Monday, November 25

Bandari ya Bagamoyo: Ujenzi wake umekumbwa na nini?

D

CHANZO CHA PICHA,AFP

Katika miongo miwili iliyopita, tumeshuhudia uwekezaji mkubwa ukifanywa na Serikali ya Tanzania kwenye miundo mbinu ya usafiri na usafirishaji.

Ukiacha ujenzi wa barabara ulioongeza mtandao wa barabara nchini humo hadi kufikia zaidi ya kilometa 86,000, kuna miradi ya Reli ya SGR iliyowekezwa zaidi ya dola bilioni 1.2 ikitarajiwa kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi, upo mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, Dodoma, upanuzi wa bandari za Dar es salaam na Mtwara na ujenzi wa bandari mpya ya kisasa ya Bagamoyo.

Hapa kwenye bandari ya Bagamoyo, panaleta hisia mseto miongoni mwa watanzania kwa namna mradi huu, unavyotazamwa na kuchukuliwa na viongozi mbalimbali, na hisia mseto hizo zinaleta mitazamo kinzani inayozidi kuongeza ‘ndimi’ tofauti kwa wananchi wa kawaida.

Wapo wanaoona ni mradi mzuri ulio na manufaa kwa watanzania na wapo wanaoutazama kama mradi usiofaaa unaokuja kuinyonya Tanzania.

Nini kilichoko nyuma ya pazia na kwa nini ndimi mbili?

Mwezi Oktoba mwaka 2015, ujenzi wa mradi wa Bagamoyo chini ya Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (SEZ), ulizinduliwa rasmi na Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwenye uzinduzi huo alikuwepo Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Usultani wa Oman Dkt. Ahmed Mohamed Al Furaisi na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya China Merchants Group Dkt. Hu Jianhua kuashiria safari ya kuelekea kupata bandari itakayokuwa na uwezo karibu mara mbili ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa ndio tegemeo na bandari kubwa nchini.

Kabla ya uzinduzi kulikuwa na majadiliano na mazungumzo ya muda mrefu kuhusu thamani ya mradi wenyewe, uwekezaji, ubia, hasara na faida zake, lakini ziara ya mwezi Machi mwaka 2013 ya Rais wa China Xi Jinping nchini Tanzania, na kusaini mikataba 16 na mwenyeji wake Rais Kikwete kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ilitoa picha ya namna utawala wa awamu ya nne ulivyoamini kuhusu mradi huu wa Bagamoyo na faida zake.

Hata Mwezi Julai mwaka huo, alipotembelea wakati huo Uwanja wa Sabasaba kwenye maonyesho ya biashara ya kimataifa (DITF), Rais Kikwete alitangaza neema kwa wakazi wa Bagamoyo ambayo wangeathirika na ujenzi huo, ikiwemo kubomolewa makazi yao.

‘hakikisha mnawasiliana na Bandari jinsi gani ya kuwalipa fidia wakazi wa bagamoyo mtakaowahamisha kwa kuwajengea nyumba sehemu nyingine ili wakazi hao wasiyumbe kiuchumi’, alinukuliwa Rais Kikwete alipokuwa akimpa maagaizo Mkurugenzi wa wakati huo wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhem Meru.

Lakini kabla ya ujenzi kufika popote Mwezi Mei, 2019 Serikali ikalitaarifu bunge la Tanzania kwamba Mradi mkubwa wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (Bagamoyo SEZ) umefutwa na hautafanyika tena.

Juni 7, 2019 Rais wa awamu ya Tano, John Pombe Magufuli aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 kuchukua nafasi ya Rais Kikwete aliueleza umma kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwanini ameamua kufanyauamuzi huo? na alinukuliwa akisema “kwenye mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo kulikuwa na vipengele vya hovyo”.

v

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Rais Magufuli

Kabla watanzania hawajasahau kauli hiyo ambayo waliiamini kwa sababu imetoka kwa kiongozi wao, miaka miwili baadaye (Juni 26, 2021), Rais wa awamu ya 6, Samia Suluhu ambaye alikuwa makamu wa Rais wakati wa utawala wa Rais Magufuli, kwenye mkutano mwingine wa baraza la taifa la biashara akaja na kauli ingine ya kufufuliwa kwa ujenzi wa bandari hiyo.

‘tumeanza mazungumzo (na mwekezaji) ya kufufua mradi wote ule wa Bagamoyo ili nao tuufungue twende nao kwa faida ya taifa letu na kwa faida ya wawekezaji pia’, alisema Rais Samia kwa ufupi.

