MAKAMU wa Pili wa rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, amesema miundombinu ilioyofanywa na rais wa Zanzibar wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya sheria ya kukuza na kulinda Uwekezaji ya mwaka 2018, ndio moja ya sababu ya kuvutia wawekezaji hapa Zanzibar.
Makamu huyo wa Pili, aliyasema hayo Chamanagwe wilaya ya Wete Pemba, kwenye uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha kuzalishia maji ya chupa cha kampuni ya Amos LTD, ikiwa ni sehemu ya wiki ya Dk. Mwinyi, ya kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake.
Alisema, wakati anaingia madarakani, alitaka kuona sheria zote zinazozuia maendeleo kufanyiwa marekebisho, ambapo moja wapo ni hiyo ya Kukuza na kulinda Uwekezaji Zanzibar nambati 14 ya mwaka 2018.
Alisema, marekebisho hayo sasa yamekuja kuruhusu mwekezaji hapa Zanzibar, kuwa anaweza kuekeza akiwa na mtaji wa dola za Marekani milioni 10 kutoka milioni 50 kabla ya marekebisho hayo.
Alieleza kuwa, hilo limefungua fursa kwa wawekezaji, hali iliyopeleka ndani ya mwaka mmoja wa Dk. Mwinyi kuanzia Novemba 2020 hadi Novemba 2021, kuwa na miradi 97 imeshasajiliwa hapa Zanzibar.
Ambapo miradi hiyo, inamitaji ya dola za Marekani milioni 788 sawa na shilingi trilioni 1.8, miradi hiyo ikitarajiwa kuzalisha ajira 7000, ambapo ni kinyume na kipindi kama hicho, kwa mwaka uliopita, ambapo kulisajiliwa miradi 30 yenye thamani ya dola za Marekani 78 za kuzalisha ajira 1,213.
Aidha Makamu huyo wa Pili, alisema kasi hiyo ya maendeleo, inatokana na dhamira ya kweli ya Dk. Mwinyi, ambapo kielelezo tosha ni ufunguzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi 12 Unguja na Pemba.
“Hata uwekaji wa jiwe la msingi kwenye kiwanda hichi cha uzalisaji maji hapa Chamanangwe, ni kielelezo thabiti cha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa Pili wa rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, alisema katika jitihada za kukikuza kisiwa cha Pemba kimaendeleo, ni kulitangaaza eneo la Chamanangwe kuwa ni la viwanda.
Aidha alisema eneo hilo, lenye ukubwa wa hekta 55.37, tayari wawekezaji wameanza kulitumia na mfano wa kiwanda hicho ni mmoja, ambapo pia mwekezaji huyo anatarajia kuzalisha mabati na juisi hapo baadae.
Alieleza kuwa, ahadi za rais wa Zanzibar alizozitoa kweye kampeni mwaka 2020, zitaendelea kutekeleza hatua kwa hatua, ili Zanzibar mpya nyenye uchumi wa kati, iweze kufanikiwa.
“Zanzibar mpya itatokana na ushiriki wa serikali katika ujenzi wa viwanda vidogo vidogo, vyakati na vikubwa, vyenye kuzalisha bidhaa bora zenye viwango na vyenya kuhimili ushindani wa soko,’’alieleza.
Hata hivyo alieleza, serikali itaendelea kushirikiana na kutoa kila aina ya msaada kwa wawekezaji wazalendo na wageni, ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji, yanakuwa rafiki kwao.
Makamu huyo wa Pili aliesema jihudi nyingine zilizofanywa na serikali kukuza uwekezaji nchini, ni kukabidhi maeneo tengefu ya ardhi ‘land bank’, mashamba ya mipira na visiwa vidogo vidogo kwa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ZIPA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ‘ZIPA’ Sharif Ali Sharif, alisema sasa mazingira ya wawekezaji yamekuwa rafiki kwao.
Nae Waziri wa nchi ofisi ya rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mudrik Ramadh Soroga, aliwataka wananchi, kuendelea kumuunga mkono rais wa Zanzibar, ili atekeleza ahadi zake.
Aliema, mwaka mmoja wa Dk. Mwinyi, umekuwa dira na kudhihirisha nia yake kwa wananchi wa Zanzibar, wakati alipokuwa akiomba ridhaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Kiwanda cha Amos LTD Husamudin Ali Mussa, alisema pamoja na kiwanda kuzalishaji maji, hapo baadae wanatarajia kuwa na kiwanda cha bati na juisi za matunda.
Alisema baada ya kuomba eneo la skweya kilomita 9,600 kutoka serikalini na kupewa, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, ambapo wameshajenga majengo matatu.
Jengo moja ni kwa ajili ya uzalishaji maji lenye ukubwa wa skweya kilomita 1200, ambapo jengo la pili ni kwa ajili ya utawala, ukumbi wa mikutano wakati jengo la tatu ni kwa ajili wafanyakazi.
Aidha alisema kiwanda kitakuwa na mashine nane, ikiwemo ya kutengenezea chupa, kusafishia, kujaza maji, kufungashio pamoja na gari mbili za kusafirishia maji.
Ujenzi wa kiwanda hicho ambao ulianza miezi mitatu iliyopita, utagharimu shilingi bilioni 1.8 hadi kukamilika kwake, ambapo pia hapo baadae wanatarajia kuzalisha juisi za matunda.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha maji lita 5000 kwa saa moja, samba mba na ajira kati ya 50 za kudumu na ajira 60 nje ya kiwanda.
Mwisho