Friday, December 27

UJENZI WA KITUO JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI PEMBA KUGHARIMU BILIONI 9.8

 

MWANASHERIA wa Mahakama Tanzania Chuka Hassan Chuka (kushoto) na Mkurugenzi wa Deep Constraction Ltd Rabinder Singh Jamal, wakibadilishana mkataba wa ujenzi wa kituo Jumuishi cha utoaji haki Pemba, hafla iliyoshuhudiwa na viongozi mbali mbali kutoka Mahakama ya Tanzania na Jaji mkuu wa Zanzibar na kufanyika mjini Chake Chake

  MAHAKAMA ya Tanzania imetiliana saini na Kampuni ya Deep Constitution Limited, ya ujenzi wa kituo jumuishi cha utoaji haki Pemba, chini ya usimamizi wa Mkandarasi Rabinder Singh Jabbal.

Akizungumza katika hafla hiyo huko ukumbi wa Mamlaka ya mapato Zanzibar ZRA Gombani Chake chake, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla alisema, tukio hilo ni la kihistoria ambalo limekwenda kufanyika Pemba ambalo linaonesha uimara wa Muungano uliopo.

Alisema, kuna kila sababu ya kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kusimamia na kudumisha Muungano wa serikali hizo mbili.

Alieleza, Majaji wa mahakama za rufaa kutoka Tanzania kuja Zanzibar kusikiliza mashauri katika mahakama za Zanzibar ambazo mazingira yake sio mazuri hivyo, msaada wa mahakama ya Tanzania kujenga kituo hicho kutaboreha mazingira bora ya utendaji wa kazi zao za kila siku.

JAJI Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla akizungumza mara baada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa kituo jumuishi cha utoaji haki Pemba, baina ya Mahakama ya Tanzania na kampuni ya Deep Constraction Ltd, hafla iliyofanyika mjini Chake Chake.

“Sasa hivi tumekusudia kuboresha utendaji wetu wa kazi za mahakama, tunajenga mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, mahakama ya Wilaya Konde na Mkoani, kwa bahati nzuri na hii mahakama ya Rufaa itakayojengwa tutakua na majengo manne mazuri na ya kisasa”, alisema.

Aidha alisema, majengo hayo yatakwenda sambamba na usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia na mfumo wa kurikodi, jambo ambalo litarahisisha utendaji wa kazi za mahakama kwa urahisi zaidi.

Kwa upande Mtendaji Mkuu wa mahakama ya Tanzania Prof: Elisante Ole Gabriel alisema, jengo hilo litagharimu zaidi ya shilingi Billioni 9.8 na endapo kutapatikana unafuu wa kodi litagharimu zaidi ya shilingi Billioni 7.8.

MTENDAJI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Jaji Profesa Elisante Ole Gabriel, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa kituo Jumuishi cha utoaji haki Pemba, baina ya Mahakama ya Tanzania na kampuni ya Deep Constraction Ltd, hafla iliyofanyika mjini Chake Chake

“Kazi hii inatakiwa kufanyika kwa muda wa miezi tisa na inatakiwa kukamilika ifikapo February 23 mwaka 2025, tunaamini kwamba Mkandarasi hatoingia katika mtego wowote wa kukwamisha muendelezo wa mradi huu ni imani yetu utakamilika kwa wakati”, alisema.

Mtendaji mkuu wa mahakama Zanzibar Kai Bashiru Mbarouk alisema, serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zinaziangalia mahakama kwa jicho stahiki, pamoja na kufanya kila juhudi kuziwezesha ili ziweze kufanya kazi zake kwa uwazi na bila kuingiliwa.

Alisema, mahakama ya Zanzibar na Tanzania zimekua katika mashirikiano ya miaka mingi ambapo miaka hii ya karibuni ushirikiano huo umekua ukiongezeka mara dufu, katika maeneo tofauti ikiwemo kujenga uwezo, kujenga mifumo ya kieletroniki ya usimamizi wa mashauri na kufaidi maarifa na juhudi kutoka kwa wenzao wa Tanzania.

Msajili Mkuu wa mahakama Tanzania Eva Nkeya alisema, kituo hicho kitakua na mahakama za ngazi tofauti, ambapo kwa upande wa mahakama ya rufaa itaweza kuja kufanya vikao vyake Kisiwani Pemba.

AFISA Mdhamini Ofisi ya Rais Katiba sheria utumishi na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali, akifuatilia hafla ya utiaji wa saini mkataba wa ujenzi wa kituo Jumuishi cha utoaji haki Pemba,hafla iliyofanyika mjini Chake Chake

“Hii itawasaidia wananchi wa Kisiwa cha Pemba katika kupunguza gharama za kutafuta huduma za mahakama, sisi tunaahidi kama watendaji kufanya kazi hiyo, kuwepo kwa mahakama hii itawafanya wananchi waendelee kutumia muda wao katika shuguli za ujenzi wa taifa”, alisema.

Akitoa maelezo mafupi ya mradi huo Mkuu wa kitengo cha maboresho Tanzania Jaji Dkt. Rumsha alisema, ujezi wa kituo hicho unakidhi kiu ya wananchi wa Kisiwa cha Pemba, kwani kitakua na ukubwa wa mita za mraba mita 3,782, gorofa nne, nyumba za walinzi, chumba cha jenereta, mgahawa na ofisi za watumishi wa utoaji haki.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Deep Constitution Limited ya Morogoro Rabinder Singh Jabbal aliahidi mradi huo kumalizika kwa wakati ambapo alisema, changamoto ndogo ndogo ambazo zitajitokeza katika ujenzi huo wataweza kuzitatua ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa muda uliotakiwa.

                        MWISHO.