Huenda kauli hii haimaanishi kutoyaona masharti ya hovyo aliyoyaona mtangulizi wake John Pombe Magufuli, lakini inatoa picha ya namna mradi huu unavyopaswa kutazamwa mara mbili mbili, ili kujenga Imani kwa watu kutokana na kauli za mamlaka.

Kauli hii ilikuwa ya matumaini kwa waliokuwa wanapigia chapuo ujenzi wa bandari hii, ikionekana kuwa na mtazamo sawa ama unaokaribiana na ule wa utawala wa awamu ya nne kuhusu ujenzi wa Bagamoyo.

Lakini kwa wale walio ishika vyema kauli ya magufuli kuhusu “masharti ya hovyo” kurejeshwa kwa mradi huu ni mwiba jichoni.

‘Mradi huu mkubwa wa uwekezaji ambao thamani yake ni zaidi ya Bajeti ya Maendeleo ya Wizara nzima ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa miaka minne (TZS 18 Trilioni) haupaswi kufutwa tu bila mjadala wa kina’, ilikuwa kauli ya kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo kuonyesha kutofurahishwa na kauli ya kufutwa kwa mradi huo.

Sasa mijadala imeibuka hasa, na maswali lukuki yakiulizwa, likiwemo la kwanini kuna kauli ‘ndimi’ mbili kuhusu mradi huu?

Hakuna anayeweza kuwa na jibu thabiti la kauli hizi, lakini inasalia kusemwa faida za mradi huu, haziwezi kuepukwa na hasara kadhaa zinazoonekana kwenye picha nzima ya mradi.

Kwanini ujenzi wa bandari hii unapigiwa chapuo?

Unaweza kutaja faida zake ndio msingi wa mradi huu kupigiwa chapuo na wanaoutaka.

Wengi wakisikia ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, wanaishia kwenye kufikiria kuhusu bandari yenyewe tu, lakini kwa mujibu wa mkataba wa mradi huu wa Bagamoyo SEZ, kunatarajiwa kujengwa pia viwanda karibu 880, awamu ya kwanza ya ujenzi wa viwanda hivi vitajengwa viwanda 190.

a

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Rais Samia wa Tanzania ameonyesha nia ya wazi ya kuendelea na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo

Jumla ya ajira 120,000 zinatarajiwa kuzalishwa kupitia viwanda hivi pekee, huku ajira 20,000 zikianza kuzalishwa kwenye awamu ya kwanza ya viwanda 190. Hii ni faida kubwa inayotazamwa na wanaoupigia chapuo mradi huu.

Patakuwa na ujenzi wa mji wa kisasa kupunguza msongamo katika jiji la Dar es laam, ambapo ni takribani kilometa kama 70 mpaka ulipo mradi huu.

Ukiacha yote ujenzi wa Kituo cha usafirishaji (Logistics Park) kwenye eneo hili kutaifanya Bagamoyo kuwa kitovu kikubwa cha uzafirishaji wa mizigo, ambapo kontena milioni 20 zingepita kwenye bandari hii na kuweza kuipiku hata bandari ya Rotterdam iliyopo Uholanzi ambayo inatajwa kuwa bandari kubwa ya mizigo barani Ulaya.

Bandari hii pia itapunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara wanaozafirisha mizigo yao kwa meli. Leo ukishafirisha mzigo kwa meli ndogo unatumia gharama mara mbili zaidi kwa mzigo ambao kwa meli kubwa ungeokoa nusu ya gharama hizo.

Kiuchumi, gharama za uendeshaji na gharama za usafirishaji ni muhimu kwenye upangaji wa bei ya bidhaa. Kutumia gharama ndogo maana yeke, bidhaa zitauzwa kwa bei ndogo, hivyo itaongeza usambazaji wa bidhaa husika huku zikimfkia mtu mwenye kipato cha chini (ambao kwa watanzania ni wengi) kwa gharama nafuu.

Je mradi huu ni tishio kwa washindani?

Bila kupepesa macho, kwa Afrika Mashariki, mradi huu ni tishio hasa kwa nchi ya Kenya, ambayo imekuja na mradi wake mkubwa wa bandari ya Lamu ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 23.

Bandari hii ya Lamu ni muhimu kibiashara kwa nchi kama Sudan Kusini na Ethiopia, ikitarajiwa kupitisha tani milioni 23.9 za mizigo ifikapo mwaka 2030 pamoja na kuunganisha pia bandari za Djibouti, Berbera (Somaliland) na bandari ya Durban Afrika Kusini.

