Wednesday, January 1

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ampongeza Rais wa Zanzibar Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipokea zawadi ya Ngalawa kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Zanzibar kwa niaba ya UWT Mhe. Swahiba Kisasi katika mkutano ulioandaliwa na Jumuiya hiyo kwa ajili ya kumpongeza leo tarehe 20 Novemba 2021 katika Viwanja vya Maisara Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,wakati akihutubia katika mkutano wa Jumiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ulioandaliwa na Jumuiya hiyo kwa ajili ya kumpongeza leo tarehe 20 Novemba 2021 katika Viwanja vya Maisara Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika mkutano wa Jumiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ulioandaliwa na Jumuiya hiyo kwa ajili ya kumpongeza leo tarehe 20 Novemba 2021 katika Viwanja vya Maisara Zanzibar.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa na nzuri ya kuiletea maendeleo Zanzibar kupitia sekta mbali mbali.

Mama Samia ametoa pongezi hizo katika mkutano maalum ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kwa ajili ya kumpongeza Mwenyekiti huyo kwa juhudi zake za uongozi uliotukuka.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja ya uongozi wake , Dk. Mwinyi ameonyesha Dira kwa kupiga vita rushwa na ufisadi, hivyo akaahidi Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maslahi ya wananchi wote, huku akibainisha kuwa Tanzania bila rushwa inawezekana.

Alisema amani na usalama unaoshuhudiwa hivi sasa hapa nchini, ni zao la Serikali anayoiongoza na akatumia fursa hiyo kuwapongeza Wazanzibari kwa kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) na kueleza kuwa Serikali hiyo imeonyesha matumaini makubwa.

Mama Samia alisema amani inapotoweka Zanzibar  athari zake hufika hadi Tanzania Bara, hivyo akatoa wito wa kudumisha misingi ya amani iliopo.

Nae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alimpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiunga mkono na kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa katika uongozi wa Rais Samia Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo.

Sambamba na hayo alitoa pongezi kwa Watanzania kwa kuendelea kumuombea dua kwani mambo anayofanya Rais Samia ni makubwa sana.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza UWT kwa wazo  zuri walilokuja nalo na pia kushirikiana na Jumuiya zote za CCM kufanikisha jambo hilo kwa msingi kuwa ni lao wote.

 

Mapema uongozi wa UWT ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi kubwa anazozichukua katika uongozi wake sambamba na kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi hasa uchumi wa Buluu katika uongozi wake kama Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ilivyoelekeza

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar