Friday, November 1

MAKALA MAALUM , SIKU 16 ZA KUPINGA UDHALILISHAJIWA KIJINSIA.

NA MARYAM SALUM – PEMBA.

 

 

TUKIANGAZIA Siku 16 za Kimataifa za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya  kimataifa ya kupinga ukatili  dhidi ya wanawake na watoto, zinazoendelea kuangaziwa duniani kote, ni wazi kuwa udhalilishaji wa kijinsia bado ni changamoto kubwa kwa ulimwengu.

Udhalilishaji  wa kijinsia kwa wanawake na watoto Duniani  mbali na kutendeka kila siku lakini  una madhara makubwa kwa jinsia hiyo  jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya nchi.

Kampeni hii hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba  na kumalizika tarehe 10 Disemba ya kila mwaka kwa ajili ya kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake .

Siku hiyo ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1991 , ikiongozwa  na kituo  cha kimataifa cha Wanawake  tarehe 10 ilichaguliwa rasmi kuwa siku ya kilele cha maadhimisho haya ikiambatana na siku ya haki za binaadamu Duniani.

Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dunia imekuwa ikiazimisha siku hiyo kwa kukumbuka madhila wanayopitia akinamama na watoto katika maeneo yao na nchi zao.

TAKWIMU ZA UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA KWA WANAWAKE NA WATOTO -ZANZIBAR, AGOSTI 2021.

Jumla ya matukio 96 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Agosti, 2021, kulikuwa na waathirika 96 ambao waathirika Wanawake ni 9 (asilimia 9.4) na watoto ni 87 sawa na asilimia 90.6, miongoni mwao wasichana ni 69 (asilimia 79.3) na wavulana ni 18 (asilimia 20.7).

Pamoja na kadhia hii kubwa Umoja wa mataifa haujakaa kinya katika kuelekea siku ya kimataifa ya kupinga ukatili wa kijinsia katika maeneo yenye mizozo Duniani kote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antoni Guterres amewataka waokozi kuzingatia hali na mahitaji ya waathiriwa wa udhalilisha wakati wakiwa wanafanya kazi ya kuzuia na kumaliza kabisa janga hilo la udhalilishaji ambalo ni miongoni mwa makosa la jinai.

“Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni ugonjwa wa kimataifa unaoleta fedheha kubwa katika jamii zote duniani”, alisema .

 Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake maalumu kuhusu siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Guterres amesema ugonjwa huo ni kinyume cha maadili kwa wanawake na wasichana wote, na ni kikwazo kikubwa  kwa maendeleo jumuishi , yaliyo sawa na endelevu.

Katika msingi wake, ukatili dhidi ya wanawake na w atoto ni udhihirisho wa ukosefu mkubwa wa heshima, kushindwa kwa wanaume kutambua usawa wa asili na utu wa wanawake kwani ni suala la haki za msingi za binadamu.

Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesaini mikataba mbali mbali inayohusiana na kadhia hiyo ili kupinga udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Siku 16 za kuadhimisha juu ya kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto inayofanyika kila ifikapo Novemba 25 ya kila mwaka lengo ni kuongeza kampeni za kupinga udhalilishaji huo.

Siku hizo 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike huadhimishwa kwa kufanywa shuhuli mbali mbali ambazo hubeba ujumbe  tofauti zinazohusiana na mapambano dhidi ya mtoto wa kike.

 Hata hivyo katika kuadhimishwa kwa siku hiyo huandaliwa vipindi , makala, mbali mbali zinazobeba ujumbe wenye kuendana na dhamira kuu ya siku hiyo maalumu.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake TAMWA Ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said alieleza kuwa kama TAMWA wamekuwa wakiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili wa mtoto wa kike kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wakiwemo wamichezo na waandishi wa habari.

“Kama TAMWA tumekuwa tukiadhimisha siku hizo kwa kufanya shuhuli mbali mbali zikiwemo kuzindua ripoti na tafiti mbali mbali ambazo zimefanywa na TAMWA na waandishi wa habari”, alisema.

Alisema kuwa wanapoadhimisha siku 16 huandaa shuhuli mbali mbali kama vile kufanya maandamano mikutano pamoja na dokumentari zinazotengenezwa na waandishi wa habari kuona juhudi mbali mbali zilizofanywa na mwamko na muitikio wa watu katika kupinga ukatili wa mtoto wa kike.

Alifahamisha kuwa chimbuko la maadhimisho hayo linatokana na tamko la katibu mkuu wa umoja wa kimataifa wa awamu ya saba Kofi anan, la mwaka 2006 na kuyataka mataifa yote yatambue uwepo wa tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na mtoto wa kike.

“Hivyo tatizo hilo limeonekana kuwa ni zito na lina umuhimu wa kipekee na kuwepo na kipindi maalum cha kutafakari namna ya kufanya kampeni ya kupinga udhalilishaji wakijinsia hasa kwa watoto wa kike,”alieleza.

Alieleza kutokana na ukubwa wa tatizo hilo kama TAMWA wataendelea kutengeneza dokumentari ambazo waandishi watazitengeneza na kuhoji watu mbali mbali kuhusiana namna ya kuunga mkono juhudi za mapambano ya kupinga ukatili wa mtoto wa kike.

Hivyo aliitaka jamii ishirikiane kuona inasaidiana na vyombo vinavyoshulikia matukio hayo kwani kumeonekana kuendelezwa zaidi kwa vitendo hivyo kila siku zinaposonga mbele, licha ya hukumu,na dhabu nyengine zinazotolewa kwa washitakiwa.  