Kuja kwa bandari ya Bagamoyo, ambayo haitakuwa mbali sana na bandari ya Mombasa, ambayo inapitisha mizigo tani milioni 14 kwa mwaka, kutaongeza ushindani wa kibiashara.

Hilo halina ubishi, lakini haitakua mshindani wa moja kwa moja wa bandari ya Dar es salaam ambayo asilimia karibu 90 ya mizigo mikubwa inapia pale.

s

CHANZO CHA PICHA,MARITINE

Maelezo ya picha,Lamu

Bandari ya Bagamoyo, itakuwa inahudumia meli kubwa (4th generation ships) ambazo hazitakuwa na uwezo wa kuingia kwenye bandari ya Dar es Salaam, maana yake ni kwamba bandari ya Bagamoyo itakuwa mshindani zaidi wa bandari kama Lamu, badala ya kuwa tishio kwa bandari ya Dar es Salaam ama Mtwara, ingawa ukweli hautakwepwa kwamba kuna meli ndogo pia ambazo zilikuwa zinapitia Dar es salaam zitakwenda Bagamoyo. Kwa kutumia dhana ya eneo, pengine bandari hizi bagamoyo na Dar es Salaam zitashindana, lakini ushindani wao utakuwa wa faida kwa nchi. Meli zitakaa mda mfupi, kutokuwepo kwa misogamano na kuzidisha huduma ya upakiaji na upakuaji wa mizigo inayotoka na kuingia nchini humo.

Kwa mtazamo wa jumla, bandari ya Bagamoyo, itaongeza biashara katika eneo la Afrika Mashariki na kati kama ilivyo kwa bandari ya Lamu, Mombasa na ile ya Dar es Salaam na hata ya Tanga. Hilo ni faida kubwa kwa uchumi wa Afrika Mashariki.

Muhimu bandari hizi zishindane kwa huduma nzuri, ikiwemo meli kutumia muda mfupi kushusha na kupakia mizigo na kupunguza milolongo ya utaratibu wa kutoa na kuingiza mizigo bandarini pamoja na kuboresha mzingira ya huduma za bandari.

Pamoja na faida zake, kwanini Mradi huu unamwendo wa jongoo?

Kwa mtizamo wa haraka haraka unaweza kusema jibu rahisi ni kwamba, uwepo wa utofauti wa kimitizamo kati ya watu wenye mamlaka wanaoweza kufanya maamuzi ya mradi huu kuendelea ama kutoendelea. Kama Mtazamo wa utawala wa awamu ya nne kuhusu mradi huu ungekuwa sawa na mtazamo wa utawala wa awamu ya tano, chini ya Rais Magufuli, pengine mradi huu leo ungekuwa mbali. Pengine leo maelfu ya watanzania wangekuwa wameanza kunufaika na bandari hii ikiwemo ajira.

Ingawa kutofautiana mtazamo ni jambo linalokubalika na sio dhambi ama kosa la kijinai, wasiwasi wa wengi ni kama utakuja utawala mwingine ambao hautaaamini kuhusu bandari hii, nini kitafuatwa? Je fedha zitakazokuwa zimewekezwa katika hatua za kwanza za ujenzi wa mradi mzima nani atalipa gharama zake?

Hivyo mazungumzo aliyoyasema Rais Samia kuhusu mradi huu ambao bila shaka yanashirikisha Serikali ya Tanzania na washirika wake China na Oman yanapaswa kujielekeza kupima faida kwa mlinganisho wa hasara kwa masharti tajwa. Inawezekana kuboreshwa kwa baadhi ya vipengele ili kuufanya mradi huu kuendelea kutekelezwa, bila kuathiri uchumi wa nchi.

Nini hatma ya masharti tata ya mradi huu?

Moja ya swali kubwa wengi wanajiuliza ni hili la hatma ya masharti ya mkataba wa bagamoyo ambayo Rais Magufuli aliyaita ya “hovyo”.

Alitaja moja ya masharti hayo ni kutojengwa wala kuendelezwa kwa bandari yoyote kuanzia eneo la Tanga hadi Mtwara. Sharti lingine lililomshitua Rais Magufuli ni lile la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotakiwa kwenda kukusanya ushuru wala kodi katika eneo la bandari na kutaka wapewe hakikisho la miaka 33.

Pia alisema wawekezaji hao wangeweza kumiliki ardhi kwa hati ya miaka 99 pamoja na kutoruhusiwa kuulizwa nani anamiliki eneo hilo huku sharti lilingine aliloliona lina ukakasi ni la gharama kwamba gharama zitakazotumiwa na mwekezaji huyo katika ujenzi wa bandari hiyo zinatakiwa zirejeshwe.

