Thursday, December 26

WAJASIRIMALI WAFUNDWA USARIFU WA BIDHAA KIVITENDO

NA ABDI SULEIMAN

WAKALA wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Ofisi ya Pemba, imesema wazo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kuwasaidia na kuwawezesha wajasirimali Kiuchumi linafikiwa.

Hayo yameelezwa na Afisa Mafunzo na miradi ya Uwezeshaji, wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar ofisi ya Pemba Fatma Ali Salim, wakati akizungumza na wajasiriamali katika mafunzo ya usarifu wa bidhaa mbali mbali na kufanyika Kisiwani Pemba.

Alisema ZEEA inaamini kwamba wajasirimali hao wataweza kufikia malengo yao ya kujikwamua kiuchumi, kama dhamira ya Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi ilivyo.

“Wazo la Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi la kuijenga taasisi ya ZEEA, katika kuwasaidia wajasirimali litafikiwa kama wajasirimali mutaenda kuyafanyia kazi mafunzo haya,”alisema.

Aidha Afisa Mafunzo huyo kutoka ZEEA, alisema mambo mengi yamefanywa na serikali ya awamu ya nane, yote hayo ni kuwasaidia wananchi wake.

Hata hivyo aliwataka wajasirimali hao, kuwa na imani na ZEEA pamoja na SMZ, ambayo imeamua kuwapatia maendeleo na kuwanyanyua kiuchumi kupitia ujasirimali.

Mtaalamu wa kilimo biashara kutoka shirika la World Vegetable Center Judth Paul Assenga, alisema lengo la mafunzo ni kuwasaidia wanajamii ya Pemba katika kuimarisha kipato na upotevu unotokana na mazao ya mbogamboga na Viungo.

Alisema changamoto ambayo wamigundua kutoka kwa jamii na wakulima ambao wanafanya nao kazi ni kwamba wanalima kibiashara, huku sokoni baadhi ya wakati bei zinashuka na mazao kuwa mengi na kushindwa kujua la kufanya.

Alifahamisha kwamba elimu waliopatiwa wajasirimali ya kutengeneza bidhaa zinazotokana na mboga mboga itawasaidia kuondokana na upotevu wa mazao pale soko linapokua baya.

“Wakulima watajua sasa bidhaa zao za mboga mboga zinapokosa soko watajua wazifanyie kitu gani, ili wasiziwache zikaharibika kama walivyokuwa wanafanya awali,alisema.

Nae mhandisi wa Kemikali na usindikaji kutoka ZEEA Pemba Umukulthum Moh’d Yussuf, alisema lengo la mafunzo ni kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango.

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo hayo, afisa sayansi ya chakula na Teknolojia kutoka ZEEA Ahmed Nassor Masoud, alisema wameamua kuleta mabadiliko katika jamii, juu ya upotevu wa mazao yanayozalishwa kwa kisingizio cha kukosa ubora, kwa kuyaokoa matunda na kudumu kwa muda mrefu baada ya kuongezea thamani.

Nao washiriki wa mafunzo hayo, wamesema kuwa mafunzo yamewafikia wakati muwafaka, kwani muda mrefu walikuwa wakisumbuka juu ya suala la usarifu wa bidhaa zao.

Walisema kwa sasa hakutakua na mazao ya mboga mboga yatakayokwama, kwani watahakikisha wanayabadilisha kwa kuyongeza thamani, ikiwemo mazao ya Tungule, pili pili boga, karoti, Pesheni na mazao mengine.

MWISHO