Monday, November 25

YETA imewataka vijana kuepuka migogoro na udhalilishaji kipindi cha uchumaji wa zao la karafuu.

NA ABDI SULEIMAN.

JUMUIYA ya Kuwezesha Vipaji vya vijana Pemba(YETA), imewataka vijana kushiriki kikamilifu katika uchumaji wa zao la Karafuu, huku wakiepuka migogoro na udhalilishaji katika kipindi hiko, huku wakiendeleza suala zima la ulindaji wa Amani na Utulivu Nchini.

YETA imesema kuwa pindi cha Uchumaji wa zao la Karafuu migogoro mingi hujitokeza katika jamii, hali inayopelekea kutokea kwa masuala ya udhalilishaji na kuiweka amani katika kipindi kigumu.

Hayo yameelezwa na Msaidizi afisa mradi wa kujenga uelewa kwa vijana, katika kuzuia migogoro ya ukatili kipindi cha mavuno ya zao la karafuu Pemba Omar Abrahman Suleiman, wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Mgogoni Kifundi Wilaya ya Micheweni.

Alisema mradi huo umekusudiwa kuwafikia vijana katika ngazi za shehia, maskulini, wakulima wa zao la karafuu, wanafamilia na jamii kwa ujumla, vyombo vya sheria, taasisi za serikali na binfsi.

Omra alisema matarajio ni kupungua kwa vitendo vya udhalilishaji kwa wasichana na watoto katika kipindi cha mavuno ya karafuu, kupungua kwa migogoro ya kifamilia inayotokana na zao la karafuu, vijana kusaidia uhamasishaji wa amani ya jamii zao.

“Sote tunajua kipindi cha uchumaji wa zao la karafuu migogoro mingi, hutokea na kupelekea uvunjifu wa amani baina ya mtu na mtu, familia na familia jambo ambalo halifai kutokea”alisema.

Akiwasilisha mada ya kutoa uwelewa juu ya kujenga Amani ya Jamii kipindi cha mavuno ya zao la Karafuu Pemba, kwa wananchi wa Mgogoni Riziki Hamad Ali, alisema Amani ni muhimu sana kuitunza hasa katika zao la karafuu kwani vurugu na migogoro hujitokeza kwa jamii.

Aliwataka wananchi kutambua umuhimu wa kuendelea kutunza amani, kwa maslahi ya nchi na jamii kwa ujumla kwani bado zipo nchi zinahitaji kujifunza Tanzania kutokana na kuendelea kuitunza amani yao.

Alisema migogoro ni sababu kubwa ya kudumaa na kuviza kwa maendeleo yoyote, jamii inapokosa amani na utulivu migogoro na fujo hushika hatamu na jamii kuporomoka kila Nyanja na kudharaulika na kubezwa mbele ya jamii nyengine.

Hata hivyo alisema vijana wananafasi kubwa ya kuhakikisha katika nchi ya Tanzania kuelewa na kuchukua hatua za makusudia ili kulinda amani ya nchi kuanzia ngazi ya shehia, Wilaya na Taifa.

Naye Bakari Ali Abdalla Mkaazi wa Mgogoni Kifundi, alisema kilio kikubwa cha wananchi ni ZSCT kushindwa kutangaza daraja la wkanza la karafuu, ikizingatiwa sasa kipindi kirefu juwa limetoka kali, hali inayoweza kupelekea kutokea kwa mgogoro baina ya wakulima na shirika.

“Ili kuendelea kulinda Amani ni wazi ZSTC kutangaza daraja la kwanza la karafuu, msimu wa vuli sijuwi kama wakulima wataziuza karafuu zao kwa hali hiyo”alisema.

Amour Khamis Ali mkaazi wa Mgogoni Kifundi, liitaka Wizara ya Kilimo wakati wa kukodisha mashamba ya mikarafuu, kuhakikisha wanawape kipaombele wananchi wa shehia husika liliposhamba, ili waweze kukodi pamoja na karafuu kuuzwa katika shehia hiyo na sio kupelekwa sehemu nyengine.