Sunday, November 24

TUZINGATIE maadili katika malezi ya watoto yatima – MAMA ZAINAB.

Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ametoa wito kwa jamii kuzingatia malezi na maadili mema katika kuwasimamia watoto yatima ili kujenga msingi bora wa maisha yao ya baadaye.
Mama Zainab ameyasema hayo leo alipotembelea Ofisi za Jumuiya ya Muzdalifa na kuongoza hafla ya kuwagawia sadaka watoto yatima, iliyofanyika katika Ukumbi wa Sebleni kwa Wazee, Jijini hapa.
Amesema licha ya dhima ya mahitaji, huduma za msingi na matunzo ya huruma wanayohitaji watoto walioondokewa na wazazi, bali la msingi ni pamoja na kuzingatia malezi bora na maadili, yatakayopelekea sehemu hiyo muhimu ya jamii kujengeka na kukubalika katika maisha ya baadaye.
Akitilia mkazo suala la malezi bora na maadili kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu wakiwemo wenye mahitaji maalum, Mama Zainab amewaasa wanafamilia kutokiuka wajibu wa matunzo, kwa kutegemea huduma za vituo vya kulelea yatima pekee, pindipo inapotokea miongoni mwa wazazi au walezi kufariki dunia.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Muzdalifah, Sheikh Farouk Hamad Khamis ameeleza azma ya taasisi yake kuungamkono juhudi za kuwahudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo wenye mahitaji maalum, ili kusaidia malengo ya Serikali katika maendeleo na ujenzi wa ustawi bora wa jamii, katika visiwa vya Unguja, Pemba na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi na watendaji mbali mbali wa Serikali, asasi za kiraia, jumuiya za kusaidia watoto yatima, Idara ya Ustawi wa Jamii, na wazazi.
Katika hafla hiyo, Mama Zainab alikabidhiwa Ngao maalum ya Utumishi na Kujitolea katika Kusaidia Watoto Yatima, Wenye Ulemavu na Wanaoishi katika Mazingira Magumu, iliyodhaminiwa na Jumuiya ya Muzdalifa.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar