Thursday, October 31

TUCHUKUE JUHUDI ZA MAKUSUDI KUYATUNZA MAZINGIRA – MHE.OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema pamoja na juhudi za Serikali katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira nchini, kunahitajika juhudi za pamoja ili kukabiliana na tishio kubwa la athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshmiwa Othman ameyasema hayo leo, Kiungoni, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ziara yake ya kimazingira, akitembelea na kukagua maeneo mbali mbali yaliyopatwa na athari za kimazingira zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akiongea na wananchi wa kijiji hicho, Mheshimiwa Othman amesema Serikali inaelewa na imeamua kushughulikia changamoto za mazingira, bali jambo la msingi ni mashirikiano ya wananchi wote katika kuyanusuru na kuyaendeleza.
Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa utunzaji wa mazingira bila kushurutishwa, ikiwemo kuepuka ukataji wa miti kiholela ili kuilinda ardhi chache ya visiwa vya Unguja na Pemba inayokabiliwa na tishio kubwa la ardhi yake kuvamiwa na maji ya bahari.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Bw. Sheha Mjaja Juma, ameeleza juhudi za dharura za kunusuru Bonde muhimu la Kilimo cha Mpunga la Tovuni-Kiungoni, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, linaloelekea kuvamiwa na maji ya bahari, ambazo zitahusisha ujenzi wa tuta kubwa la urefu wa takriban mita 450, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, ikiwemo Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji.
Akifafanua juu ya hatua hiyo Afisa Mkuu wa Kilimo cha Umwagiliaji kisiwani Pemba, Bw. Mbarouk Ali Mgau, amesema licha ya tishio hilo kubwa liliopelekea juhudi binafsi za takriban wakulima 150 kwa kujenga matuta madogo yasiyohimili athari zake, bonde hilo lina umuhimu wa pekee katika upatikanaji wa mbegu za zao la mpunga na mavuno mazuri yanayoleta tija kwa wananchi.
Katika hatua za awali za ziara hiyo Afisa Mdhamini wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Bw. Suleiman Mohamed Omar, ameeleza athari kubwa za uharibifu wa Mazingira katika Machimbo ya Mawe yaliopo Micheweni, ambayo yameshawahi kupelekea vifo vya takriban watu saba, yanayoendelea kuwa tishio la watu na makaazi.
Aidha Madaktari Dhamana wa Hospitali za Micheweni na Wete kisiwani Pemba, Dokta Zubeir Omar Zubeir na Dokta Said Mohamed, wameeleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao, zikiwemo za ukosefu wa raslimali, vitendeakazi na uhaba wa majengo ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi Salama Mbarouk ameeleza kupokea mapendekeo na haja ya kuandaa mbinu mbadala zikiwemo za kuwawezesha wananchi kiuchumi, kupitia mafunzo ya ujasiriamali ili kuwaepusha na uharibifu wa mazingira kwa kisingizio cha ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Othman aliyeambatana katika ziara hiyo na viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa, ambao ni pamoja na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Wakuu wa Wilaya za Wete na Micheweni, Bw. Hamad Omar Bakar na Bi.Mgeni Khatib Yahya, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak na Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bw. Ahmed Abubakar, amekagua na kusikiliza kero za wananchi mbali mbali katika Hospitali za Micheweni na Wete pamoja na Machimbo ya Mchanga ya Shumba Viamboni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.