Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amemuamuru Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto kumsimamisha Kazi mara Moja Afisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii anayehusika na utoaji wa Kibali kwa ajili ya Uendeshaji wa Huduma za Watoto Yatima kwa kosa la kudharau Wito.
Mheshimiwa Hemed alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya Watoto Mayatima hapo katika Mtaa wa Jumbi Wilaya ya Kati na kutokukuta Afisa yeyote wa Idara hiyo katika eneo hilo licha ya kupewa taarifa ya ziara hiyo mapema asubuhi.
Alisema hicho ni kitendo cha dharau kilichoonyeshwa na Mtumishi huyo wa Idara ya Ustawi wa Jamii kwa vile hadi inamalizika ziara hiyo hakuna sababu zozote zilizowasilishwa kwa kutokuwepo kwake katika wito huo wa Mtendaji Mkuu huyo wa Shughuli za Serikali.
Alisema haiwezekani kuona kwamba bado baadhi ya Watu hasa Watumishi wa Umma wanaendelea kwenda katika mfumo wa mazoea wakati Taasisi, Jumuiya na hata baadhi ya Mashirika ya kiraia zimeshajitolea kusaidia nguvu katika uwezeshaji wa hifadhi ya Watoto walioondokewa na Wazazi wao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja kufuatilia suala la ucheleweshwaji wa upatikanaji wa Kibali kwa ajili ya Uendeshaji wa Huduma za Watoto Yatima katika Majengo hayo ya Jumbi la zima kipatikane mara Moja ili huduma hizo zianze kwa wakati.
Akizungumza na Wasimamizi wa Mradi wa Ujenzi huo mara baada ya kuutembelea Mheshimiwa Hemed alisema Watumishi watakaopewa jumuku la kuwahudumia Watoto Yatima lazima wawe makini na kuwa macho kwa kuwaepusha Watoto hao na wimbi la vitendo vya Udhalilishaji vinavyoleta sura mbaya katika Jamii.
Alisema Watoto Yatima wanahitaji matunzo mazuri na uangalizi mkubwa utakaowapa faraja ya kujihisi kama wenzao mfumo utakaohitaji kwenda sambamba na haki zao zote zinazowajibika kuzipata katika mazingira yao ya Kimaisha ya kila Siku.
Mheshimiwa Hemed alisisitiza umuhimu wa kuzingatia mazingira bora ya usafi ndani ya Majengo hayo ili Watoto wote waendelee kusihi kwa Amani, Afya na upendo mingoni mwao anWalezi wao.
Mapema Msimamizi wa Mrasi wa Ujenzi wa Majengo hayo kwa ajili ya makaazi ya Watoto Yatima Bwaana Mohammed Mansour alisema Makaazi hayo yatahudumia Watoto Yatima 15 wanawake Wanane na wanaume Saba wakiwa na Mlezi wao Mkuu atakayekuwa akiishi mahali hapo.
Bwana Mohammed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kasi ya Ujenzi wa Majengo hayo inaendelea vizuri kwa lile la Ghorofa Moja Nyumba ya Mwalimu, sehemu ya kushi Walezi Wawili, sehemu ya Jiko na mahali maalum pa kulia.
Alisema ujenzi huo umezingatia Zaidi suala la upatikanaji wa huduma Maji safi na salama zilizopelekea kuchimbwa kwa Kisiam maalum katika eneo hilo ili kuondoa usumbufu wa huduma hiyo muhimu kwa Jamii.
Naye kwa Upande wake Bibi Zainab Ali Kutoka Ubalozi wa Kuweit Nchini alisema Uongozi wa Kituo hicho umezingatia kwa kina Watu watakaoajiriwa katika Kazi hiyo tayari wana uzoefu wa kina katika huduma za Usimamizi wa Malezi kwa vile tayari wameshastaafu.
Bibi Zainab alisema ujenzi wa Mradi huo umetokana na Michango ya Wananchi mbali mbali wa Kuweit waiojiwekea utaratibu wa kusaidia Makundi ya Watu wakiwemo Watoto Yatima na hata Wazee wasiojiweza.
Ziara ya Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar katika kukagua Mradi huo wa Ujenzi wa Makaazi ya Watoto yatima katika Kijiji cha Jumbi imekuja baada ya kupata Taarifa ya Wasimamizi wa Kituo hicho kuzunguushwa katika upatikanaji wa Kibali cha Kuendesha Kituo hicho.