Thursday, October 31

PECEO yawapa elimu vijana na wanawake juu ya suala zima za kudumisha amani nchini.

NA ABDI SULEIMAN.

AFISA Mdhamini Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ Pemba, Thabit Othman Abdalla, ameipongeza Jumuiya ya PECO kwa kubeba dhima ya kuelimisha jamii juu ya suala dhima za kudumisha amani nchini, kwa kuwatengeneza vijana na wanawake kuwa mabalozi wakubwa wa kuifikisha elimu hiyo kwa jamii.

Mdhamini huyo aliyaeleza hayo mjini Chake Chake, wakati alipokua akizungumza na vijana na wanawake, juu kuwajengea uwezo katika utatuzi wa migogoro na Uchafuzi wa amani, na ujenzi wa amani endelevu katika jamii kabla ya na baada ya uchaguzi.

Alisema iwapo Vijana na wanawake wataelewa ipasavyo elimu hiyo ya ujenzi wa amani na utatuzi wa migogoro, basi jamii iliyokuwa itaweza kubaki salama na kutokushawishika.

Alifahamisha kuwa Amani ni kitu kikubwa, ndio maana tunatakiwa kuendelea kutafuta miundombinu, misingi na mikakati yakiweza kuhakikisha tunaendelea kuienzi, kuidumisha na kuiwekea misingi  misingi imara ya kuilinda na kuweza kusimama.

“PECEO imebeba dhima ya kuimarisha amani katika nchi, kwa kuwatengeneza vijana na wanawake kusuluhisha migogoro itakapotokea katika jamii”alisema.

Aidha alisema jambo kubwa litakaloweza kusimamisha amani ni kuwa tayari kwa viongozi, katika kuwatumikia wananchi na kutelekeza kwa vitendo ahadi zao, pamoja na utekelezaji na utii wa sheria bila shuruti ndio jambo pekee litakalowezesha kuwa na amani katika jamii.

“Mambo mengi yanapoharibika katika jamii, nchi au duniani, ukitafuta sababu utagundua watu wachache wamepuuza miongozo, taratibu, sheria au kanuni zilizowekwa katika kulinda na kusimamia jambo hilo, tunaposimamia tulioyaandika na kuyaamini katika kutuongoza kama sheria, basi sote tutakua salama na jamii iliyobora kwa maendeleo”alisema.

Kwa upande wa Vitendo vya Udhalilishaji, alisema hatuwezi kusema tuna amani wakati tunawimbi la udhalilishaji wa kijinsi, vijana wengi wamejiingiza katika wimbi la madawa ya kulevya, huku kukiwa na Viongozi wala Rushwa, wahuhujumu uchumi na kurudusha nyuma juhudi za serikali.

Naye kaimu Mrajis wa NGOs Pemba Ashrak Hamad Ali, alisema Jumuiya ya PECEO ilifanya vizuri katika mradi wa kuhamasisha umiliki wa ardhi kwa wanawake shehia sita Mkoa wa Kusini na kuweza kupunguza migogoro kwa kuwapatia hati miliki za ardhi kwa wanawake.

Aidha alisema kuendelea kutokea kwa vitendo vya Udhalilishaji wa wanawake na Watoto nchini, kutapelekea kutokupatika kwa amani, sambamba na kujiingiza katika vitendo vya uvutaji wa dawa za kulevya.

Akitoa neno la shukurani, shekh Said Ahmad Mohamed alisema amani ndio kila kitu, kila mtu anahitaji amani zaid kuliko chakula wala kinywaji, amani unaihitaji muda wote na kuitafuta kwa gharama yoyote.

Katibu wa Jumuiya ya PECEO Juma Said Ali, alisema bila ya amani katika nchi hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana, huku akiwataka vijana kutambua kuwa wanamchango mkubwa katika suala la ujenzi wa amani.

Kwa upande wao vijana Sidi Omar Said, alisema vijana wanaumuhimu katika utunzaji wa amani katika familia na jamii zao zilizowazunguka na kuwa wasuluhushi mkubwa wa migogoro.

Amina Shaib Mohamed, alisema vijana ndio nguvu kazi katika jamii, hivyo aliwasihi vijana wenzao kuwa wazalendo wakubwa wa utunzaji wa amani na kuepusha vurugu na migogoro isiyo ya lazima.