Friday, November 1

Taasisi ya REPOA yawafunda wakulima wa mwani Kisiwani Pemba

 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa mahitaji ya zao la mwani yatazidi kuongezeka kutokana na maamuzi ya kujenga kiwanda cha mwani katika eneo la viwanda la Chamanangwe chenye uwezo wa kusarifu tani elfu 30,000 za mwani mkavu kwa mwaka.

 

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya ukulima wa mwani katika kina kirefu cha maji ya bahari, kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasi na Mifugo Zanzibar Soud Nahoda Hassa, huko katika ukumbi wa kiwanda cha Mkonyo Wawi Wilaya ya Chake Chake.

 

Alisema hicho ni kiwango kikubwa na kwa Zanzibar hakijawahi kufikiwa tangu ukulima wa mwani ulipoanza miaka ya 90, huku akisema kuwa kiwango kikubwa ambacho kiliwahi kufikiwa ni Tani 16,000 mwaka 2016.

 

Aidha aliwataka washiriki hao kuhakikisha wanapata uwelewa wa kutosha katika mafunzo hayo, ili kwenda kuwafundisha wenzao kwani wakulima wengi hawakubahatika kupata elimu hiyo, jambo ambalo wanapaswa kwenda kuwafundisha wenzao vijijini.

 

Waziri wa Kilimo alisema mipango ya serikali ya awamu ya nane ni kuendeleza viwanda hususan vile vinavyozalisha bidhaa kutokana na malighafi zinazopatikana nchini, hivyo kiwanda kitakachojengwa kinatoa hakikisho la soko kwa mwani wote utakaozalishwa na bei tulivu isiyobadilika.

 

Alifahamisha kuwa lengo la kuwa na viwanda pamoja na mambo mengine ni kuongeza tahamini mazao ya kilimo na kuhakikisha bei ya mazao ya wakulima inakuwa tulivu wakati wote.

 

“Zao la Mwani lina fursa kubwa ya kupunguza umasikini, kuongeza ajira na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi, tunakoelekea kumejaa matarajio mema, matarajio mema hayo ni pale tu kila mmoja wetu atakapojituma na kufanya kazi kwa bidii”alisema Waziri.

WAZIRI wa Kilimo Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar Soud Nahoda Hassan, akifungua mafunzo kwa wakulima wa mwani 30 juu ya kulima kisasa wataoweza kuwenda kuwafundisha wakulima wenzao vijijini, yaliyoandaliwa na taasisi ya REPOA na kufanyika mjini Chake Chake.

Aliongeza kuwa juhudi nyingi zilifanywa katika awamu iliopita kulikuza zao la mwani, ambapo inasadikiwa zaidi ya wananchi 23,000 wanajishuhulisha na shughuli za ukulima wa mwani Unguja na Pemba, huku zaidi ya asilimia 80 wakia ni wanawake.

 

Alifahamisha kuwa zao la mwani ni lakwanza kusafirishwa kwa wingi nje ya nchi na vile vile ni zao la pili linaloingiza fedha nyingi za kigeni likitanguliwa na zao la karafuu.

 

“Kutokana na hali hiyo serikali yatu ya awamu ya nane inalitazama zao la mwani, miongoni mwa mazao ya kimkakati hasa tunapoelekea kwenye uchumi wa buluu”alisema.

 

Aidha alisema kwa sasa zao hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, kuongezeka kwa joto la bahari linalosababisha mwani kushindwa kuota vizuri, kuibuka kwa mardhi ya mwani yanayopelekea mwani kukatika.

 

Hata hivyo kwa niaba ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliishukuru taasisi ya REPOA kuona kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kusaidia kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wakulima wa mwani Zanzibar.

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya utafiti wa sera za maendeleo na umasikini Tanzania (REPOA)Dkt.Donald Mmari, akitoa maelezo mafupi juu ya malengo ya taasisi hiyo katika kuwasaidia akulima wa mwani nchini na kuinua kipato chao, mafunzo yaliofanyika mjini chake chake

Akitoa salamu za Taasisi ya Utafiti wa sera za maendeleo na Umasikini Tanzania (REPOA), Dkt.Donald Mmari alisema kufanyika kwa mafunzo ya wakufunzi wa wakulima wa mwani, ni kuonyesha wazi utayari waserikali katika kuwasaidia wakulima kuongeza tija na uzalishaji wa mazao mbali mbali, ili kupata mapato zaidi na kuinua uchumi katika kuelekea uchumi wa kisasa.

Alisema taasisi ya REPOA imefanya tafiti nyingi na kuzitumia katika kushawishi na kushauri, katika maandalizi ya mapitio ya sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo nchini, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kupunguza umasikini.

Naye katibu Mkuu Wizara ya biashara na maendeleo ya viwanda Juma Hassan Reli, akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu zao la Mwani, alisema asilimia 80 ya mwani wote unaozalishwa Zanzibar unatoka Pemba, kiwanda pia kipo pemba na mahitaji ya kiwanda hicho kwa mwaka ni tani 30,0000, wakati uzalishaji wa mwani uko chini ya tanbia 15,000 ili kiwanda kiweze kuzalisha na kufikia kulipia gharama na kupata faida kinahitaji tani 30,000.

Aidha alisema kipindi cha mavuno mazuri ya mwani kwa mwaka huingizia nchi hadi Dola Milioni nane kwa mwaka, hivyo aliwaasa wakulima kuongeza bidii katika uzalishaji wa mwani  kwa kuhitaji uwepo wa soko la ndani na nche ya nchi, huku ZSTC ikinunua aina ya kotonii kwa shilingi 1800 na spinosam kwa shilingi 7000.

kwa upande wake waziri mstaafu wa wizara ya biashara na viwanda Zanzibar Balozi Amina Salim Ali, aliwataka akinamama kuwa shajihisha vijana wao kulima zao hilo, na sio kukaa vibarazani na kufanya mambo yasio faa.

Alisema asilimia kubwa wakulima wa mwani ni wanawake, hivyo aliwataka akinababa kuwaunga mkono katika kilimo hicho, ambacho serikali imeanza mikakati ya kukiboresha zaidi.