Bakar Mussa Juma alipokea megu za miti ya mikandaa kutoka kwa mkurugenzi wa CFP Pemba Mbarouk Mussa kwa ajili ya kupanda eneo lililoathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi, huko kambini kichokochwe.

   NA HANIFA SALIM, PEMBA.

KLABU ya Wandishi wa habari Pemba (PPC) kwa kushirikiana na taasisi ya uhifadhi wa misitu ya jamii Pemba (CFP) na jumuiya ya uhifadhi wa mazingira shehia ya Kambini Kichokochwe, imepanda miti ya Mikoko zaidi ya 10,000 kwa lengo la kurejesha uwoto wa asili.

Miti hiyo iliopandwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ilioadhimishwa na Klabu ya wandishi wa habari Pemba (PPC) ikiwa ni muitikio wa kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu isemayo ‘Wandishi wa habari na mabadiliko ya tabia nchi”.

Akizungumza na wadau mbali mbali walioshiriki katika shuhuli hiyo ya upandaji wa miti huko katika eneo la Kambini Kichokochwe Mwenyekiti wa Klabu ya wandishi wa habari Pemba, Bakar Mussa Juma alizitaka taasisi hizo kuendelea kuishajihisha jamii juu ya suala zima la upandaji wa miti.

Alisema, mabadiliko ya tabia nchi yalikuwa yakizungumzwa kutokea
mataifa ya mbali Duniani, lakini kwa sasa Pemba tayari yamefika ambapo yapo zaidi ya maeneo 48 ambayo tayari yameshavamiwa na maji ya chumvi huku wananchi wakikosa maeneo ya kilimo.

Aidha Mwenyekiti huyo alisema, mbali na hilo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kupiga matuta ya kuzuwia maji ya chumvi yasiingie katika makaazi ya watu na mashamba ambapo jumla ya matuta sita yamepigwa Pemba, fedha ambazo zingefaa kwa shuhuli nyengine za kijamii.

“Sasa hivi Kisiwa cha Pemba tayari kumekuwa na athari ya mabadiliko ya tabia nchi, maji tayari yanapanda kwenye maeneo ya kilimo na makaazi ya watu, sisi wandishi tuzimie kalamu na sauti zetu kuihamasisha jamii juu ya upandaji miti ili kukabiliana na janga hili”, alisema.

Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa, ni vyema sasa wananchi kuifanyia kazi kampeni ya serikali ambayo ilikuwepo miaka ya nyuma ya “Panda mti kata mti’ ili kunusuru jangwa katika maeneo mbali mbali kutokana na upotevu wa miti.

Alisema, PPC imeamuwa kupanda miti hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kwa dhamira ile ile ya kuhifadhi mazingira kwani Kisiwa cha Pemba ni miongoni mwa waathirika wa mabadiliko tabia nchi na wandishi nao ni sehemu ya jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya uhifadhi wa misitu ya jamii Pemba (CFP) Mbarouk Mussa Omar aliipongeza Klabu hiyo kwa uamuzi wao kupanda miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.


Alisema, suala la uhifadhi wa mazingira linamuhusu kila mmoja hivyo ni vizuri jamii ikawa na tabia kama hiyo ya kupanada miti ya misitu na matunda kwani ndani yake  munapatikana mafanikio mengi ikiwemo malipo kwa Mwenye-ezi Mungu kwani ni jambo la ibada pia.

Alieleza kuwa, CFP itaendelea kushirikiana na PPC katika kuona inahamasisha jamii juu ya suala zima la uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko tabia nchi kwa vile waandishi wanasauti kubwa inayofika kwa jamii kwa haraka sana.

Alisema, sasa hivi mvua inaendelea kunyesha lakini hali ya joto limekuwa na ujazo mkubwa jambo ambalo linachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi hususani kwa kukata miti ovyo.

“Suala la mabadiliko tabia nchi linamuathiri kila mmoja, sio kwa wavuvi, wala wakulima pekee hata wandishi lina wakumba hivyo
ushirikiano wenu kwetu ni muhimu sana”, alisema.

Kwa upande wao, wananchi wa jumuiya ya Uhifadhi ya mazingira shehia ya Kambini Kichokochwe Wilaya ya Wete, walisema, mashirikiano hayo ambayo waliyapata kutoka kwa wandishi wa habari ni njia moja wapo ya kupata mafanikio.

Nae  Katibu wa uhifadhi ya shehia ya Kambini Bakar Suleiman Juma alisema, waandishi wamekuwa na mchango mkubwa katika kusukuma mbele mambo mbali mbali hivyo, zoezi hilo limetowa mwanga mkubwa kwa wananchi wa Kambini Kichokochwe.

Hivyo aliiomba jamii kuwa tayari kulinda , kuhifadhi mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwani athari zake zimekuwa kubwa.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya habari Duniani ni ‘VYOMBO VYA HABARI NA CHANGAMOTO YA MABADILIKO TABIA NCHI’

                         MWISHO.