Sunday, November 24

WAFUGAJI NYUKI PEMBA WAPATIWA MAFUNZO JUU YA MABADILIKO TABIA NCHI NA KALENDA YA UFUGAJI WA NYUKI

BAADHI ya washiriki wa mafunzo ya Mabadiliko ya Tabia Nchi na Kalenda ya Ufugaji wa Nyuki Kisiwani Pemba, wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo, yaliotolewa na wakala uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar na Kufanyika Pujini Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA ZEEA)

  NA ABDI SULEIMAN.

AFISA Mafunzo na miradi ya Uwezeshaji, wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ofisi ya Pemba Fatma Ali Salim, amesema wakati umefika kwa wafugaji wa nyuki Kisiwani Pemba, kuwa na utayari katika ufugaji, ili kuweza kufikia malengo yao kiuchumi.

Alisema wafugaji wanapokua tayari katika ufugaji, na kuweka mbele imani yao kwa wakala uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA) katika kuwawezesha kiuchumi, basi wataweza kufikia malengo ya jamii, serikali na hata mtu mmoja mmoja.

Aliyaeleza hayo wakati akizungumza na wafugaji wa nyuki Kisiwani Pemba, katika mafunzo ya mabadiliko ya Tabia Nchi na Kalenda ya ufugaji Nyuki, yalioandaliwa na ZEEA na kufanyika Pujini Wilaya ya Chake Chake.

“ZEEA ni taasisi iliyojikita na uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwa wananchi hao wamejijenga katika miradi ya mtu mmoja mmoja ama miradi ya vikundi,”alisema.

AFISA Mafunzo na miradi ya Uwezeshaji kutoka wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ofisi ya Pemba Fatma Ali Salim, akizungumza na wafugaji wa nyuki wakati wa mafunzo ya mabadiliko ya Tabia Nchi na kalenda ya Ufugaji wa nyuki, yaliotolewa na ZEEA na kufanyika Pujini Wilaya Chake Chake.(PICHA NA ZEEA)

Aidha alisema ZEEA imeamua kuwapatia mafunzo hayo, kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji wa nyuki, ili waweze kupata mafanikio kutokana na shuhuli zao wanazozifanya za ufugaji wa nyuki.

Alisema mafunzo hayo yamekuja kufuatia tathmini ambayo wameifanya mwaka huu, na kuona wafugaji wengi wa nyuki wanalalamikia namna gani mizinga yao ya nyuki inashika nyuki na baada wanatoka.

Aliongeza kwamba athari za mabadiliko Tabia nchi, ndio kitu kinachopelekea kutokuingia kwa nyuki au kutokuzalisha asali baada ya nyuki kuingia katika mizinga na kuhama kwa muda.

“Mafunzo haya yanaendana na kalenda ya ufugaji wa nyuki, ili wafugaji waweze kujipanga kwa kujua kipindi, muda na miongo ipi wanaweza kutega mizinga kwa ajili ya kuzalisha makundi, kipindi gani wanakagua na kusafisha na kujua ni muda wa kuvuna asali.

Nae mkufunzi wa mafunzo hayo Khamis Dadi Khamis, alisema mada ya mabadiliko ya Tabia nchi ni muhimu kufundishwa kwa wafugaji wa nyuki, kwani inaungana moja kwa moja na kalenda ya ufugaji wa nyuki, kalenda ambayo itaondosha mizozo kwao.

Alisema kila mfugaji wa nyuki anapaswa kuendana na kalenda yake, kwa shuhuli zake anazozifanya kwa mwaka mzima, katika ufugaji wa nyuki.

“Ukitizama dhana hali ya mafunzo yetu yanagusa moja kwa moja na dhana ya hiyo, kwani wafugaji wanakua wameshajipangia katika shuhuli zake,”alisema.

Aidha alifahamisha kuwa wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuhusisha dhana ya ufugaji wa nyuki na hali halisi ya mabadiliko tabia nchini.

Hata hivyo aliwasihi wafugaji wa nyuki wakati wanapotaka kufuga, kuzingatia suala zima la hali ya hewa, ili kuweza kupata mazao mazuri na yaliokua bora.

MKUFUNZI wa mafunzo ya mabadiliko ya Tabia Nchi na kalenda ya Ufugaji wa Nyuki Pemba Khamis Dadi Khamis, akiwasilisha mada kwa wafugaji wa nyuki kutoka Mikoa miwili ya Pemba, mafunzo yaliotolewa na wakala Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ofisi ya Pemba na kufanyika Pujini Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA ZEEA)

Kwa upande wao wafugaji wa nyuki wamesema kupatiwa kwa mafunzo hayo ni kitu muhimu kwani sasa wataweza kutega mizinga kulingana na kalenda zao pamoja na kuangalia hali ya hewa.

Mwenyekiti wa kikundi cha Mazingira Cooperative Society Kassim Ali Omar, alisema mabadiliko ya Tabia nchi na kalenda ya ufugaji inawasaidia sana kwa kujua mfumo mzima unavoathoriwa na mabadiliko hayo.

“Unapata kujua kipindi gani kina joto sana, kipindi hiki kina baridi sana, pia mabadiliko yanaweza kusaidia uzalishaji kutokana na kluwepo kwa mauwa au mvua na nyuki wakakubali kuzalisha asali,”alisema.

Nae Mafunda Nassor Mbarouk kutoka kikundi cha Mashallah Cooperative Society, alisema mabadiliko ya Tabia Nchi yanawathiri wafugaji wa nyuki, kwani nyuki wanahama hama na uzalishaji unapungua.

Alisema hali ya hewa na miongo wanayoitumia zamani na sasa ni vitu tafauti, kwani zamani mvua zikinyesha kama inavyotakiwa lakini sasa kila kitu kimepotea.

Alifahamisha kwamba kwa sasa mvua ni za msimu lakini kwa sasa hakuna kitu, ni wakati wa kuwa na mimea inayotoa mauwa ya kudumu kwa ajili ya nyuki.

MWISHO