Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewapongeza viongozi na wazee wa Tumbatu kwa hatua nzuri iliofikia ya kukubali kumaliza tofauti zao zilizodumu kwa muda mrefu.
Mhe. Hemed ameleza hayo katika kikao maalum kilichowakutanisha Viongozi pamoja na wazee wa Tumbatu kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais. Dk. Mwinyi imedhamiria kuwaletea maendeleo wanachi wake waliopo katika Kisiwa cha Tumbatu, hivyo kufikia hatua hiyo la kupatikana kwa suluhu itakwenda kushajihisha serikali kufikia azama yake ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais amewakumbusha viongozi na Wazee wa Timbatu kuendelea kuzitumia hekima na busara zao kwa ajili ya kuwaongoza vijana kuwa kitu kimoja na kuachana na tabia ya kubaguana jambo litakalopelekea mapenzi na huruma miongoni mwao.
“Kwa umoja wetu tusibezane, tusichukiane,tusiuziane kwani kuimarisha kwa hayo Tumbatu kwa muda mfupi itapiga hatua za kimaendeleo” Alisema Mhe. Hemed
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amewataka viongizi wa Dini kuendelea kukiombea Kisiwa cha Tumbatu na wakaazi wake kutourudi tena katika maisha ya dhiki na dhulma ili kuondokona na mateso yaliokuwa yakiwakabili kwa muda mrefu.
Akizungumzia mikakati ya maendeleo Mhe. Hemed amewahakikishia wananchi wa Tumbatu kuwa serikali katika kipindi kisichozidi cha wiki mbili fedha nyingi zitakifikishwa kisiwani humo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya Maji, ujenzi wa skuli, vyookwa ajili ya wanafunzi pamoja na kuimarisha sekta ya Afya.
Katika hatua nyengine Mhe. Hemed amewaagiza viongozi wa vyama vya siasa kutojiaribu kuingilia mchakato huo mzuri uliofikiwa kwa kusababisha chokochoko miongoni mwa wanachama wao wanaowaongoza.
Pia Makamu wa Pili wa Rais amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kusimamia suala la undwaji wa Kamati itakayoendelea kuratibu na kuimarisha maendeleo ya suluhu iliofikiwa kupitia kikao hicho cha Viongozi na Wazee wa Tumbatu.
Nae Muwakilishi wa Jimbo hilo la Tumbatu Mhe. Haji Omar Kheir amesema kuna haja kwa wananchi wa Tumbatu kupiga mstari kwa kuachana na tofauti zao sambamba na kusahau mambo yote mabaya yaliopita.
Mhe. Haji Omar Kheir amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua alioichukua ya kumuagiza Makamu wa Pili wa Rais kwa kuipatia Ufumbuzi changamoto ya sintofahamu ya wananchi wa Tumbatu iliodumu kwa muda mrefu sasa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amesema kitendo cha kupatiwa Suluhu kwa mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kwa wananchi wa kisiwa cha Tumbatu ni jambo la kihistoria ambapo wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo za Mhe. Rais Dk.Mwinyi kwa kuwataka wananchi kuwa kitu kimoja.
Nao, Viongozi pamoja na wazee waliohudhuria katika kikao hicho wamemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa, kwa niaba ya wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu wamekubali kuzika tofauti zao zilizopita lengo likiwa ni kushajihisha maendeleo kwa wakaazi na wananchi wa Kisiwa hicho.
Viongozi hao wameeleza kwamba, kwa Muda mrefu wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu wameishi katika madhila na dhiki kutokana na kukosekana kwa umoja, mshikamano na mashirikiano miongoni mwao hali iliosababisha watu wake kutoshirìkiana kakatika masuala ya msingi ikiwemo Sherehe na misiba.
Kikao hicho kimewakutanisha Viongozi wa serikali wa ngazi tofauti, Vyama vya siasa, viongozi wa Dini, pamoja na wazee wa vijiji vya Tumbatu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)