Uchafuzi wa hewa katika sekta ya usafiri umeongezeka zaidi ya mara mbili tangu mwaka 1970 huku takribani asilimia 80 ya ongezeko hilo limesababishwa na magari barabarani.
Shirika la umoja wa Mataifa la mazingira UNEP linakisia kwamba sekta ya usafiri duniani inategemea kwa akaribu asilimia kubwa mafuta ya kisukuku.
Hali inaweza kubadilika miongo ijayo
Kwenye mkutano wa COP26, zaidi ya serikali 100, miji, majimbo na makampuni ya biashara wametia saini Azimio la Glasgow kuhusu magari na vani kumaliza uuzaji wa ndani wa injini zinazotoa hewa chafuzi ifikapo 2035 na katika masoko yanayoongoza kote duniani ifikapo mwaka wa 2040.
Takriban mataifa 13 pia yamejitolea kukomesha uuzaji wa magari ya kubebea mizigo yanayoendeshwa na mafuta kisukuku ifikapo mwaka 2040.
Juhudi za ndani pia zinaendelea, huku miji ya Amerika Kusini, ikijumuisha Bogota, Cuenca na Salvador, ikilenga kubadilisha meli za usafiri wa umma na kutumia zisizotoa hewa chafu ifikapo 2035.
Ujumbe kwa watoa maamuzi ni kwamba: Tunahitaji kuhakikisha kuwa tunaanza kurekebisha hali hii ifikapo mwaka 2035, lazima tuache kuuza magari ya petroli na dizeli.
Kwa mabasi, itakuwa mapema zaidi mwaka 2030, malori makubwa, yanaweza kupewa muda zaidi hadi mwaka 2040.
Hoja ni kuzoea wazo la kuwa na kalenda ili tuweze kuhamia kwenye chaguo la kutozalisha kabisa hewa ukaa katika sehemu zote. Hii sio tu kwa masoko ya juu katika nchi zilizoendelea, pia ni kwa uchumi unaoendelea kwa sababu tunajua uchafuzi mbaya zaidi upo,” amesema Monica Araya kutoka mpango wa kimataifa wa kampeni ya kuendesha magari yanayotumia umeme.”
Bi. Araya alikuwa wazi “wakati wa kipindi cha mpito , nchi zinazoendelea asilani zisiwe dampo la kutupa magari ya teknolojia ya zamani kutoka nchi Tajiri na badala yake zionekane kama waongozaji wa mabadiliko.”
Sekta ya usafiri inayojali mazingira
Sekta ya usafiri wa meli pia imepiga hatua leo ikiwa na biashara 200 kutoka kote kwenye mnyororo wa thamani wa usafiri wa meli zinajitolea kuongeza juhudi na kufanya biashara ya usafiri wa meli kutotumia mafiuta yanayochafua mazingira ifikapo 2030.
Pia sekta iyo imetoa wito kwa serikali kupata kanuni na miundombinu sahihi ili kuwezesha mabadiliko ya haki ifikapo mwaka 2050.
Wakati huo huo, nchi 19 zimetia saini azimio la Clydebank kusaidia uanzishwaji wa njia za usafirishaji zisizotoa gesi chafu.
Hii inamaanisha kuunda angalau njia sita za baharini zisizotoa kabisa hewa chafuzi ifikapo katikati ya muongo huu, huku tukitamani kuona nyingi zaidi zikifanya kazi ifikapo 2030.
“Kuna meli za wafanyabiashara zipatazo 50,000 huko nje duniani kote kwa hivyo ni kazi kubwa iliyopo, na nadhani sehemu tofauti za usafirishaji zitasonga kwa kasi tofauti. Kwa hivyo, kuwa na dhamira ya azimio la Clydebank kwa kuweka mazingira safi na kuwezesha wasafirishaji kwanza kujaribu na kutumia teknolojia kisha kupunguza gharama, kuunda sera, kuwezesha mifumo ya ikolojia inayohitajika, na kisha wengine wanaweza kujifunza kutokana na hilo na kisha kufuata nyayo,” amesema Katharine Palmer mchagizaji mkubwawa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa.
Habari nyingine Njema ni kwamba makampuni yenye majina makubwa ikiwemo Amazon, IKEA, Michellin, Unilever na Patagonia yametangaza kwamba ifikapo 2040 yanapanga kubadili asilimia 100 ya vyombo vyake vya usafirishaji na kuingia kwa visivyozalisha kabisa hewa ukaa.
Changamoto ya usafiri wa anga
Biashara za sekta ya usafiri wa anga na wateja wa makampuni makubwa pia wametangaza marekebisho katika muungano wao wa Anga Safi kwa ajili ya Kesho, ambao dhamira yake ni kuharakisha utumaji wa nishati safi na endelevu za anga.
Sasa, watia saini 80 wamejitolea kuongeza matumizi ya mafuta yasiyochafua mazingira hadi asilimia 10 ya mahitaji ya kimataifa ya mafuta ya ndege ifikapo 2030.
Haya ‘mafuta yanayojali mazingira ’ huzalishwa kutokana na malisho endelevu kama vile mafuta ya kupikia, taka za mawese kutoka kwa wanyama au mimea, na taka ngumu kutoka majumbani na katika sekta za biashara, na kikemia zinafanana sana na nishati ya jadi inayotumiwa na ndege.
Lengo hili likifikiwa, litapunguza utoaji wa hewa ukaa kwa tani milioni 60 kwa mwaka na kutoa karibu ajira 300,000 za kazi zinazojali mazingira.
Mtaalam huyo pia ametangaza kwamba “ndege za kwanza za kutumia umeme na hewa ya hidrojeni zitaanza kutumwa ifikapo 2030, na mabadiliko ya tasnia pia yanaweza kutoa maelfu ya ajira za zinazozingatia mazingira katika nchi zinazoendelea.”
Rasimu ya makubaliano ya COP26 yawekwa bayana
Zaidi ya usafiri, habari nyingine kubwa katika mkutano huo wa Jumatano ni rasimu ya makubaliano ya COP26 iliyochapishwa na ofisi ya Rais, ambayo ni hakikisho la hati ya mwisho ya matokeo ya mkutano huo utakapokamilika Ijumaa.
Waraka huo unazitaka nchi kuimarisha ahadi zao za kitaifa na kuwasilisha mikakati yao ya mipango ya kutozalisha hewa ukaa ifikapo mwaka wa 2022 ili kuhakikisha lengo la kusalia na nyuzi joto 1.5C linafikiwa.
Pia rasimu inajumuisha, kwa mara ya kwanza katika maandishi ya matokeo ya COP, kutajwa kwa ‘hasara na uharibifu’, pamoja na wito wa kukomesha ruzuku za mafuta kisukuku.
“Macho ya dunia yanatutazama . Kwa hivyo, ninawaomba ,kabiliane na changamoto hiyo” amersema Alok Sharma, Rais wa COP26, aliwaambia washiriki wakati wa kikao hicho kisicho rasmi.
Akizungumza na waandishi wa Habari Sharma amesema “Kila mtu anajua nini kiko hatarini katika mazungumzo haya. Tunachokubaliana hapa Glasgow ndio kitatanabaisha mustakabali wa watoto na wajukuu zetu, na tunajua hakuna anayetaka kuwaangusha.”