Sunday, March 9

WASTAAFU WATARAJIWA WAPEWA MBINU YA KUJIKWAMUWA NA UMASKINI BAADA YA MUDA WA UTUMISHI

 PEMBA

WATUMISHI wa Umma kutoka Idara mbali mbali za Serikali ambao wanatarajiwa kumaliza muda wao wa utumishi hivi karibuni Kisiwani Pemba wametakiwa kuwa makini juu ya matumizi ya fedha ambazo watapatiwa (kiinua mgongo) ili ziweze kuwasaidia katika maisha ya baada wa Utumishi wa Umma na fedha hizo  kuwa endelevu.

Wito huo ulitolewa na  Afisa mdhamini Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala bora  Pemba Halima Khamis Ali wakati akifungua mafunzo kwa wastaafu hao katika Ukumbi wa Mikutano wa ZSSF Tibirinzi Chake Chake.

Alisema lengo la fedha ambazo watapatiwa baada ya kustaafu zikatumike kwa malengo ili ziweze kuwasaidia kuinua hali za maisha yao baada ya kumaliza muda wao wa utumishi.

Alieleza kuwa kustaafu sio mwisho wa safari, bali wajuwe  kwamba wametoka hatua moja wanaelekea hatua nyengine,hivyo waendelee kuwa na furaha kama zilivyokuwepo hapo mwanzo.

” Sisi hapa tupo katika mkusanyiko kutoka kwenye taasisi tofauti, kupatiwa mafunzo mara baada ya kustaafu, hivyo musijinyonge,musijikalifishe,musisononeke, kwani tukumbuke hapo nyuma wazee wetu walipokuwa wanastaafu hali ilikua ngumu, familia mzima ilikuwa inalia kwa kuhofia wataishi vipi baada ya kustaafu na wengine wakistaafu bila kutayarishwa, yote hayo yakileta mshituko maradhi upweke, lakini sasa yote hayo yamemaliza tunasema tunastaafu kazi hatustaafu maisha,” alisema Mdhamini.

Alifahamisha kuwa maisha lazima yaendelee na ili maisha yaendelee kila mtu anapaswa kujipanga sio kwamba mtu anastaafu kazi yake ni kulala ,kustaafu isiwafanye kama vile mumetupwa na kuifanya familia ianze kusononeka kwa sababu mama au baba ametoka kwenye utumishi hivyo wakajiona kama watakosa huduma zote ambazo wakizipata hapo mwanzo.

“Isifikie hali hiyo kwani yapo mambo mazuri ambapo kama Serikali imeandaa kwa ajili yetu hivyo tunampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa namna ambavyo anasimamia utumishi wa Umma kwa kuleta mabadiliko katika utumishi  huo tokea hujaingia mpaka mtu anangia katika kustaafu mpaka anatoka,” alieleza.

Alieleza kuwa utumishi wa umma sasa umekuwa ni utumishi ambao unasifika sana kwani una  mageuzi makubwa sana ambayo yapo katika Idara ya  Utumishi wa Umma.

Mdhamini huyo alifahamisha kuwa hapo zamani mtu akistaafu ikifikia miezi mitatu hadi mitano mstaafu hajapata fedha zake hadi kukaribia kufariki mtu hajapata stahiki yake,lakini sasa  ni mwezi tu mtu anapata stahiki zake, na zote hizo ni juhudi za Serikali ya awamu ya nane,jimsi inavyoendelea kuwajali wananchi wake.

Aidha stahiki hizo ni haki zao ambazo walichuma kwa kipindi chote ambacho mtu amefanya kazi Serikali katika utumishi wa umma.

Alisema kuwa mtu anapostaafu kila mmoja kwenye jamii atafika kutoa ushauri wake juu ya fedha hizo, hivyo ni vyema kutuliza akili na kuwa makini , kufuata ushauri ulio mzuri ili kufikia lengo la mafao hayo na siyo kuolea na kufanyia shuhuli nyengine ambazo hazina hazina ulazima.

‘’ Tumieni taasisi zenu za kifedha kwa ajili ya kuwekeza, kuweka akiba ama kujiendeleza katika kipato na hizo ndizo sehemu salama Zaidi za kuweka fedha zenu’’, alisema.

Aliwataka wasataafu hao watarajiwa ni lazima baada ya kukabidhiwa fedha hizo kutuliza akili zao kwani fedha hizo ni lazima kuwa namkakati mwengine ambao ni mbadala kwao wa maisha ili waweze kuwa na maisha mazuri zaidi.

Aidha  Mdhamini huyo aliwataka wastaafu hao watarajiwa kuhakikisha wanaendeleza kudumisha amani na utulivu kwenye jamii hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi mkuu Oktobar mwaka 2025, kwani bado wanajukumu hilo licha yakustaafu kwao.

Akiwasilisha mada  ya matayarisho ya kustaafu na maisha baada ya kustaafu muwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka taasisi ya Uhusiano Tanzania (TIA) Willium sone Fednarnd aliwataka wastaafu watarajiwa kufikiria kuekeza katika miradi mbali mbali ambayo itawakwamuwa kiuchumi na kuweza kujiptai fedha sambamba na mazoezi .

‘’ Mazoezi ni muhimu kwani yanalinda afya ya mfanyaji na kujiepusha na maradhi ya aina mbali mbali hususan wakati mukiwa hamuko katika mahangaiko mulioziwea ( Kazini)’’, alisema.

Mapema Kaimu Mkurugenzi ZSSF Pemba Omar Nasib alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo kwa wastaafu ambao wanatarajiwa hivi karibuni ni kuhakikisha kwamba wanakuwa pamoja na wastaafu.

“Kwa sababu katika kipindi cha Utumishi wastaafu hao watarajiwa walikuwa wakichangia ZSSF kwa lengo kwamba baada ya kustaafu ZSSF iweze kushuhulikia mambo yao mbali mbali,” alisema.

Alieleza ZSSF imejipanga juu ya kuhakikisha inawapatia huduma bora watumishi wote baada yakustaafu kwa wakati na kwa kiwango stahiki kwa mujibu wa sheria ya ZSSF.

Nao Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo Kheri Juma Basha na Ali Mohamed Ali waliwashauri wenzao kujikita kwenye miradi mbali mbali ikiwemo ya maendeleo kama vile ufugaji nyuki, Ng’ombe wa maziwa kwani itaweza kuinuwa kipato chao kwa haraka kwani chochote kinachotokana na ufugaji ni mali.

Hata hivyo mada mbali mbali ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na mpango mkakati kabla na baada ya kustaafu , lishe na ulaji unaofaa, msongo wa mawazo , matayarisho na taratibu ya wastaafu pamoja na Afya ya akili.

MWISHO.