Monday, November 25

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na Uongozi wa Maskani kaka Kisonge (CCM) Ikulu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Uongozi wa Maskani kaka Kisonge (CCM) mara baada ya mazungumzo na Uongozi huo alipokutana nao leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Uongozi wa Maskani kaka Kisonge (CCM) mara baada ya mazungumzo na Uongozi huo alipokutana nao leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.[Picha na Ikulu) 24/11/2021.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba iwapo bahari itatumika ipasavyo hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza dhana ya uchumi wa Buluu ambayo inahusisha matumizi endelevu ya bahari.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Maskani ya Kachorora, ambao ulifika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza vyema majukumu aliyopewa na wananchi ndani ya mwaka mmoja tokea apate wadhifa wa Urais sambamba na kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Nane imeamua kwa makusudi kutekeleza Dira ya Uchumi wa Buluu kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo pamoja na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Alieleza kwamba miongoni mwa sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika Dira hiyo ni sekta ya uvuvi ambao lengo kubwa ni kuhakikisha sekta hiyo inaimarishwa ili iweze kuleta tija kwa wavuvi wenyewe pamoja na nchi kwa ujumla ambapo serikali itahakikisha inawawekea mazingira mazuri wavuvi ikiwa ni pamoja na kuwapatia zana za kisasa na elimu inayohusiana na sekta hiyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba maendeleo makubwa yataendelea kupatikana Zanzibar iwapo amani, utulivu na ushirikiano vyote kwa pamoja vitaendelea kudumishwa huku akitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Maskani hiyo kwa kuthamini na kuzipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliunga mkono wazo la uongozi huo la kufufua mashindano ya ligi ya Muungano ambayo alisema yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza soka la Zanzibar.

Katika hatua hiyo, Rais Dk. Mwinyi alitilia mkazo na kueleza hatua za makusudi zinazendelea kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza kupitia Wizara husika katika  kuhakikisha ligi Kuu ya Zanzibar inapata udhamini ikiwa ni pamoja na kufanya harambee iliyokusanya fedha za kutosha kwa ajili ya kuiunga mkono ligi ya Zanzibar.

Mapema uongozi huo wa Maskani ya Kachorora yenye makaazi yao Jijini Zanzibar ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza vyema majukumu yake ambayo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake wananchi wameweza kufarajika na kuonesha matumaini yao makubwa waliyokuwa nayo kwa kiongozi huyo.

Uongozi huo, ulimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza zana na Dira ya Uchumi wa Buluu ambao walieleza  iwapo utatekelezwa ipasavyo mafanikio makubwa yatapatikana katika sekta ambali mbali zinazohusiana na uchumi huo ikiwemo sekta ya uvuvi.

Aidha, uongozi huo uleileza haja ya kuwepo kwa namna bora ya uvuvi ili kuweza kuhifadhi mazingira pamoja na kulinda viumbe vya bahari.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Maskani ya Kachorora ulieleza haja ya kufufuliwa kwa mashindano ya ligi ya Muungano ambapo walieleza kwamba mashindano hayo yanazisaidia timu za Zanzibar kuweza kushiriki katika ligi za Kimataifa sambamba na kuweza kupata kipato kwa timu shiriki.

Katika hatua nyengine, uongozi huo wa Maskani ya Kachorora umeahidi kuendelea kushirikiana na Rais Dk. Mwinyi sambamba na kuendelea kumuunga mkono katika uongozi wake uliotukuka kwani wameanza kuona mwanga wa matumaini ya Zanzibar kuzidi kupata maendeleo endelevu.

Imetayarishwa na kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.