Monday, November 25

RAIS DKT.HUSSEIN MWINYI AFUNGUA MADRASATUL MARYAM -MFENESINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimkabidhi Cheti Mwanafunzi Nadya Haroub Nassor akiwa ni miongozi mwa Wanafuzi 52 waliohifadhi vizuri Juzuu 30 za Quran katika madrasa hiyo wakati wa Sherehe ya Ufunguzi wa Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi, Sheikh Hemed Suleiman katika sherehe za ufunguzi uliofanyika leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akifungua pazia akiwa mgeni rasmi katika sherehe ya Ufunguzi wa Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi leo wakiwepo na Mwalimu Mkuu wa madrasa hiyo Sheikh Hemed Suleiman na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mhe.Machano Othman Said
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Viongozi mara alipowasili katika viwanja vya Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi kwa ajili ya kuifungua madrasa hiyo leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuifungua Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi leo (kushoto) Mwalimu Mkuu wa madrasa hiyo Sheikh Hemed Suleiman na Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini Mhe.Machano Othman Said
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Muanzilishi wa Madrasatul-Maryam iliyopo Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi Bibi Mariam Omar Mohamed (katikati) mara baada ya kufungua madrasa hiyo leo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu wa jamii kuwatunza walimu wa madrasa kwa kuandaa  mpango maalum wa kuwawezesha ili wahamasike katika ufundishaji , ikiwa pia ni hatua ya kuondokana na udhalili wa maisha walionao hivi sasa. 

 Dk. Mwinyi ametoa wito huo Mfenesini katika hafla ya ufunguzi wa Madrasatu Maryamu iliofanyika Mfenesini Mkoa wa Mjini Magharibi.

 Amesema kuna umuhimu wa kuwatunza  walimu wa madrasa ili waweze kupata utulivu na kuwafundisha vyema wanafunzi, huku akitilia mkazo kuwepo mipango ya kuwawezesha ili kuondokana na maisha duni waliyonayo.

 Aliwataka walimu na wazazi kuwahimiza watoto kudurusu masomo yao ili waweze kufanikiwa, huku akiunga mkono juhudi za Madrasa hiyo za kutoa msukumo katika ufundishaji wa muda wa ziada, hususan kwa wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani ya Taifa ya mwisho wa mwaka.

 Alisema serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kusomea katika skuli Unguja na Pemba, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mlundikano wa wanafunzi uanosababisha kuwepo mikondo miwili ya masomo, hatua inayochangia wanafunzi kukosa muda wa kwenda madrasa kusoma masuala ya Dini.

 Aidha, aliutaka Uongozi wa Madrasa hiyo kuunda kamati kushughulikia uendeshaji wa Madrasa, ambapo pamoja na mamabo mengine itashughulikia suala la usafi.

 Rais Dk. Mwinyi alisema mfadhili wa ujenzi huo tayari ametelekeza wajibu wake, hivyo akawataka waumini wengine kujitokeza kuendeleza ujenzi huo, akibainjisha wajibu huo kuwa ni wa watu wote na sio wa wafadhili pekee.

 Vile vile, alisiitiza umuhimu wa waumini kutoa sadaka kutoka miongoni mwa yale aliyowaruzuku Mwenyezi Mungu, kwa kigezo kuwa suala hilo limeelezwa katika Qoraan na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) , huku akiwataka kutumia vyema majengo ya Ibada.

 Dk. Mwinyi aliwapongeza wahisani na watu wote waliotabaruki kwa njia mbali mbali na hatimae kufanikisha  ujenzi huo.

 Aliahidi kuchangia upatikanaji wa Computa pamoja na kuahidi kushirikiana na wafadhili mbali mbali kufanikisha ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa madrasa hiyo.

 Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisema suala la ufunguzi wa madrasa sio kuwa ni la utamaduni wa Zanzibar, bali ni dini iliorithiwa na Mtume Muhammad (SAW) pamoja na masahaba zake.

 Mapema, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, akitoa salamu za Ofisi ya Mufti alisisitiza na kushajihisha usomaji wa Qur-an, huku akifafanua kuwepo kheri , fadhila na ujira mkubwa kwa walimu wa Qur-an, wanafunzi, waumini wanaosikiliza,  wazazi wa wanafunzi, wajenzi wa madrasa, pamoja na wale wanaofungua madrasa hizo.

 Aliitaka jamii ya Wazanzibari kuwapa heshima wanayostahili walimu wa madrasa  ikiwa ni hatua ya kuondokana na udhalili uanowakabili hivi sasa.

 Alisema Ofisi ya Mufti imeandaa masomo ya walimu wa madrasa ili kuwasaidia namna ya ufundishaji na njia za kuwaadabisha wanafunzi pale wanapokosea.

 Akisoma Risala ya Madrasa hiyo  Sheikh Suleiman Mohamed Omar alisema miongoni mwa changamoto inazokabiliana nazo Madrasa hiyo ni pamoja na uzito wa Wazazi katika kuchangia ada za mwezi pamoja na mashirikiano madogo kati ya walimu na wazazi.

 Madrsatul Maryamu  yenye wanafunzi wapatao 1091, iliasisiwa mwaka 1995 na Bi Maryamu Mohamed Omar Ziwani kisiwani Pemba, ambapo ujenzi wa Madrasa hiyo ya kisasa ya ghorofa mbili , unahusisha vyumba 22, Ofisi ya walimu, maktaba pamoja na  Chumba cha Komputa ulianza mwaka  2005 kupitia kwa wafadhili mbali mbali.

 Katika hafla hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alitembelea madarasa ya zamani ya Madrsa hiyo pamoja na kuwakabidhi vyeti wnaafunzi sita waliohitimu Juzuu 30.

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar