Thursday, December 26

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya watu wa China kwa ajili ya Maendeleo ya Wazanzibar

  MARYAM SALUM PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China katika kuleta Maendeleo hususani kwenye sekta ya Afya.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa sekta ya Afya pamoja na wananchi huko katika hospital ya Abdalla Mzee Mkoani, kwenye ufunguzi na makabidhiano wa nyumba za makaazi za wafanyakazi wa sekta hiyo.
Dk Mwinyi alisema kuwa hospital ya Abdulla Mzee Mkoani  inayo historia kubwa katika utowaji wa huduma za afya Zanzibar na hasa katika Kisiwa cha Pemba.
Alieleza kuwa historia hiyo inatokana na kuwepo kwa Ushirikiano wa dhati na wa  muda mrefu kwa watu wa Jamhuri ya watu wa china.
“Mnamo mwezi April mwaka 1969 Serikali ya Jamhuri ya watu wa china iliweza kujenga na kuizindua hospotali ya Abdulla Mzee kwa mara yake ya kwanza,huku wakiendelea kutupatia huduma ya msaada wa Madaktari wa fani mbali mbali na vifaa vya huduma vya Afya kwa zaidi ya miaka 54 sasa, ili kuimarisha huduma za afya,”  alieleza Dk Mwinyi.
Alifahamisha kuwa mnamo mwaka 2016 Serikali ya watu wa china ilifanya ukarabati mkubwa wa majengo yote ya hospital hiyo na kuifikisha katika kiwango cha ubora uliopo sasa, ambapo katika kuendeleza azma yao hiyo yakusaidia utowaji wa huduma za afya Serikali ya watu wa china walitoa ahadi zao kujenga nyumba za wafanyakazi.
“Kwa hakika ahadi hiyo imetekelezwa kwani azma hiyo yakujenga makaazi kwa wafanyakazi karibu na hospital inalengo la kuwapunguzia masafa ya watoa huduma wa Afya na kuboresha huduma na matibabu kwa wananchi “, alieleza.
 Alisema ipo kila sababu yakuishukuru na kuipongeza Serikali ya watu wa China kuunga mkono vipao mbele muhimu vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hususani katika sekta ya fya.
Aidha Dk Mwinyi alieleza kuwa licha ya nyumba hizo za makaazi kwa wafanyakazi wa hospital ya Abdalla Mzee, pia kipindi kifupi kijacho wataweka mawe ya msingi ya nyumba nyengine kwa wafanyakazi katika hospitali za Wilaya kwa Pemba na Unguja.
“Baada ya kukamilika kwa miradi hiyo kutakuwa kumeweza kuondosha kwa kiasi kikubwa tatizo la kukosekana kwa makaazi ya watumishi wa Afya kunakosababisha kuzorota kwa utowaji huduma kwa wakati katika hospital zetu,” alisema Dk Mwinyi.
Alisema kuwa jumla ya shilingi bilioni 16 za kitanzania . bilioni 5 zimeweza kutumika katika kujenga nyumba nne za ghorofa, ambapo nyumba hizo zitawahudumia familia 76 zikijumuisha nyumba 52 za chumba kimoja,na nyumba 24 za vyumba viwili.
Alifahamisha kuwa ni mategemeo ya Serikali kwamba makaazi hao yatatoa fursa kwa wafanyakazi wa sekta hiyo kuweza kupata kufanya kazi na muda wa kupumzika badala yakufikiria usafiri wa kwenda na kurudi masafa ya mbali.
Dk Mwinyi alitoa wito kwa Uongozi na watakaoishi katika nyumba hizo kuhakikisha wanazitunza na kuzingatia kwamba gharama zilizotumika katika kujenga majengo hayo nikubwa.
Aliwataka kuweka utaratibu uliomzuri wakuzifanyia marekebisho kwa wakati stahiki ili ubora wake uendelee na kudumu kwa muda mrefu.
Nae Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui ,alisema kuwa Jamhuri ya watu wa China ni sawa na familia sasa kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Alisema kuwa hiyo inatoka na Ushirikiano baina ya nchi mbili hizo kwani ni makubwa na wa muda mrefu sasa.
” Kujengwa kwa nyumba za makaazi kwa wafanyakazi ni moja kati ya Maendeleo muhimu na hiyo ni ushirikiano baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya watu wa china katika sekta ya Afya zanzibar,” alisema.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imekuwa mbele katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta Maendeleo.
Alifahamisha kuwa hospital ya Abdalla Mzee kwa sasa inawafanyakazi 143,wa kada mbali mbali  wakiwemo Madaktari bingwa 6.
Waziri Mazrui alitoa wito kwa wafanyakazi watakaopata nafasi yakuishi nyumba hizo, kwa mujibu wa utaratibu utakao pangwa kuzitunza ili lengo liweze kufikiwa.
Wakati akisoma taarifa ya kitaalamu ya Mradi huo, Katibu mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dk, Habiba Hassan Omar alieleza kuwa hospital ya Abdalla Mzee ambayo ilijengwa kwa msaada wa watu wa China mwaka 1971 na kufanyiwa matengenezo na kuzinduliwa mwezi Novemba mwaka 2016.
“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwakushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya watu wa  China zilikubaliana kujenga nyumba za makaazi ya wafanyakazi karibu na hospital ili kuwapunguzia masafa wafanyakazi ili waweze kuendesha huduma na matibabu kwa wananchi kwa wakati,” alisema
Alisema kuwa Mradi huo umejengwa kwa msaada kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China na Mkandarasi Zanchain group na kigharimu RMB 47 na tisiini elfu, ambazo ni sawa na bilioni 16 milioni mianane thamanini na moja na lakini tano za kitanzania.
Alifahamisha kuwa ujenzi huo unahusisha majengo manne,mablok matatu ya gorofa tatu kwa kila moja na jengi moja  la ghorofa nne na ndani yake zikihudumia familia 76.
Hivyo Mradi huo utaweza kutoka fursa kwa kuimarisha huduma za afya Kisiwani humu,kwani kulikuwa na kilio kikubwa kwa watoa huduma kwani Serikali ilikuwa unatumia gharama kubwa kwakuwakodia nyumba Madaktari katika mji wa Chake Chake ambazo zilikuwa zinagharimu zaidi ya shilingi milioni mia moja kwa mwaka.
Akitoa salam za Mkuu wa Mkoa kusini Mattar Zahor Massoud alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya China inalengo la kuhakikisha inawapatia wananchi Maendeleo.
Sambamba na hilo aliwataka wananchi kuthamini jitihada zinazofanywa ili Maendeleo yaweze kupatikana zaidi nchini.
Mapema Balozi mdogo wa china Zhang Ming  akisoma taarifa alisema kuwa ufunguzi wa miradi hiyo ni ahadi iliwekwa na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujenga nyumba hizo ili kuwaondoshea usumbufu  wafanyakazi wanaotoka masafa ya mbali.
Hivyo aliwataka wafanyakazi watakaopata nafasi yakuishi katika nyumba hizo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kutoa huduma  kwa wakati.
MWISHO.