Sunday, November 24

Nchi za Bara la Afrika Kuhakikisha Zinafanya Biashara ya Pamoja Baada ya Kuelekeza Nguvu Nje ya Bara hilo Itaimarisha Uchumi na Kuleta Maendeleo

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika mkutano wa ufunguzi wa Maonesho ya Wafanyabiashara wa Nchi za Afrika, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, ulifanyika katika ukumbi wa ICC Arena Jijini Darbab Afrika Kusini
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia hutuba ya Ufunguzi wa Maonesho ya Biashara kwa Nchi za Afrika, wakati Rais wa Afrika Kusini Mhe Cyril Ramaphosa akihutubia mkutano huo wa ufunguzi (hayupo pichani) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa ICC Arena Jijini Durban Afrika Kusini.
WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban na (kushoto kwake) Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania Mhe.Exaud Kigahe wakifuatilia hutuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akihutubia katika mkutano wa Ufunguzi wa Maonesho ya Biashara kwa Nchi za Afrika uliofanyika katika ukumbi wa ICC Arena Jijini Durban Afrika Kusini, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa (kushoto kwa Rais) na (kulia kwa Rais) Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe.Olusegun Obasanjo, alipowasili katika jengo la Mikutano la Kimataifa la ICC Arena Jijini Durban Afrika Kusini, kuhudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Maonesho ya Biashara kwa Nchi za Afrika, akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja kwa nchi za Bara la Afrika kuhakikisha zinafanya biashara ya pamoja badala ya kuelekeza nguvu zaidi nje ya Bara hilo hatua ambayo itaimarisha uchumi na kuleta maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Maonyesho ya Biashara baina ya nchi za  Afrika, unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Inkosi Albert Luthuli, KwaZulu-Natal, Jijini Durban, nchini Afrika Kusini ambapo Rais Dk. Mwinyi amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ili kuweza kufikia azma iliyokusudiwa ni muhimu kutekeleza malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambapo katika utekelezaji wake alihimiza haja ya nchi wanachama wa (AfCFTA) kushirikiana katika kuzifanyia kazi changamoto zilizopo ambazo ni kikwazo kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji.

Alizitaja miongoni mwa changamoto zinazozifanya nchi za Afrika zishindwe kufanya biashara baina yao ikiwa ni pamoja na kuwa bado zina vikwazo vingi vinavyosababisha kiwango cha biashara kuwa ndogo baina yao ikiwa ni pamoja na ufinyu wa miundombinu kati ya nchi zenyewe, utatanishi uliopo kuhusu viwango vya ushuru, migongano ya sheria na uhaba wa bidhaa zinazozalishwa.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba lengo la Mkutano pamoja na Maonyesho hayo ya Biashara ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi za Afrika hivyo, kuna kila sababu ya kutiliwa mkazo na kufanyiwa kazi ipasavyo azma hiyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kiwango cha kufanya biashara baina ya nchi za Afrika bado ni kidogo mno na badala yake sehemu kubwa ya biashara inafanywa katika  nchi zilizoendelea zikiwemo za Ulaya na Marekani.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa washirika wa mkutano huo kutilia  mkazo na hatimae kuonesha njia bora za kukabiliana na hali hiyo.

Alisema kwamba ni wajibu wa nchi za Bara la Afrika kuhakikisha kwamba zinachukua hatua madhubuti ili kuweza kuondoa changamoto zilizopo.

Akitoa hotuba yake hiyo, katika uzinduzi wa Mkutano huo, Rais Dk. Mwinyi alizieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hali iliyopo hivi sasa ambayo bado nchi za Afrika zinaendelea kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hata zile ambazo zingeweza kuzalishwa na wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika nchi hizo.

Alisema kwamba Tanzania hivi sasa imeanzisha miradi mikubwa ya maendeleo inayohusu ujenzi wa miundombinu ya bandari na reli kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuweza kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.

Vile vile, Rais Dk. Mwinyi alibainisha utayari wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na vikwazo vyote ambavyo vinarejesha nyuma maendeleo ya biashara katika nchi za Afrika.

Alisema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshasaini Mkataba wa kuwa mwanachama wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kwa hivyo, itahakikisha inatekeleza malengo na mikakati iliyowekwa ili kuyafikia madhumuni yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kwa eneo hilo.

Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza viongozi na wananchi wa Afrika ya Kusini kwa makaribisho yao na ukarimu mkubwa waliouonesha kwa ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kwake yeye binafsi.

Sambamba na hayo, katika suala zima la Maonyesho ya Biashara, Rais Dk. Mwinyi  alisema kuwa maonyesho hayo yana umuhimu mkubwa katika kukuza maendeleo ya biashara Barani Afrika.

Nao Marais na viongozi kutoka nchi mbali mbali waliohudhuria Mkutano huo walipata fursa ya kueleza mikakati na juhudi zinazochukuliwa na nchi zao katika kuhakikisha suala zima la biashara Huria linapewa kipaumbele katika Bara la Afrika ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana huku wakieleza athari za UVIKO 19 zilivyorejesha nyuma hatua hiyo.

Nae Rais wa Afrika ya Kusini Cyril Ramaphosa ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo aliwakaribisha wageni wake wote aliowaalika huku akieleza mikakati ya nchi yake na kueleza utayari kwa nchi hiyo katika kutoa ushirikiano juu ya suala hilo.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.