Nae mkuu wa idara jinsia na watoto Pemba  Mwanaisha Ali Massoud akielezea siku 16 za kupinga udhalilishaji Duniani alisema  huadhimishwa kila ifikapo Novemba 25 ya kila mwaka ikiwa na lengo makhususi juu ya kupinga udhalilishaji.

“Vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto nchini vimeonekana kushika kasi kutokana na visababishi mbali mbali, ambapo ni pamoja na umasikini,misimamo ya kidini,kukwepa majukumu ya malezi,hizo ni miongoni mwa vyanzo vinavyopelekea kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji na utekelezaji wa wanawake na watoto,”alieleza.

Alifahamisha kuwa kutoka na vyanzo hivyo vinapelekea watoto wengi kukosa haki zao za msingi, elimu,afya, upendo na huduma nyengine muhimu,hivyo kupelekea watoto kuathirika kisaikolojia, kimwili na hisia.

“Kuachana kwa baba na mama isiwe chanzo cha kuwatekeleza watoto, kwani migogoro yao ya ndoa isiwashirikishe watoto na kuwakosesha haki zao jambo ambalo hupelekea kutofikia ndoto zao walizotarajia kuzifikia, na badala yake familia kuwa karibu na watoto wao ili kupiga vita janga hilo,”alisema.

Alieleza kuwa mara nyingi migogoro ya kindoa baina ya mwanamke na mwanamme yakutofahamiana ndio inayopelekea kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.

Aidha alitoa wito kwa jamii kwamba watoto ni taifa la kesho wanahaki ya kutunzwa kupata upendo kuelimishwa na haki zote za msingi,hivyo jamii familia kuwa karibu kupiga vita tatizo la utekelezwaji wa watoto, ili jamii iwe katika hali ya usalama.

Kwa upande wake Ofisa jinsia Wilaya ya Micheweni Bizume Haji Zume alieleza kuwa suala la utekelezwaji wa watoto bado ni changamoto kwa jamii na Serikali kwa jumla.

“Sisi wanaharakati wa kupambana na vitendo vya udhalilishwaji wa watoto tunahakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na kuondokana na yale madhila yanayowafanya kutofikia malengo yao,”alieleza.

Akitoa sababu za kuwepo kwa udhalilishaji wa watoto zinachangiwa na wanaume pale inapotokezea mgogoro wa kindoa baina ya mama na baba.

“Endapo mtoto atatekelezwa zipo athari nyingi zinazoweza kumpata mtoto katika maisha yake, ikiwemo kukosa huduma muhimu, elimu, afya bora kwa wakati,kupelekea wizi, kujiingiza kwenye madawa ya kulevya, ajira za watoto,kutafuta haki kwa njia nyengine jambo ambalo linaweza kupelekea kujiingiza kwenye ukahaba,na tabia nyengine mbaya,”alisema.

Hivyo alitoa wito kwa jamii kwa walio kwenye ndoa na wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa kusoma elimu ya ndoa ili watakapoingia kwenye ndoa waweze kujua haki na wajibu kwa mwenza wake ili ndoa iwe endelevu  kwa maslahi ya  kizazi kilichopo na kijacho.

Nae mratibu wa jumuia ya Tumaini jipya(TUJIPE) Pemba Tatu Abdalla Mselem  alieleza kuwa siku 16 za kupinga udhalilishaji kwa wanawake na watoto inalengo la kuelimisha jamii zaidi juu ya kushirikiana pamoja katika kupambana na vitendo hivyo bila kuoneana aibu na muhali.

“Sisi wanaharakati tunapambana na changamoto nyingi tunapopambana na vitendo vya udhalilishaji kutokana na matukio hayo kuwa mengi na ya muda mrefu, lakini tutakwenda hatua kwa hatua wala hatukati tamaa, kwani tuna lengo tuhakikishe tumelifikia,” alieleza.

Alisema kuwa kutokana na changamoto nyingi wanazopitia katika kupambana na kupiga vita vitendo hivyo, kwao imekuwa kama fursa kwa hiyo wanataka kuitumia ili kuhakikisha wanaisaidia jamii.

Alieleza kuwa licha ya jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji, lakini bado rushwa ya pesa inazidi kucheza mikononi mwa baadhi viongozi waliopewa nyadhifa za kushuhulika na kesi hizo bila kuangalia athari zinazoweza kujitokeza.

Alisema kuwa zipo kesi nyingi ambazo tayari zilikuwa zimeshafikia hatua nzuri lakini kwa vile aliyefanya tukio ni mwenye uwezo basi kesi hile hufinywafinywa mwisho wa siku haki haitendeki kwa sababu tu familia ya mtoto aliyefanyiwa kitendo kibaya ni maskini, jambo ambalo linarejesha nyuma kufikia lengo.

Aidha kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo, alitoa wito kwa Serikali kwamba kuwepo kwa mabadiliko ya sheria moja tu ambayo itabeba kila kitu ili wale wanaofanya matendo hayo wasipate fursa za kuendeleza kuwadhalilisha watoto.

“Tunaendelea kuiomba Serikali kuwepo na mabadiliko ya sheria, sheria iwepo moja tu ambayo itabeba kila kitu, kwani sheria zilizopo ni nyingi hizo zinawafanya wahalifu waendeleze kwa sababu tu kuna sheria inamwangalia, pia kuwepo na sheria itakayombana mtu asiyetaka kutoa ushahidi hapo tunamini tutaweza kufikia lengo,” alisema.

Hivyo kila mdau anawajibu wa kuhakikisha anatowa ushirikiano pale anapohitajika ili kupinga mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa wanawakae na watoto  ili kwenda sambamba na kauli za kidunia juu ya suala hilo.

                              MWISHO.