NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema lengo kuu la kutokomeza umaskini litabakia ndoto kwa waliowengi, iwapo hatutoshirikiana katika kudumisha amani na utulivu iliyopo nchini.
Alisema umasikini unaweza kuondokana na kubaki historia, ikiwa tutahakikisha amani na utulivu inaendelea kudumishwa kwa nguvu zote, vijana bila ya kushawishiwa na wanasiasa au viongozi wa dini na kupelekea kutokea machafuko.
Mkuu huyo wa mkoa aliyaeleza hayo, wakati wa uzinduzi na utambulisho wa mardi wa kuhamasisha vijana na wanawake kutunza amani ndani ya Mkoa huo, unaotekelezwa na Jumuiya ya PECEO kwa kushirikiana na Search For Common Ground kwa ufadhili wa Foundation For Civil Society na Umoja wa Nchi za Ulaya.
“Suala la kuhubiri na kudumisha amani ni muhimu sana, sio tu kwa ustawi wa jamii bali pia kwa ustawi na ujenzi wa uchumi imara, tuna kila sababu ya kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa tuliona Zanzibar kwa sasa”alisema.
Aidha alisema nilazima kama taifa kutatua migogoro mbali mbali kuhusu jamii zetu, kama migogoro ya ardhi, mashamba, wizi wa mazao na mifugo, ndoa, rasilimali hata ndani ya familia na familia, pamoja na kuongeza muhimu wa makundi mbali mbali katika kuimarisha utawala bora, utawala wa kisheria, haki za kibinaadamu na haki ya maendeleo kwa wote.
Katika hatua nyengine, Mkuu huyo aliwasihi vijana kujitahidi kadri inavyowezekana kutokuwa kundi litakaloshiriki katika uvunjifu wa amani, kwani zipo baadhi ya nchi zaidi ya miaka 30 wanaitafuta amani na wanatamani kujifunza kama ilivyo Zanzibar na Tanzania.
“Nchini kama Congo, Sudani Kusini, Somalia na baadhi ya nchi, ukitizama wahusika wanaotazama kufanya vurugu ni vijana, sitopenda vijana wa Zanzibar wakawa huko, gharama ya kuitunza na kudumisha amani ni ndogo mno, gharama ya kurudisha pale inapoharibika hatuna uwezo wa kuirudisha”alisema.
Akizungumzia serikali ya awamu ya nane, alisema imedhamiria kuboresha maisha ya watu, kupunguza na kuondosha shida za watu, ikizingatiwa Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi ameunda Serikali ya SUK licha ya kuikuta ndani ya katiba.
Naye OCD wa Wilaya ya Chake Chake Akama Mohamed Shaaban, alisema suala la amani na utulivu ni jambo muhimu sana kwa mwanaadamu tokea kuzaliwa kwake, kwani hata vitambu mbali mbali na mitume iliyopita ndani ya nchi na dola walizungumzia amani.
“Suala la amani limekuwa likizungumzwa na viongozi mbali mbali, ikiwemo kuundwa kwa serikali ya SUK jambo lililondoa visasi, chuki, hasama kwa wakaazi wa visiwa hivyo, zipo baadhi ya nchi amani wanaitafuta kufuatia machafuko yaliyotokea”alisema.
Aliwataka wananchi kujivunia amani iliyopo, kwani jeshi la polisi jukumu lao kulinda raia na mali zao, kudumisha amani ya nchi, huku akiwataka washiriki kuwa mabalozi wazuri katika kuhubiri amani katika maeneo yao yaliyowazunguruka ikizingatiwa amani ni tunu.
Mratibu wa Jumuiya ya PECEO Juma saidi Ali, alisema vijana ndio wanaoshawishika katika suala la kila kitu na ushawishi wao unakuwa juu sana, nchini haiwezi kuwa samala kama sio kudumisha amani.
Akizungumzia Sababu ilipelekea kuwashirikisha wanawake na walemavu, alisema wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa panapotokea vurigu, wakitengemea vijana kuwa ndio walindaji wakubwa wa amani hiyo.
MWISHO