Sunday, November 24

Hizi ni tamaduni 6 tata na za kushangaza ‘zaidi’ duniani

d

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Jambo moja linalowatofautisha binadamu na ulimwengu wa wanyama ni tabia ya kukuza mila na desturi katika kila kitu kinachowazunguka kuanzia urembo wa kimila hadi tabia. Ni ukweli kuwa Ulimwengu umetajirishwa na maelfu ya tamaduni tofauti tangu mwanzo, kitu kimoja muhimu cha utamaduni wowote ni kanuni tiifu.

Kwa mujibu wa mtandao wa ncbi.nlm ulionukuu Price ‘Atlas of Ethnographic Societies, Kuna tamaduni zaidi ya 3800 duniani za kipekee ambazo zipo zilizozeleka na hazionekani kama za kushangaza lakini zipo ambazo ukizisikia zitakushangaza. Kwa jamii husika inayosimamia na kufuata tamaduni hizo inajivunia uwepo wa tamadunia wanazoziamini, wanaziheshimu, kuzithamini na kuziendeleza kutoka vizazi na vizazi.

Muhimu ni kwamba jamii duniani inatambua utofauti wa tamaduni na zinaheshimika bila kubeza, na hilo linafanya kuwepo kwa urahisi wa mtu yoyote kwenda kuishi na jamii nyingine bila kuwepo kwa mizozo ya kitamaduni, kwa sababu ya heshima na kutambua umuhimu wa tamaduni za watu wengine.

Pamoja na uwepo wa tamaduni nyingi, zipo za kushangaza zaidi ulimwenguni, miongoni mwa hizo ni hizi 6

6: Kuonyesha kitu kwa ishara ya midomo (lips)– Nicaragua

d

CHANZO CHA PICHA,VILLATAINA.COM

Kufanya vitendo kwa kutumia ishara ya mikono ni mila iliyozoeleka katika tamaduni mbalimbali. Watu wengi hutumia kidole hasa cha shahada kuonyesha kitu, Lakini huko nchini Nicaragua ni kawaida kabisa kwa raia kuonesha ishara kwa kutumia midomo (lips) badala ya kidole kama watu wengi walivyozoea duniani. Midomo inatumika kwa ishara ya kukubaliana kitu, kuonyesha kitu, ama njia ama kukupa ujumbe.. Kwa hivyo kwenye mazungumzo na watu wa utamaduni huu inakupasa ukodoleee macho na kufuatilia zaidi midomo yake kuweza kuelewa kuliko mikono.

Unaweza kujiuliza inakuaje mtu anatumia ishara ya midomo kuelekeza kitu? Huanza kwa kuuvuta mdomo ili kutengeneza sura yenye mdomo wa bata na kisha huanza kupeleka mdomo mbele au upande mmoja na mwingine kuonesha unachokusudia.

Ishara kwa mdomo hutumiwa katika mazungumzo kuashiria kitu kinachotokea karibu. Wenyewe wanaelewana vizuri na ni kitu kinachokutambulisha ukaribu wa kijamii kwa watu wa Nicaragua.

5: Kulala kifudifudi kama heshima – Nigeria

v

CHANZO CHA PICHA,JOSHUA OREKHIE

Maelezo ya picha,Kulala kifudifudi kama hivi kwa jamii ya wayoruba Nigeria ni ishara ya heshima mbele ya wakubwa zako

Kwa watu wa jamii ya Yoruba, kabila ambalo limechukua sehemu kubwa nchini Nigeria, mila ya kulala kama salamu inachukuliwa kwa uzito mkubwa hasa wakati wa kusalimia wazee ama watu wazima. Imezoeleka upigaji wa magoti kaa mila iliyo maarufu Afrika. Lakini kwa Yoruba, kijana kulala chini kabisa na kuweka uso chini ni ishara ya utii kwa wakubwa.

Vijana kutoka kabila la Yoruba hususani mabinti hupiga magoti wakati wa kusalimiana na kwa wanaume kwa kawaida hulala kifudifudi. Hii ni Ishara ya heshima na kwa wazee katika jamii. Utamaduni huo ndiyo unatofautisha Wayoruba na makabila mengine nchini Nigeria.

4: Salamu za mabusu – Ufaransa

a

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Umjue usimjue, kumpiga busu mtu unayekutana naye ni utamaduni wa salamu wa kawaida kabisa Ufaransa

Kupiga busu ni jambo kama la kawaida katika jamii nyingi hasa za Magharibi, lakini kupiga busu kila mtu na kwa idadi zaidi ya mara moja na kila wakati ni utamaduni uliozoeleka sana nchini Ufaransa.

Katika kila utamaduni kuna namna yake ya kusalimiana. Ufaransa ili uonekanae umethamini mtu na kumsabahi ni muhimu kumpiga busu, na unavyompiga busu mara nyingi zaidi ni kuonyesha thamani yake na namna unavyomuheshimu zaidi. Tamaduni za Amerika ya kusini hutumia kitendo cha kubusu wapendwa wao wa karibu na marafiki wapya kwenye shavu kama njia ya kusalimiana.

