Wednesday, October 30

IFRAJI yakabidhi jengo la skuli ya maziwa Ng’ombe Micheweni

NA ABDI SULEIMAN.

KUKABIDHIWA kwa banda moja lenye madarasa mawili ya kusomea wanafunzi wa skuli ya Msingi Mwiza Ngombe Wilaya ya Micheweni, kutoka kwa Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation, itapelekea kupunguza msongamano wa wanafunzi kutoka 85 hadi 65 kwa darasa moja.

Hayo yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Kombo Rashid Hilali, wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhiwa kwa banda moja lenye vyumba viwili vya kusomea lililogharimu Milioni 27.

Alisema licha ya skuli hiyo kuingia mikondo miwili asubuni na mchana, lakini wanafunzi darasani hukaa 85 hali inayopelekea kuwa ngumu kwa mwalimu wakati wa kufundisha na kupitia wanafunzi mmoja mmoja.

“Skuli yetu tuna madarasa 12 na wanafunzi 2118 wanaume ni 952 na wanawake 1169, lakini haipendezi kuona darasa moja lina wanafunzi 85 hili ndilo lililopelekea wezetu Ifraji kutusaidia kutujengea madarasa hayo”alisema.

Alifahamisha kuwa sasa wamepata makaazi mazuri kwani madarasa ni marefu na mapana, litamsaidia kwa kiasi kikubwa mwalimu kufikia malengo yake.

Kwa upande wake Mratib wa Taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said Abdalla, alisema ujenzi huo ulianza baada ya kuona video ya mwanafunzi wa darasa la tatu akiomba kusaidia madarasa katika skuli yao ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika skuli hiyo.

Alisema ujenzi wa mabanda hayo yatasaidia kuondosha tatizo la usumbufu wa wanafunzi katika skuli hiyo, pamoja na kupata nafasi nzuri ya kusoma.

“Hili banda moja lenye vyumba viwili vya kusomea limegharimu Milioni 27, mjenzi ni mwananchi mzalendo na ameweza kutumia fedha vizuri na kumalizika kwa wakati, ili wanafunzi wasome kwa bidii”alisema.

Kaimu Mratib wa Idara ya Mipango Sera kutoka WEMA Adam Kombo Nassor, alisema kukamilika kwa jengo litaweza kupunguza msongomano wa wanafunzi madarasani katika skuli hiyo.

Alisema changamoto za elimu zinagusa kila mtu, hivyo WEMA inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Ifraji Zanzibar Foundatio katika kusaidia huduma mbali mbali za jamii.

Hata hivyo aliwataka wadau mbali mbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia huduma mbali mbali za elimu, ikiwemo vikalio, ujenzi wa madarasa pamoja na kumaza kwa mabanda ambayo hayajamaliza.

MWISHO