Friday, November 1

RC Ayoub azindua kikundi.

 

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud, amewataka vijana kisiwani Pemba kujiendeleza kitaaluma katika fani mbali mbali, ili wawe na uwezo wa kuzitumia fursa za mabadiliko makubwa ya kiuchumi pale zitakapokuwa tayari kutekelezwa.

 

Alisema tayari serikali imesha karibisha wawekezaji tofauti kuwekeza kisiwani Pemba, kwa lengo la kuimarisha uchumi wao, hivyo haitokuwa jambo la busara kuona fursa za ajira zinapotokea katika makampuni vijana wa YCCG wanashindwa kuzitekeleza.

 

Alifahamisha kuwa kumezoeleka vijana kukaa mitaani baada ya wawezekaji kuwekeza, na kutangaza ajira waza wanabakia nyuma na ajira hizo zinachukuliwa na wageni.

 

“Mimi katika mkoa wangu ajira nyungi tena muhimu katika mahoteli zimechukuliwa na wageni, wazawa wanabaki kusema ajira zao zimechukuliwa wakati fani mtu hana”alisema.

 

Mkuu huyo wa Mkoa Ayoub alitoa wito huo, katika ukumbi wa Dolfin Wete kwenye uzinduzi wa kikundi cha Vijana cha mapishi, uhudumu na usafi (Youth Caterin and Cleaners Group).

 

Aidha alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane inamtazamo mpana sana kwa mchango wavijana katika maendeleo,sio katika ngazi za uongozi, vikundi, kampuni na asasi za kiraia tu.

 

Aliwataka vijana hao kutokana na hali ya dunia ilivyo ni vyema kwenda katika mfumo wabiashara na sio kikundi, kwa kuwa na mawazo ya kibiashara kwa kutengeneza chombo ambacho kitawatoa kutoka sehemu moja kwenda nyengine.

 

Mkuu huyo aliwataka viongozi wa Chama, Serikali na taasisi binafsi kuwatumia vijana hao wanapokuwa na shuhuli zao za serikali au chama katika suala zima la mapishi, uhudumu , mapambo na usafi, kwani kufanya hivyo itakuwa wamewasaidia vijana hao.

 

Aliwataka vijana kufikiria kuanzisha kampuni nyengine, ili Pemba itakapofunguka kwa uwekezaji iwe tayari kampuni imeshajitangaza, na kuzitumia fursa zitakazopatikana ili zisitumiwe na wageni.

 

“Tusipojipanga mapema ili kutumia fursa zetu zinatakapoanza, vizuri kuanza kujifunza sasa jinsi gani ya kuzitumia fursa hizo zitakapokuja”alifahamisha.

 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema atakisimamia kikundi hicho kwa kushirikia na viongozi mbali mbali, ili vijana hao waondokane na umaskini kupitia maeneo waliojiajiri.

 

Akiwasalimia vijana hao mlezi wa kikundi hicho na mbunge wa jimbo la Kojani Hamad Hassan Chande na Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Pemba Asia Sharif, wameahidi kuendelea kuvisaidia vikundi vya ujasiriamali, ili viondokane na maisha tegemezi.

 

Walisema watahakikisha katika uongozi wa serikali ya awamu ya nane, siku moja Pemba kunatoka kampuni ambayo itaweza kufanya kazi ndani nan je ya kisiwa cha Pemba.

 

Akisoma risala katibu wa YCCG Abdillah Massoud Ali, alisema lengo lao ni kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali kama inavyohimiza serikali ya awamu ya nane ya vijana kujiajiri wenyewe ili waweze kujitegemea.

 

Katika uzinduzi huo Mkuu huyo wa Mkoa kaskazini Unguja, alipigisha harambee ya kusaidia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitu mbali mbali, ambapo shilingi Milioni 1025000/= zimepatikana taslimu, shilingi Milioni 2145000/= zimetolewa ahadi.