Mmoja wa wachumi kutoka chuo kikuu cha Ushirika Moshi, Dokta Barnos Willium anasema ni muhimu masharti haya yatupiwe jicho, ‘Sijauona mkataba, lakini kama ni kweli hayo masharti yapo, ni muhimu yakawekwa kwenye mjadala, ingawa nafahamu kwa muwekezaji kutoa matrilioni ya shilingi, bila kunufaika kwa namna yoyote, sidhani kama ni rahisi’, alisema Dokta Barnos Willium

Kuhusu sharti la Tanzania na mamlaka zake za kodi kutokusanya kodi ya mapato kwenye bandari hiyo kwa miaka 30, mchumi huyu anaeleza, ‘haiwezi kukubalika hata kama kuna faida za kiwango gani, chanzo kikubwa cha mapato cha taifa ni kodi, na bandari ni chanzo kikubwa sana cha mapato, nadhani namna bora ni kuweka asilimia fulani ya kodi iingie hazina’, alisema.

a

CHANZO CHA PICHA,HABARI LEO

Maelezo ya picha,Mchoro wa ujenzi wa bandari hiyo utakavyoonekana

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bandari ya Dar es Salaam inaingiza zaidi ya shilingi bil. 70 kwa mwezi. Kama Bandari ya Bagamoyo itakuwa na ukubwa mara mbili mpaka 20 ya bandari ya Dar es Salaam itakapokamilika, kama mradi huu hautojengwa maana yake Tanzania itapoteza mabilioni ya fedha, achilia mbali ajira zaidi ya 120,000, miundo mbinu ya kisasa zikiwepo barabara, huduma za maji na makazi, pamoja na biashara ambayo ingeimarisha mahusiano ya diplomasia ya uchumi baina ya Tanzania na mataifa washirika kibiashara.

‘kwa ujumla kutokujengwa kwa bandari ya Bagamoyo ni hasara kubwa kuliko kuijenga, ni vyema kufikia muafaka kwenye kuboresha masharti yaliyoko bila kongeza gharama ili pande zote kufaidika’, alisema Dokta Willium

Analolisema mchumi huyu, aliwahi kugusia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ambaye alisisitiza wakati huo kuwa serikali kuacha mradi wa Bagamoyo inafanya makosa makubwa kwa kuwa masharti yake yanayoonekana mabovu yanazungumzika. Sijui Serikali kunanini, lakini ukisikiliza yale mawasilisho yao (China Merchants Ports Limited, wawekezaji wa mradi), huwezi kuacha kuunga mkono ujenzi wa bandari ya Bagamoyo’, ni mradi mkubwa mno, si mradi wa kuacha jamani chonde chonde’, alisema Spika Ndugai akizungumzia moja ya ziara zake alizoenda China na kupata wasaa wa kukutana na wawekezaji hao.

Lakini bado kuna maswali mengi miongoni mwa raia juu ya masharti ya ”hovyo” ya mkataba wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. Hasa ni lile la umiliki wa ardhi kwa miaka 99 na zuio la mamlaka husika kukusanya kodi katika bandari hiyo kama ambavyo alikemea rais wa awamu ya tano.

Kwani moja ya eneo analosifiwa sana kufanikiwa Rais Magufuli ni kwenye eneo la madini alipoamua kuanzisha mazungumzo na mjadala mzito kuhusu Makinikia ya kampuni ya ACACIA inayomilikiwa na Barrick Gold, lakini pia faida na umiliki kwenye uchimbaji wa madini kwa faida ya nchi.

Ukinzani hauwezi kukosekana lakini kwa sasa hilo litakuwa rahisi zaidi iwapo patakuwa na uwazi na mtazamo mmoja kuhusu faida na hasara za mradi wa bandari hii itakayo gharimu zaidi ya dola bilioni 10 za kimarekani.

Muhimu zaidi mikataba ya aina hii, inayohusu miradi mikubwa na inayogusa maisha ya watu wengi ni vema ikawakwekwa wazi kila mtu akaisoma na kuifuatilia. Inapaswa kuwekwa kwenye tovuti za serikali ama kwenye maktaba za serikali, ili kupunguza na kuondoa mizozo na sintofahamu ya kueleweka. Ingawa ipo miradi inayopitia bungeni, lakini ni muhimu pia wananchi wenyewe wakaweza kuifikia