Lakini nchini Ufaransa utamaduni huo unaenda mbali zaidi, kama njia ya kutoa salamu ambapo kuna tofauti ya busu kati la wanaume na wanawake. Namna unavyomsubu mwanamke ama mwanaume kunatofautina. Pili, idadi ya busu zinazohitajika kukamilisha mabadiliko ya salamu hiyo na zaidi ya hayo ni kwamba Wafaransa wanatakiwa kusalimiana na kila mtu kwenye sherehe au mkusanyiko baada ya wageni kuwasili iwe wanawajua waliohudhuria au la.

Uiwa Ufaransa, jiandae kupigwa mabusu mengi na jitayarishe kupiga mabusu mengi, kwani ni utamaduni wa kawaida kabisa.

3: Kuwatemea mate mabibi harusi – Ugiriki

v

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Mabibi harusi nchini Ufaransa, hujiandaa kutemewa mate kama sehemu ya utamaduni maarufu katika baadhi ya maeneo

Hii mila ilipata umaarufu mwaka 2002 kupitia filamu ya ‘My big fat greek wedding’.

Kutemea mate katika tamaduni za Kigiriki ni namna ya mtu kukutakia heri na kusaidia kuondoa mikosi na mabaya. Leo, desturi hiyo imebadilika na kuwa kitendo cha ishara zaidi ambapo wageni hutamka kwa nguvu “ftou ftou ftou.” Na kutema mate.

Wagiriki hufanya hivyo katika matukio mengine ya pekee kama vile ubatizo ili kumtakia afya njema mtoto. Kutema mate kunaweza kufanywa pia kama hatua ya kutambua ushirikiana ili kuepusha maovu wakati wa mazungumzo ya kawaida.

2: Siku ya kupeana mimba – Urusi

as

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Katika hotuba yake ya Hali ya Taifa hilo ya mwaka 2006, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitaja janga la idadi ya watu kuwa ni tatizo la dharura zaidi linaloikabili Urusi na akatangaza jitihada za kuongeza kiwango cha idadi ya watu na kuongeza uzazi kwa Urusi, ikiwa ni pamoja na kutoa motisha ya pesa taslimu kwa familia ambazo zina zaidi ya mtoto mmoja, ili zihamasike kuongeza watoto.

Septemba 12 kila mwaka ni siku muhimu sana Urusi hasa eneo la Ulyanovsk, ambapo wanaipa heshima kama ‘siku ya kupeana mimba kwa raia wa Urusi. Utamaduni huu kawaida unazungumzia wenza kukupata muda maalumu wa faragha ya ndoa na uzazi kwa njia ya kipekee. Hivyo Serika ikaanzisha siku ya mapumziko kwa umma maalumu kwa ajili ya kuwapa wanandoa muda wa faragha kwa matumaini kwamba watashika mimba. Wazazi ambao watoto wao huzaliwa miezi tisa baadaye wanaweza hata kushinda zawadi kwa kusaidia kuwa mstari wa damu kuendelea damu ya Urusi. Watoto wanaozaliwa Septemba 12 hupata zawadi kutoka kwa Mamlaka.

Mnamo mwaka wa 2005, Gavana Sergey Ivanovich Morozov wa Ulyanovsk, eneo lililoko kilomita 800 Mashariki mwa Moscow, aliongeza kipengele cha kufurahisha kwa kampeni ya kitaifa kwa kutangaza Septemba 12 kama Siku ya Kupeana mimba na kuwapa wanandoa likizo ya kazi ili kupata fursa ya faragha kwa ajili ya kutengeneza kizazi kijacho.

Tuzo kuu ya 2007 lilikwenda kwa Irina na Andrei Kartuzov, ambao walipokea UAZ-Patriot, gari la kifahari huko Ulyanovsk. Washiriki wengine walizawadiwa kamera za video, TV, friji na mashine za kufulia. Urusi imeamua kutenga siku hiyo na zawadi zingine kama hamasa kutokana na viwango vya uzazi nchini humo kupungua pamoja uwiano usio sawa kati ya wanaume na wanawake na maisha mafupi ya wanaume wa Urusi yanaleta wasiwasi mkubwa kwa jamii.

1: Kubarizi kwenye makaburi – Denmark

c

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Makaburi ya ‘Assistens’ ni maarufu kwa mapumziko ya watu kubarizi wakiwa na wenza wao ama familia

Wakati makaburi ni sehemu ya kuogofya katika nchini nyingi, lakini Wadenmark wanaona inafaa kubadili makaburi yao kuwa maeneo ya kujumuika na kubarizi. Makaburi yao yamepambwa vizuri na hutembelewa na wengi wakati hali ya hewa inapoanza kuwa joto.

Sehemu ya makaburi ya Assistens Cemetery iliyopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Copenhagen ni mfano mzuri wa makaburi hayo ambapo kubarizi hapa utakuwa unashiriki pamoja na wadenmark wengi maarufu waliozikwa hapo akiwemo Christian Andersen.

Katika makaburi haya utakuwa watu wametandika virago vyao wamepumzika huku wakijisomea vitabu, kuangalia filamu kwenye simu na Kompyuta zao au kuzungumza tu huku wakila na kunywa viburudisho mbalimbali.